Kifo ni maendeleo kwa maana ya mabadiliko yanayomtoa mwanadamu kutoka katika hali moja hadi nyingine. 

Moja ya maana ya kifo ni kutengana kwa roho na mwili baada ya kuunganishwa kwa njia ya kupuliziwa roho katika mwili pale mimba inapofikisha arobaini ya tatu au siku mia na ishirini tangu ilipotungwa.

Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ameuelezea mchakato huu wa makuzi ya mimba katika Hadith kutoka kwa Swahaba Abuu Abdir-Rahmaan Abdillaah bin Mas-uud (Allaah Amridhie) ambaye amesema: “Ametusimulia Mjumbe wa Allaah (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ambaye ni meli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arobaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arobaini zijazo huwa ni donge la damu, kisha arobaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake). Na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; kuandika riziki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, na (ni) mtu muovu au mwema. Wallaahi! Naapa kwa Yule Ambaye hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa Peponi (Jannah) hadi ikawa baina yake na Pepo (Jannah) ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya amali za watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa Peponi (Jannah) akaingia Peponi (Jannah)”. (Hadith hii inapatikana katika vitabu cha Hadith za Mtume Muhammad viitwavyo Sahih Al-Bukhary na Sahih Muslim).

Tunafundishwa hapa kuwa kifo si kuangamia kwa Roho bali kutengana Roho na kiwiliwili chake kama tukio hilo linavyotokea kwa kila mmoja wetu pale anapolala. 

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 39 (Surat Az-Zumar), Aya ya 42 kuwa: “Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapokufa. Na zile zisizokufa wakati wa kulala kwake, huzishika zilizohukumiwa kufa, na huzirudisha nyingine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri.”

Kufa kwa Roho hapa ni kule kutengana na kiwiliwili chake ili kutimiza ule muda wa uhai na maisha ya mwanadamu duniani. Kila Nafsi (Roho) huonja mauti. Mwanadamu ana umauti wa aina mbili na uhai wa aina mbili. Kabla ya Roho kupulizwa katika mwili pale mimba inapotimiza siku mia na ishirini mwanadamu anahesabiwa kuwa katika hali ya umauti (umauti wa Kwanza).

Roho ikipulizwa anauanza uhai wa kwanza hadi pale anapoufikia umauti wa pili, tunaoujua sana, ili afikie uhai wa pili, wa mwisho na wa milele.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah), Aya ya 28 kuwa: “Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu, akakufufueni! Kisha atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?”

Kwa nini leo tunazungumzia kifo? Asubuhi ya Alhamisi ya Februari 13, 2020 ilishuhudia kutangulia kurudi kwa Mola wetu mlezi mmoja wa nguzo imara katika kushughulikia mambo ya Uislamu na Waislamu nchini Tanzania, Alhaj Iddi Mohamed Bin Simba Iddi wa Simba-Ndume maarufu Mzee Iddi Mohamed Simba.

Hadi anafariki dunia, marehemu mzee Iddi Simba, kwa upande wa Uislamu, alikuwa muasisi wa Jopo la Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania; Mshauri wa Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu katika mambo ya uchumi na maendeleo; Msuluhishi wa migogoro baina ya viongozi wa Kiislamu; Mshauri Maalumu wa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Bin Zubeir Bin Ally Mbwana; Mhisani wa mambo mbalimbali ya kidini na kijamii na Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania. 

Marehemu Alhaj Iddi Simba alizaliwa Oktoba 8, 1935 jijini Bujumbura, Burundi ambapo baba yake, mzee Simba Iddi Simba-Ndume, Mrufiji wa Muhoro, Rufiji, Mkoa wa Pwani, alikwenda kwa shughuli za kueneza dini akiwa mwalimu wa dini ya Kiislamu. Mzee Simba Iddi Simba-Ndume alihakikisha mwanawe huyu anarudi Tanganyika (Tanzania) na kupata elimu yake nchini, hivyo mwaka 1943 marehemu Iddi Simba alijiunga na Shule ya Msingi Mchikichini, jijini Dar es Salaam akitokea Shule ya Kiislamu ya Jaamiatu pale New Street (sasa Shule ya Msingi Lumumba iliyopo Mtaa wa Lumumba) kabla ya mwaka 1946 kujiunga na Shule ya Kati ya Kitchwele (sasa Uhuru), iliyopo Barabara ya Uhuru, jijini Dar es Salaam na hatimaye baada ya kufika darasa la kumi kujiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora.

Alipomaliza Tabora, marehemu Alhaj Iddi Simba alipata fursa ya kwenda Punjab, India kusomea Diploma ya Sayansi ya Kilimo na baadaye akiwa mtumishi wa serikali alibahatika kuchukua Shahada ya Sayansi katika Kilimo nchini Pakistan na Stashahada ya Uzamili katika Uchumi na Maendeleo nchini Ufaransa ambapo alisoma pia lugha ya Kifaransa.

