Ndugu Rais, aliyekuwa Rais wa Kenya kwa takriban miaka 24, Rais Daniel arap Moi, naye sasa amepita! Wakati fulani nikiwa Nairobi nikaambiwa kuwa kufikiria tu kuwa Rais Daniel arap Moi anaweza kuugua au kufa, ulikuwa ni uhaini! Lakini sasa naye amepita. Kumbe ni kweli sisi ni wapitaji tu katika hii dunia. Ulimwenguni hapa si kwetu.

Moi amepita lakini Kenya inaendelea kama kawaida. Alizaliwa akaikuta Kenyatta naye amekwenda ameiacha Kenya. Nayakumbuka vema maneno ya Brutus katika kitabu cha Julius Kaizari kama kilivyotafsiriwa na Julius Kambarage Nyerere. Alisema: “Sijaja hapa kumlilia Kaizari, bali nimekuja hapa kumzika Kaizari.” Ni kawaida mtu akishakufa huzikwa pamoja na mema yake, bali mabaya yake huachwa yakielea na kupeperuka! Basi, na iwe hivyo kwa Julius Kaizari”. Na vivyo hivyo iwe kwa Daniel Arap Moi.

Maziko ya Daniel arap Moi yalikuwa makubwa kupindukia kiasi cha kuzisimamisha karibu shughuli zote nchini Kenya. Mikusanyiko ya watu ilikuwa mikubwa ikionekana kama milima iliyoungana. Mistari ya waandamanaji ikawa mirefu kiasi cha kushindwa kuiona mwisho wake. Gwaride lilirindima. Askari walivalia sare zilizowapendeza sana lakini bado walikuwa wanatisha kama nini. Jeneza lake lilifunikwa Bendera ya Taifa la Kenya kama sanda.

Nikayakumbuka yale maandiko katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu: “Ala, kumbe! Kila zama ina kitabu chake. Itanifaa nini mimi hata nikikusanya watu wengi kupindukia siku ya maziko yangu? Hata wakija viongozi mbalimbali wa dunia na maiti yangu ikafunikwa sanda ya bendera ya taifa itanisaidia nini huko niendako? Nitakuwa peke yangu. Safari hii haina wasindikizaji wala haihitaji nauli. Ala, kumbe! Nilikuja bila kitu na nitaondoka bila kitu. Haijalishi jeneza langu litakuwa na thamani kubwa kiasi gani, lakini litafukiwa chini.”

Baba, ungekuwapo, ni jua tu la Kenya ndilo ambalo halikubadili ratiba yake siku ya maziko ya Moi. Lilichomoza mashariki na kuzama magharibi siku aliyokufa na siku aliyozikwa sawa na siku aliyozaliwa! Hii maana yake ni kwamba Daniel arap Moi hakuwa ni kitu chochote cha tofauti na Wakenya wengine. Hata ukiwa rais unabaki na masikio yaleyale mawili, hayaongezeki. Hivi ndivyo ilivyo hata hapa kwetu na duniani kwa ujumla. Ni ushamba tu alionao mwanadamu akiwa mwenyekiti hata wa mtaa tu, diwani, mbunge au rais, kujiona sasa amekuwa mtu muhimu.

Maziko ya Daniel arap Moi yalihudhuriwa na marais wa nchi nyingi na viongozi wakuu na watu wengi maarufu wa dunia. Hata hivyo baadhi ya marais hawakuonekana mazikoni! Wanafunzi wa Yesu walimuuliza: “Jirani yangu ni nani?” Akawajibu kwa mfano ulioonyesha kuwa, jirani yako si kukaribiana tu kwa nyumba au mipaka ya nchi. Bali aliye na utayari wa kuwa pamoja nawe katika wakati wako mgumu kama wakati wa msiba.

