Asikwambie mtu, hakuna timu isiyopenda kuitwa timu ya kimataifa, miaka ya hivi karibuni msemaji wa zamani wa Yanga, Jerry Muro, alikuwa akijigamba kuwa timu hiyo ni ya kimataifa kwa sababu wanapanda ndege na wanashindana na timu za nje ya Tanzania.

Bila kukinzana na kauli hii, timu nyingi zimekuwa katika mapambano makali ya kufanya vizuri katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ili ziweze kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Shirikisho barani Afrika ambalo ni la pili kwa ukubwa Afrika, kwa kuwa si rahisi timu kubeba ubingwa wa Ligi Kuu.

Mara baada ya kusubiri kwa hamu ratiba ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam, hatimaye wiki iliyopita ratiba hiyo iliweza kutolewa na wadhamini wa mashindano hayo ya FA, Kampuni ya Azam Media kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

 

Mara baada ya kutoka kwa ratiba hiyo, timu nyingi zimedhihirika kujipanga vizuri kuelekea hatua hiyo ya michuano. Kwa ujumla, ni timu zilizojizatiti vema kusaka tiketi ya kucheza mashindano ya kimataifa.

Katika ratiba hiyo timu zimepangwa kucheza kama ifuatavyo; Kagera Sugar dhidi ya Azam katika dimba la Kaitaba, mkoani Kagera na timu ya Alliance dhidi ya Yanga, mchezo utakaopigwa katika dimba la CCM Kirumba, Mwanza, wakati timu ya Lipuli ikipangwa kucheza dhidi ya Singida United kwenye dimba la Samora, Iringa.

Timu ya KMC itakaribishwa na African Lyon katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar e Salaam. Michezo ya timu hizi itafanyika kati ya Machi 28 hadi 31, 2019.

Aidha, ratiba hiyo ilitoa timu zinazoweza kukutana katika hatua ya nusu fainali ambapo mshindi kati ya mechi  namba 111, Alliance dhidi ya Yanga, mshindi katika mechi hiyo atakuwa ugenini kuchuana na mshindi wa mechi namba 114 – Lipuli dhidi ya Singida United.

 

Vilevile mshindi kati ya mechi namba 112, Kagera Sugar dhidi ya Azam, atakuwa nyumbani kumenyana na mshindi kati ya African Lyon dhidi ya KMC.

Fainali hizi kwa mwaka huu zimekuwa tofauti kidogo kutokana na timu za daraja la kwanza kuleta ushindani mkubwa katika mashindano haya. Timu hizo ni Namungo kutoka mkoani Lindi na Mashujaa ya Kigoma. Vilevile timu za KMC na Alliance zimeingia hatua ya nane bora licha ya kuwa timu ngeni katika Ligi Kuu.

Mashindano haya yalianza kwa kushirikisha timu 107, lakini mpaka sasa zimesalia timu nane ambazo ndizo zimeingia hatua hii ya nane bora, kwa maana ya robo fainali.

Mara baada ya ratiba hiyo kutangazwa, mwakilishi wa Kagera Sugar anasema: “Mechi ni ngumu lakini tumejipanga, tunatamani kufanya vizuri ili kubeba taji hili.”

 

Lakini mwakilishi wa KMC, Anuary Binde, anasema mechi yao dhidi ya African Lyon ni ngumu, ingawa wamekwisha kuchonga kabati la kuhifadhi kombe la michuano hiyo.

Festo Sanga, mwakilishi wa Singida United ambaye timu yake hiyo ilishika nafasi ya pili katika michuano ya fainali kama hizi mwaka jana nyuma ya Mtibwa Sugar, naye anasema: “Sisi tulikuwa tunatamani kukutana na Yanga lakini tutajipanga kupata ushindi pale Samora.”

 

Kwa sasa Mtibwa Sugar ndiye alikuwa bingwa mtetezi wa Kombe hili la FA, lakini alitolewa kwenye hatua ya kuingia robo fainali dhidi ya KMC katika Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Hali hii inaonyesha kuwa timu zote nane zilizoingia hatua hii (robo fainali) zinapambana katika kutafuta tiketi ya kuiwakilisha nchi.

Aidha, tangu kuanzishwa kwa michuano hii miaka minne iliyopita, hakuna timu ambayo imewahi kutwaa taji hili zaidi ya mara moja.

Tangu kuanzishwa kwa mashindano haya ya Kombe la Shirikisho la Azam miaka hiyo minne iliyopita, timu zilizofanikiwa kutwaa taji ni Yanga, Simba na Mtibwa Sugar. Aidha, timu mbili tu, Yanga na Azam, ndizo zimefika hatua ya robo fainali mara zote katika maisha ya mashindano haya.

Ikumbukwe kuwa Kombe la FA ndiyo mashindano pekee yanayozikutanisha timu za Ligi Kuu na zile za Ligi Daraja la Kwanza, na katika hatua hii ya robo fainali, timu hizo za daraja la kwanza zimekwisha kutolewa kwenye mashindano haya, lakini timu ya Mashujaa kutoka Kigoma iliwashangaza wadau wengi wa soka baada ya kuitoa timu ya Simba msimu huu katika hatua za awali.

Please follow and like us:
Pin Share