Copy+of+Hayati+Hashim+Mbita+(1)Wiki mbili tangu kufariki na kuzikwa kwa Brigedia Jenerali Hashim Idd Mbitta, gazeti la JAMHURI limeibuka na makala ya mwisho aliyofanya mpiganaji huyo na aliyekuwa mwandishi wa mwandamizi wa gazeti hili, EDMUND MIHALE.
 Katika mahojiano hayo yaliyofanyika Desemba 2013, Mhariri anakuletea neno kwa neno kwa wakati ule alipozungumza na gazeti hili akianzia kusema kazi ya ukombozi ya Bara la Afrika haikuwa rahisi, kwani ilihitaji moyo wa kujitoa, kutumia akili na nguvu zote na watu walijitoa na kufanikisha kwa kiwango ambacho ana wasiwasi iwapo vijana wa sasa wanaweza.


  Anasema viongozi wa nchi za Afrika akiwamo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, waliona kuwa baada ya baadhi ya nchi za Afrika kupata uhuru kamili, haipendezi kwani kuna nchi nyingine bado zilikuwa hazijapata uhuru.
 Anasema mwaka 1963 viongozi wa nchi zilizopata uhuru walikutana na kupitisha maazimio mawili makubwa. Kwanza ni kuanzisha umoja utakaosaidia nchi zilizosalia kupata uhuru na pili kuunda chombo kitakachosaidia ukombozi wa nchi ambazo bado ziko chini ya wakoloni. Mei 25, 1963 Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ulianzishwa na makao yake makuu yakawekwa Addis Ababa, Ethiopia.


  Brigedia Jenerali Mbitta anasema mkutano huo ulihudhuriwa huku baadhi ya nchi zikiwa zimepata uhuru na viongozi wa nyama vya wapigania uhuru.
Anawataja viongozi wa vyama vya wapigania uhuru kuwa ni Kenneth Kaunda wa Zambia, Holden Roberto wa Angola, Sam Nujoma wa Namibia, Dk. Agustino Netto (Angola), Dk. Kamuzu Banda (Malawi), Kaimu Rais wa ANC, Oliver Tambo, Katibu wa ANC, Alfred Nzo na Severino de Almeida Cabral wa Guinea Bissau.


“Hawa walialikwa kusikiliza. Hawakuwa na uwezo wa kuchangia katika mkutano, lakini ilipotakiwa kutoa ufafanuzi aliitwa mmoja mmoja na kueleza matatizo katika chama chake na kisha suala lake lipelekwe mbele ya kikao na kufanyiwa kazi,” anasema Brigedia Jenerali Mbitta.  
 Anasema baada ya kikao hicho ikaanzishwa kamati ya uongozi wa Afrika chini ya iliyokuwa OAU. Baada ya kuanzishwa kwa kamati hiyo ukatokea ushindani ni wapi ofisi za makao makuu ya kamati hiyo zikae, kwa kuwa kila rais alitaka ofisi hizo ziwe nchini mwake.
  Anasema ushindani huo ulikuwa ni kati ya Rais Kwame Nkrumah wa Ghana, Rais William Tubman wa Liberia na Rais Gamal Abdel Nasser wa Misri, Rais Modibo Keita wa Mali, Mfalme Haile Selassie wa Ethiopia na Rais Nnamdi Azikiwe wa Nigeria.
  Ushindani ulikuwa mkali kwani ikumbukwe kuwa wakati huo Misri ilikuwa imepiga hatua kubwa kiuchumi. Ilikuwa na rekodi kubwa iliyoteuliwa na Bunge la nchi hiyo kuhakikisha inatumika kulikomboa Bara la Afrika.


  “Ilifanya kazi kubwa mno kwa kupiga propaganda za kuwaondoa wakoloni kwa kuwaita ‘nguruwe weupe’ ‘mabeberu’, ‘mijibwa myeupe’, ilifanya kazi kila siku na ilikubalika kwa sehemu kubwa kwa kuwa ilikuwa na uwezo mkubwa ilisikika sehemu kubwa ya duniani.
 “Nkrumah naye wakati huo alikuwa na joto la ukombozi, alitaka kuhakikisha bara hili linakuwa huru, hivyo naye alikuwa mbele kutaka ofisi hizo ziwe kwake,” anasema Brigedia Jenerali Mbitta.
  Brigedia Jenerali Mbitta amesema uamuzi wa wapi yawe makao makuu yawe ulifikiwa kwa kupiga kura na Tanganyika ilipata bahati ya kuwa makao makuu ya kamati hiyo.


