Haikuwa rahisi kwa timu ya Simba SC kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika. Ni safari ya milima na mabonde lakini hatimaye Simba wamevuka na kuingia katika hatua ya robo fainali, na haikuwa safari ya usiku mmoja.

Kauli mbiu mahususi ya ‘Do or Die’ (kufa au kupona) kama viongozi wa Simba walivyoinadi kwa mashabiki wao ilitimia, maelfu ya wananchi hawakuamini kama Simba ingechomoza katika hatua ya nane bora pale kwenye Uwanja wa Taifa baada ya kuwafunga waliocheza fainali za Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana, timu ya AS Vita kwa magoli 2-1.

Kwa matokeo hayo, Simba imefuzu hatua ya robo fainali katika kundi ‘D’ baada ya kujikusanyia alama tisa, hivyo kuungana na Al Ahly iliyovuna alama 10.

Hebu fikiria, timu kadhaa miamba katika soka barani Afrika zimeshindwa kufikia hatua hii, timu zenye majina makubwa kama vile Asec Mimosas, Orlando Pirates na Ismaily SC. Hali hii inaleta tafsiri soka la Simba limeanza kuvuka mipaka.

Simba imeingia anga za timu nyingine mashuhuri Afrika kama TP Mazembe, Mamelodi Sundowns na hata Al Ahly. Kuna kila sababu za kuilinganisha timu ya Simba na klabu nyingine mashuhuri barani Afrika, na zaidi ya hapo, kuna kila sababu ya kuwapongeza viongozi wa timu ya Simba kutokana na mikakati yao thabiti hadi kufikia hatua hii ya mafanikio, hatua ya nane bora katika michuano migumu zaidi ya soka barani Afrika.

Tangu timu hiyo kuingia kwenye mfumo wa hisa imekuwa na mwelekeo mzuri katika kufanya mapinduzi ya soka nchini. Aidha, viongozi wake wamekuwa msitari wa mbele kuhakikisha wachezaji wanaishi katika mazingira mazuri, yaani kuwaweka katika kambi nzuri kwa ajili ya maandalizi, sambamba na kuhakikisha wachezaji wanalipwa stahiki zao kwa wakati.

Lakini kwa upande wangu, kati ya mambo yanayoniweka katika tafakuri nzito tangu Simba ifuzu hatua ya nane bora (robo fainali) ni mtiririko wa pongezi kwenda kwa mchezaji Clatos Chama. Ni kweli kwamba Meddie Kagere hakuwa nyota wa mchezo siku ile ya mechi kati ya AS Vita na Simba, safu ya ulinzi ya AS Vita ilimbana sana, mabeki visiki kina Yannick Bangala na Kazidi Kasangu walimbana ili kuhakikisha haleti madhara.

Ni dhahiri kwamba timu ya Simba imekuwa na wachezaji wengi wazuri waliokamilika karibu katika kila idara, lakini kazi kubwa imekuwa ikifanywa na Kagere uwanjani, kuanzia hatua za awali za mtoano katika michuano hii ya Klabu Bingwa Afrika hadi hatua ya makundi.

Kule Ulaya, hata kama Messi na Ronaldo ikitokea hawafungi magoli kwenye mechi ya fainali, bado wamekuwa wakibaki na sifa yao ya kuzitoa mbali timu zao, kwa kuzingatia mashindano wanayoshiriki kwa wakati husika.

Hebu kumbuka fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ile ya mwaka jana, mechi kati ya Liverpool dhidi ya miamba ya Hispania, Real Madrid katika Uwanja wa Olimpisyskiy, Kiev nchini Ukraine. Licha ya Ronaldo kutokufunga goli lolote bado ndiye aliyeonekana shujaa.

Chama apewe sifa zake kama shujaa wa mchezo, Haruna Niyonzima haliu kadhalika kwa kuingia kubadilisha mchezo kiasi cha kuifanya timu ishambulie zaidi.

1255 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!