Kuna wakati huwa najiuliza, hivi ni kweli kwamba ngozi nyeusi ni alama ya laana au mkosi? Sipati jibu kwa kuwa wapo ambao wana ngozi nyeusi na hawakumbwi na laana hiyo, lakini pia huwa najiuliza, ni kweli kwamba kutawaliwa ni dalili ya kuwa wajinga?
  Napo pia jibu huwa ni hapana kwa kuwa ni sisi wachache tulioonja utumwa na bado tukadai uhuru kwa kutumia akili timamu tulizokuwa nazo.
  Huu ni waraka maalum ambao sina budi kuanza kwa kuomba radhi kwamba kuna mambo ambayo yanasigana na imani za kuaminishwa kuwa tuko sahihi katika mambo yetu, lakini ukweli ni kwamba ujinga ni mwingi kuliko akili chache ambazo zinatuongoza.
  Miaka ya mwanzo kabisa wakati nchi hii tumepata uhuru, tulikuwa na wasomi wachache sana, inawezekana hawakuzidi watu mia ambao walikuwa na uwezo wa kusema wamehitimu elimu ya chuo kikuu. Hao  watu wachache ndiyo waliopokea kijiti cha utawala wa mkoloni na kuifikisha nchi kuwa Jamhuri inayojitegemea.


  Kipindi hicho Watanganyika wengi tulikuwa wajinga, lakini siyo wapumbavu, tulianza elimu ya ngumbaru na kusisitiza elimu ya msingi kwa kila mtoto ili kwanza tuweze kupigana na adui ujinga.
 Tulitumia nguvu zetu kujenga shule nyingi za msingi na kisha sekondari na kumalizia na vyuo vikuu, lengo likiwa ni kufuta ujinga nchini na kuweza kupata wataalamu mbalimbali katika fani mbalimbali na na kuhitimisha dhana kamili ya kujitegemea pasi na kutawaliwa kielimu na waliosoma ambao ni wakoloni, na kutawaliwa huku ni pamoja na kuamuliwa mambo ya kujitegemea kuwa ya kutegemea.


  Duniani kuna mataifa mengi, ili taifa litambuliwe ni lazima liwe na mfumo wake wa kiutawala na kujitegemea, ni lazima liwe na mfumo wake wa siasa ambao kwa namna yoyote ndiyo unaoongoza taifa hilo, ni lazima liwe na sheria na taratibu zake za kiutawala ambazi zinalindwa kikatiba.
  Tanzania ni moja ya mataifa hapa duniani, ni Taifa ambalo lazima liwe na heshima miongoni mwa mataifa mengine, liwe na heshima ya kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa. Ili liweze kuwa na heshima ni lazima liweze kujitegemea kama mataifa mengine.
  Hizi wiki chache zilizopita Taifa letu limepata anguko kubwa la sarafu yetu, thamani ya dola imepanda kuliko wakati mwingine wowote katika uhai wake wa uhuru, hii imetokana na matumizi makubwa ya dola kuliko fedha yetu, kiuchumi ni kosa kubwa sana na inaweza ikasababisha umaskini mkali usiweza kuthibitika kwa urahisi.


  Kuna wakati tulipokuwa katika vita ya kuwakomboa Waganda tuliamua kwa pamoja kama Watanzania kwamba hali yetu kiuchumi imedorora kutokana na kutumia amana yetu ya fedha za kigeni kununulia silaha na vitu vingine, tuliamua kujifunga mkanda kuzalisha zaidi na kuuza nje kuliko kununua kutoka nje.
  Taifa letu kwa sasa na hakika linaweza likawa linaongoza duniani kwa kutegemea bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi. Kama taifa hatuzalishi zaidi ya kuagiza, kama taifa hatuna tena wasomi wa masuala ya uchumi kama wa wakati ule wa elimu kiduchu ya kidato cha sita na siyo PhD za leo. Huu ni ujinga lakini siyo upumbavu.


  Kama kwa elimu yangu hii ya ngumbaru, ambayo niliipata mwaka ule wa Azimio la Arusha, basi ningehimiza kufufua viwanda vyetu vya ndani ili kuacha kuagiza bidhaa kutoka nje, ningeongeza kodi maradufu kwa wale manguli wanaotulazimisha bidhaa zao zinunuliwe kisa zimetoka nje.
  Kwa elimu hii fake ya ngumbaru, ningeshauri kuwa wafanyabiashara wasitoke na fedha za kigeni badala yake wapeleke bidhaa kutoka ndani ili wauze na kuweza kununua bidhaa huko huko kwa fedha hizo hizo bila kubughudhi hazina yetu ya fedha za kigeni, fedha ambazo ni kigezo cha kukua kwa uchumi.  
  Ningerejea mfumo wa zamani, ili kurudisha heshima ya fedha yetu na kuimarisha uchumi, suala la fedha kiuchumi ningekuwa nalo bega kwa bega ili kuwezesha viwanda vya ndani visife na ningeimarisha biashara ya kuuza nje zaidi badala ya kununua nje zaidi.


  Haiwezekani tuagize nje matunda, mboga za majani, vipuri, kalamu, nguo, maziwa, nyama, samani, vyombo vya kupikia, matairi ya gari, karatasi, mafuta ya chakula, khanga, chumvi na kadhalika halafu tuseme viwanda vyetu havizalishi wakati tumevitengenezea mazingira ya kifo.
  Hili ni wazo langu la kipumbavu, naomba wenye akili mtafakari na mjue hatima yenu ikoje. Sitashaanga kwa mtindo huu siku moja shilingi milioni zikiwa na thamani ya dola moja.

Wasaalamu,
Mzee Zuzu
Kipatimo

1791 Total Views 2 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!