‘Bureau de Change’ zafungwa Dar

Vyombo vya dola vimefunga maduka kadhaa ya kubadilishia fedha (Bureau de Change) jijini Dar es Salaam, yanayohusishwa na utakatishaji na usafirishaji fedha zinazotokana na biashara ya dawa za kulevya.
Vyanzo vya habari vya uhakika vimelithibitishia JAMHURI kuwa tayari maduka matano yamefungwa kwenye operesheni hiyo inayohusisha Kikosi Kazi kinachoundwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Usalama wa Taifa.
Maduka ambayo yamefungwa yakihusishwa kwenye tuhuma hizo ni Highland Bureau de Change lililopo Mtaa wa Livingstone, Kariakoo; Assalaam Bureau de Change lililopo Mtaa wa Sikukuu, Kariakoo; Rangers Burea de Change lililopo Magomeni Mapipa; Nanai Bureau de Change lililopo jengo la IPS, Posta; na GM Bureau de Change lililopo Kinondoni.
“Bureau de Change hizi zinatuhumiwa kukusanyia pesa za kigeni na kuzituma nje ya nchi,” kimesema chanzo chetu.

Highland Bureau de Change
Upekuzi uliofanywa katika duka la Highland Bureau de Change ambalo mmiliki wake ni James Chacha, ulifanikisha kuzuiwa kwa milioni kadhaa za fedha za mataifa mbalimbali.
Nyaraka kadhaa zilizuiwa ikiwa ni pamoja na watuhumiwa wawili waliotajwa kwa majina ya Khamis Mselem (29), mkazi wa Mbagala Matitu, na Ramadhani Emmanuel (22), mkazi wa Kimara, Dar es Salaam.

Assalaam Bureau de Change
Uchunguzi unaonesha kuwa katika duka la Assalaam ambalo hapo awali ilikuwa ikiitwa Kingdom Bureau de Change, mmiliki wake ni Said Salum (a.k.a Said Obama). Kikosi kazi kiliweza kukamata Sh milioni 105. Uchunguzi unaonesha kuwa watuhumiwa watatu walikamatwa. Nao ni Rashid Othman (35), mkazi wa Magomeni Kagera; Khatib Idd Khatib (32), mkazi wa Kigamboni, Vijibweni; na Ally Bakari Khamisi (38), mkazi wa Buguruni Malapa.

GM 2007 Bureau de Change
Kwenye duka hili ambalo lipo Kinondoni Studio, mmiliki wake ni Gasper Mwakanyamale, ambaye anaishi Kitunda. Sh milioni 33 zilikamatwa.
Watuhumiwa watatu walikamatwa na kutambuliwa kuwa ni Andrew Mwanjisi (32), mkazi wa Kinondoni; Aman Lyimo (25) na Sudi Tweve (34), mkazi wa Kigamboni Kibugumo.

Rangers Bureau de Change
Miliki wa Rangers Bureau de Change ni Ibrahim Madega. Fedha zilizozuiwa wakati wa operesheni ni Sh milioni 45. Watuhumiwa waliokamatwa ni Rashid Shemkaluwe (35), mkazi wa Kimara Temboni; na Halima Mohamed (33), mkazi wa Tandika Transfoma.
 
Nanai Bureau de Change
Mmiliki wa Nanai Bureau de Change, Ali Khatibu Haji (Shikuba). Kwa sasa yupo mahabusu akikabiliwa na tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Serikali ya Marekani imeleta maombi maalumu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania apelekwe nchini humo kujibu mashitaka yanayomkabili ya kujihusisha na mtandao wa dawa za kulevya. Duka hilo lilikuwa likisimamiwa na mdogo wake anaitwaye Khamis Haji. Kwenye operesheni hiyo Sh milioni 156 zilikamatwa.
Mtuhumiwa aliyekamatwa na kuhojiwa ni Haji Mohamed (30), mkazi wa Mabibo Jeshini.
Mmoja wa maofisa wa Polisi aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa vile si msemaji wa Jeshi hilo, amesema watuhumiwa wako nje kwa dhamana wakati upelelezi ukiendelea.
Machi 4, mwaka huu, Rais John Magufuli aliitaka BoT na Wizara ya Fedha kuyamulika maduka ya kubadilishia fedha, akihofia baadhi ya maduka hayo kushiriki michezo michafu ya kuvunja sheria za nchi.
Rais alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la BoT Kanda ya Kusini – mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.
Alisema baadhi ya maduka hayo ya fedha yamekuwa yakishiriki utakatishaji fedha haramu na hata biashara ya dawa za kulevya.

Kunaswa kwa mapapa
Katika kukabiliana na biashara hii haramu, Rais Magufuli, ametoa maelekezo mahsusi kwa Jeshi la Polisi, Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kushirikiana na vyombo vingine vya dola kuhakikisha wanawakamata wote wanaojihusisha na biashara hiyo bila kujali umaarufu wa mhusika.
Kutokana na agizo hilo, tayari matajiri kadhaa wa biashara hiyo nchini na ambao wamekuwa wakiheshimiwa na hata kuogopwa kutokana na ukwasi wao, wameshatiwa mbaroni.
Hatua hiyo imesaidia kumesaidia kukamatwa kwa watuhumiwa wengine muhimu na hivyo kuwapo matumaini ya kudhoofisha upatikanaji na usambazaji dawa hizo.
Miongoni mwa waliokamatwa ni ‘watu wenye heshima’ katika jamii, huku wakionekana kuwa mstari wa mbele kuhudhuria ibada misikitini na makanisani, wakiwa pia ndio wafadhili wakuu wa shughuli mbalimbali za kijamii.
Miongoni mwa watu wanaotajwa kuwa vinara wa unga ni Lwitiko Samson Adam (Tikotiko),  Mwinyikambi Zuberi Seif (Kambi), Muharami Abdallah (Chonji), Ali (Shikuba), Mohamed Khariri, Ahmed Ameran Shebe, Emeka Nwachukwu, Doreen John, Fred William ‘Chonde’, Christina Naphtali, Moreen Lyumba, na Salma Omar.
Katika mapambano hayo, Jeshi la Polisi nchini limefanya uhamisho wa haraka wa askari wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, na ule wa Tanga ukitajwa kuwa ni mkakati wa kuvunja mtandao wa dawa za kulevya ndani ya jeshi hilo.
Asilimia kubwa ya ‘mapapa’ wa biashara hiyo wapo Dar es Salaam. Kinondoni, Magomeni na Mbezi Beach, yanatajwa kuwa ndio maeneo yanaongoza kwa kuwa wauza ‘unga’ wengi.