MuhongoWaliokuwa wafanyakazi wa mgodi wa Acacia Bulyanhulu, wamemuomba Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo awasaidie.

Zaidi ya wafanyakazi 1,375 wa Kampuni ya Acacia Bulyanhulu ya Shinyanga na Acacia North Mara mkoani Mara, wamehoji kiburi cha mwajiri kuwatimua kazi kwa uonevu, bila haki na kufuata utaratibu wa mkataba.

Sambamba na hilo wafanyakazi wanamlalamikia mwajiri kushindwa kutekeleza mkataba baada ya kukatisha ajira zao – kubwa ikiwa ni kupimwa afya na kuhudumiwa kwa wale wanaobainika kupata madhara yanayotokana na kazi za uchimbaji.

 Ukiacha madai hayo, baadhi ya wafanyakazi wanadai mwajiri amesitisha matibabu yao kinyume cha sheria ya fidia kwa wafanyakazi sura 263 ya mwaka 2002.

 Wameliambia JAMHURI kuwa mwajiri alichukua aliwaonea wafanyakazi waliokuwa viongozi wa Chama cha Wafanyakazi Migodini (Tamico).

Wanadai baadhi ya wafanyakazi walifukuzwa wakiwa mapumziko ya wiki, likizo ya mwaka au ugonjwa, huku wengine wakiwa kazini kwa utaratibu wa kawaida nao wakaondolewa.

 Wanasema kabla ya kufukuzwa kazi walizuiwa kuingia getini Novemba 14, 2007 ilhali ndani walikuwa na makabati yaliyohifadhi vitu vyao zikiwamo nyaraka muhimu.

 “Mwajiri hakutekeleza makubaliano siku ambayo aliamua kuvunja mkataba. Makubalino ni kwamba tunapoachishwa kazi, lazima tupimwe afya na anayegundulikuwa kuwa na matatizo basi hutibiwa, lakini imekuwa ni tofauti.

 “Kuna wafanyakazi ambao walikuwa wanatibiwa katika hospitali mbalimbali, lakini mwajiri amejiondoa kugharamia matibabu ya watu hao, ana maana gani? Anataka watu wafe?” anahoji Novatus Makene, aliyekuwa anayendesha mitambo ya kuchimba madini.

Pamoja na wafanyakazi hao kuhaha kutafuta haki zao, mwajiri ambaye ameitwa kwenye vyombo vya serikali, amekuwa akikubali kusitisha ajira na matibabu kwa baadhi ya wafanyakazi.

“Cha ajabu ni kwamba kwenye vikao hivyo hukubali kuendelea kutuhudumia au kupimwa afya zetu baada ya kukatisha ajira zetu kikatili, lakini akitoka kwenye vikao hatekelezi makubaliano,” anasema.

Haji Luge anasema, “Tumehangaika sana, lakini sijui kiburi cha mwajiri kinatoka wapi? Alikatisha matibabu, malazi na chakula na kunitekeleza katika mazingira mabaya.

“Mazingira hayo yanaashiria nia ya kutoa uhai wangu kwa kukusudia kwa kukatisha huduma za matibabu, malazi na chakula. Nimetelekezwa hapa Dar es Salaam tangu mwaka 2011, wakati yeye ndiye ndiye aliyenileta hapa Dar es Salaam kutoka Bulyanhulu.

 “Kwenye kikao chetu katika Wizara ya Kazi aliafiki kuwa majukumu ya kula, kulala pamoja na matibabu yatakuwa juu yake hadi nitakapopona au daktari wangu atakapoelekeza vinginevyo,” anasema.

 Anasema yeye na wizara wamekuwa wakimsihi kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria, “Bado mwajiri anakaidi huku akibeza barua za wizara akiziita ni za mapenzi. Sijui jeuri hii anaipata wapi.”

 Miongoni mwa barua hizo ni Novemba 20, 2008 yenye Kumb. HA.78/394/02/45 kutoka kwa Kamishna wa Kazi iliyomwagiza Meneja wa Mgodi kuwapa gharama za matibabu wafanyakazi walioachishwa kazi na matibabu yao kusitishwa.

 Barua nyingine ni yenye Kumb. Na. HA.78/394/02/51 ya Januari 26, 2009 ambayo iliagiza kuwalipa stahiki wafanyakazi kwa mujibu wa makubalino.

Luge anasema kwamba amepoteza mtoto wake Machi, 2013 na mke wake Septemba 26, 2014 kwa kushindwa kuwahudumia kutokana na hali mbaya ya maisha baada ya maradhi yaliyotokana na kazi za mwajiri, kutolipwa na kukatishwa matibabu.

 Mbali ya wafanyakazi hao waliotimuliwa, wengine walioko kazini wanadai ya kuwa mwekezaji, anaendelea kuwanyanyasa.

 Mmoja wa maofisa anayelalamikiwa ni Simon Kleb wa kitengo cha magari ambaye baada ya kulalamikiwa na wafanyakazi wengi amehamishiwa Bulyanhulu ambako pia anadaiwa kuwanyanyasa wafanyakazi.

 Mfanyakazi huyo ambaye kwa sasa ameombwa kutotajwa jina lake gazetini, anasema: “Tunamwomba Waziri wa Nishati na Madini na Waziri wa Kazi na Vijana, Waziri wa Katiba na Sheria watusaidie. Wajue kabisa huyo mwekezaji ni jipu.”

 Anasema Kleb amekuwa na tabia ya kuagiza bangi, “Na ikitokea unakataa anakufitini na anamtumia kibaraka wake akutimue kazi kwa matusi ya kudhalilisha.”

 Anasema ametoa taarifa kwa uongozi wa mgodi tangu Februari 4, 2016, lakini hajajibiwa. “Viongozi nendeni kwenye huo mgodi na kuhoji. Wametimuliwa zaidi ya wafanyakazi 20. Sio siri hili ni jipu la kutumbua kwa mkuki ili wazawa wapone,” anasema.

 Kwa upande wao, Kampuni ya Acacia imesema suala madai ya wafanyakazi hao kupimwa afya liliratibiwa na kuwa baadhi yao walianza kupatiwa vipimo katika zahanati ya Mgodi, Hospitali ya Wilaya ya Kahama na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Nector Pendaeli alitoa majibu kupitia ofisa mapokezi yakisema: “Majibu tumetoa kupitia magazeti ya The Guardian na The Citizen ya Machi 16, hayo ndiyo majibu yetu kwa sababu tumetoa kama taarifa kwa vyombo vya habari maana tuhuma zimekuwa nyingi na tumejibu kwa pamoja.”

Katika magazeti hayo, wametoa majibu ya juu juu wakisema habari hizo ni za uongo na kwamba wafanyakazi wanaolalamika wameondolewa kazini kwa mujibu wa sheria.

By Jamhuri