  Amesema pamoja na Tanganyika kutokuwa katika ushindani ilipata nafasi hiyo na Rais Julius Nyerere alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukombozi. Mwenyekiti wa Kamati alikuwa na nafasi kumteua katibu mtendaji bila kumshirikisha mtu mwingine na uamuzi wake ulikuwa wa mwisho.
 Anakumbuka Rais Nyerere alimteua Katibu Mtendaji wa kwanza Mtanzania, Sebastian Chale, na wa pili alikuwa Balozi George Magombe na katibu mtendaji wa mwisho hadi ofisi hizo zinafungwa Agosti 1994 alikuwa ni Hashim Mbitta.
 Tanganyika ilipata bahati hiyo kwa kuwa ilikuwa imeanza kuwakaribisha na kuwasaidia wapigania uhuru kutoka Congo, Zambia na Zimbabwe ambazo zilichagua kuweka kituo chao Tanganyika kurahisisha mapambano ya ukombozi wa nchi zao. Msumbiji pia walikuwa wamekusudia kuanzisha chama cha siasa kifanye kazi kutokea nchini Tanganyika.
 
Madhumuni ya Kamati    
Brigedia Jenerali Mbitta anasema kamati ilikuwa kuvisaidia vyama vya ukombozi kwa kuvisimamia katika mambo ya kidiplomasia, kiuchumi, kiufundi na kiutendaji chini ya mwavuli wa OAU.
“Ilifanya kazi ya kuvisaidia mambo ya kiufundi ikiwamo kufuatilia mwenendo wa vyama hivyo kimoja baada ya kingine. Kamati ilihusika kuangalia kila chama na kuvisaidia katika mahitaji ya kisasa, kiuchumi na kidiplomasia. Tulifanya hivyo kwa kupitia maazimio ya vyama hivyo anasema.
Anasema kamati hiyo ilitakiwa kupaza sauti na  kuomba vyama vingine kuvisaidia vyama hivyo  kutafuta ukombozi.
 
Wapigania uhuru kuja Tanganyika
Anasema kambi ya kwanza ilianzishwa mkoani Pwani katika mji wa Bagamoyo, ambako wapigania uhuru wa chama cha Frelimo kutoka Msumbiji waliwekwa katika eneo hilo.
 Viongozi kama akina Samwel Daniel Shafishuna Nujoma wa Namibia kutoka chama cha ukombozi cha SWAPO na Agustino Netto wa Angola wa chama cha MPLA walifungua kambi ya kongwa mkoani Dodoma.
Kambi hiyo ilizidi kupokea wapigania uhuru wengi kutoka katika vyama vya ANC cha Afrika Kusini, Frelimo (Msumbiji), MPLA (Angola) na ZANU cha Zimbabwe.


 Anasema kambi hiyo ilikuwa chini ya usimamizi na kuhudumiwa kiuongozi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wapigania uhuru hao hawakupata misaada kutoka Tanganyika tu, bali kutoka katika nchi mbalimbali za Mashariki ambazo zilisaidia kutoa misaada ya chakula mafunzo na silaha.
Nchi zilizosaidia wapigania uhuru ni Ujerumani Mashariki (wakati huo), Urusi na China. Nyingine kutoka Magharibi zilikuwa ni nchi za Scandinavia za Denmark, Norway na Sweden.


Wapigania uhuru walipata nafasi ya kwenda kujifunza mbinu mbalimbali za kivita na baada ya kumaliza walirudi Tanganyika na kuendeleza mapambano ya kudai uhuru.
Tanganyika ilipokea misaada hiyo na kuhifadhi na pia kuwahifadhi baada ya vyama hivyo kuulizwa ni wapi wanataka misaada hiyo ipelekwe wakijibu Tanganyika inaletwa kwetu nasi tunapokea hata walimu tuliwahifadhi sisi kwa uwangalifu mkubwa.
 
Mgawanyiko wa kambi
Baada ya kambi ya Kongwa kuzidiwa na wingi wa watu, wapigania uhuru kutoka Msumbiji walihama katika kambi ya Kongwa na kuhamia kambi ya Nachingwea ambako walifanya mazoezi ya kivita mpakani mwa Tanganyika na Msumbiji.
  “Mashambulizi ya ukombozi yalianzia Nachingwea na kuingia Msumbiji,” amesema Brigedia Jenerali Mbitta.
 
Usikose wiki ijayo upate mengi aliyonena Brigedia Jenerali Mbitta.

2747 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!