Kwa upande wa kazi, amehudumu katika Tume ya Mipango akiwa msaidizi wa Mkurugenzi wa Tume (Mzungu); Benki ya Dunia; muasisi na Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ambayo kwa uimara wake haikutetereka pale Jumuiya ya Afrika Mashariki ilipovunjika mwaka 1977; Mkurugezi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika; mjumbe wa bodi za wakurugenzi za makampuni mbalimbali na hatimaye Mbunge wa Ilala; Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi ya CCM; Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri wa Viwanda na Biashara.

Mwaka 2008 ulipotokea mgogoro wa uongozi katika Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) uliosababisha kuondolewa kwa wajumbe wa Baraza la Ulamaa miongoni mwa Masheikh na Wanazuoni wakubwa wa Kiislamu nchini marehemu Alhaj Iddi Simba alifadhaishwa sana hasa akikumbuka juhudi zake na wenziwe za kuundwa Kamati ya Maendeleo ya Waislamu (Medco) ndani ya Bakwata na mipango mizuri waliyokuwa nayo na namna ilivyosambaratishwa kwa kuvunjwa kiajabu kabisa.

Kwa uchungu wa dini marehemu Alhaj Iddi Simba alikubali kuwa muasisi wa Jopo la Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania lililokusanya masheikh kutoka maeneo mbalimbali nchini wakiwemo wale waliondolewa Bakwata na wengine.

Kwa utaalamu wake wa usuluhishi wa migogoro na uzoefu wake wa utawala, marehemu Alhaj Iddi Simba alifanikiwa kumuunganisha tena marehemu Mufti Sheikh Issa Bin Shaaban Simba (Allaah Amrehemu) na masheikh aliowafukuza Bakwata na hatimaye marehemu Mufti Sheikh Issa Bin Shaaban Simba alikuwa mjumbe wa heshima katika Jopo la Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu akiwa pamoja na Kadhi Mkuu wa Tanzania, Mufti wa Zanzibar na Kadhi Mkuu wa Zanzibar.

Ni suluhu hii aliyoisimamia marehemu Alhaj Iddi Simba ndiyo ilirejesha uhusiano mwema na kuumaliza mgogoro baina ya masheikh kiasi cha marehemu Mufti Sheikh Issa Bin Shaaban Simba kuwateua tena kwa nafasi mbalimbali masheikh aliowatimua mwaka 2008. 

Marehemu Alhaj Iddi Simba alifanya juhudi kubwa kuwasuluhisha masheikh wa mji wa Tanga na hususan wale waliotokana na Taasisi ya Kiislamu ya Tamta baada ya kufariki dunia  kiongozi wao mkuu, marehemu Sheikh Mohamed Bin Ayyubu Bin Khamis Al-Kamadhy na ninakumbuka wakati mmoja, kwa lengo la kupata utulivu na umakini, aliweza kugharamia kikao cha suluhu cha masheikh hao kilichofanyika katika Hoteli ya East African Jacaranda Resort, nchini Kenya.

Ni marehemu Alhaj Iddi Simba aliyeanzisha vikao vya tafakuri tunduizi kwa masheikh wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania vilivyokuwa vinafanyika kwa kuzunguka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku akiwapa masheikh na wanazuoni hao ‘darsa’ maalumu juu ya ulimwengu na mifumo yake ya uendeshaji, maana ya nguvu za kidunia, Taasisi za Kimataifa – Bretton Woods Institutions – mifumo, uendeshaji wake na athari zake kwa maendeleo ya nchi changa na kadhalika.

Moja ya matunda ya mchakato huu wa tafakuri ni kuchapishwa kitabu ‘Je, Tumetafakari na Kujiuliza?” ambapo mada sita nyeti ikiwemo ‘uhusiano wa Waislamu na Wakristo nchini Tanzania’ na ‘Pengo kati ya Masheikh na Wasomi Waislamu wa Elimu-Mazingira’ zilijadiliwa. Kwa hakika Uislamu na Waislamu wa Tanzania wamempoteza msomi aliyejitolea kwa hali na mali kujenga daraja kati ya wasomi wa Dini (Masheikh) na Wasomi wa Elimu-Mazingira na ambaye ndoto yake wakati wote ilikuwa kujenga jamii bora ya Kiislamu yenye kutoa mchango stahiki kwa maendeleo ya Dini yao, jamii yao na nchi yao.

Allaah Mtukufu azikubali juhudi zake hizi, amsamehe makosa yake na amruzuku Pepo (Jannah) – Allaahumma Aaamiiin! Maneno yake ya mwisho kwetu yatabaki yakigonga akili na nyoyo zetu aliposema: “Hawa wana-Jopo (Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania) ni wenzangu na nitakutana nao Peponi (Jannah)”. Akaongeza: “Fanyeni juhudi, kwa hali yoyote ile, jopo lisife.” Tunamuomba Allaah Mtukufu akurehemu mja wake, Ewe Iddi Mohamed Simba…Ulikuwa Tumaini, Utabakia mfano, kwetu na kwa vizazi vijavyo. 

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Bakwata na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania. Simu: 0713603050/0754603050

By Jamhuri