Katika hali ya kawaida hakuna sababu yoyote inayoweza kumzuia mwanadamu wa kawaida kwenda kumzika jirani yake. Lakini nafsi ya mtu humsuta zaidi akiwa mazikoni. Wako wengi waliowahi kuanguka mazikoni si kwa sababu ya uzito wa msiba waliouendea, bali wakiyakumbuka maovu yao waliyowafanyia wanadamu wengine, yakiwamo mauaji. Waliposimama miguu yao ililegea nao wakaanguka.

Watanzania bado wanamkumbuka yule mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki kutoka Kenya aliyejiapiza jijini Arusha kuwa Mungu akiwapatia maisha wakaja kuwa watu wa maamuzi katika nchi yao, hawatashirikiana na baadhi ya viongozi aliowaita ‘madikteta wanaowaweka wapinzani wao jela.’

Mlinzi wa kweli wa mwanadamu ni matendo yake na Mwenyezi Mungu, siyo bunduki wala risasi. Walipomaliza kumzika Moi, askari walirudi walikotoka na silaha zao zote. Daniel arap Moi aliachwa peke yake.

Habari za kifo cha Robert Ouko, aliyekuwa waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Kenya zilitikisa katika maziko. Niliandika wakati ule kumuuliza marehemu swali lilelile wanafunzi wa vyuo vikuu vya Kenya walilokuwa wanamuuliza: “Who killed Robert Ouko?” (nani alimuua Robert Ouko?). Mpaka anazikwa majuzi, marehemu hakuwahi kutoa jibu. Sasa dunia inamjibia.

Yamewekwa hadharani majina ya wahusika wote ili Wakenya na dunia ione jinsi kifo cha Robert Ouko kilivyokuwa cha kinyama. Mpelelezi gwiji John Troon kutoka Shirika la Upelelezi la Uingereza ndiye aliyetaja, Got Alila. Akasema Robert Ouko alichukuliwa nyumbani kwake usiku na kusafirishwa hadi Ikulu alikopigwa risasi ya kichwa na kufa.

Lakini alipoelekea kumtaja mhusika mkuu, Rais Daniel arap Moi alimtimua John Troon atoke Kenya. Kesho yake ikaokotwa maiti yake ikiwa imeungua moto. Mikono yake ilikuwa imevunjwa. Pembeni yake kulikutwa dumu la mafuta na bastola wakitaka kuweka imani kwamba baada ya kujipiga risasi kichwani na kufa alijimwagia mafuta na kujichoma moto.

Baada ya Mo Dewji wetu kupatikana mchora katooni aliandika: “Nendeni mkawachukue waigizaji kutoka Holy Wood, sinema yenu imefeli!” Baba naye kwa kutupenda wanae alilihutubia taifa akasema: “Watanzania si wajinga sana. Hata kama watanyamaza, mioyo yao haiwezi kuwa ‘clear’” (safi).

Habari kuwa jasusi mwandamizi wa Marekani, Michael D’ Andrea wa CIA aliishi sana Tanzania zifanyiwe kazi haraka. Anaitwa ‘undertaker’, yaani mtayarishaji wa mazishi. Alianza kazi za ujasusi nje ya Marekani mwaka 1979 alipoteuliwa kuwa mwanadiplomasia katika Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam. D’Andrea amekuwa akiwafahamu vizuri baadhi ya wanasiasa wa Tanzania akiwa karibu na Watanzania kadhaa wenye ushawishi nchini. Waliofanya naye kazi wanasema kwamba yeye D’Andrea ndiye aliyeongoza msako wa Osama bin Laden nchini Pakistan. Akiwa Washington, ni yeye aliyeongoza mauaji ya bin Laden, aliyekuwa kiongozi wa Al Qaeda.

Kupatikana kwa habari hizi nchini mwetu kunazidisha hofu miongoni mwa wananchi wetu, kwani zinawasukuma kuanza kufikiri kuwa upo uwezekano kuwa yuko mtu ndani ya nchi yetu anayeondoa roho za Watanzania wenzetu. Hapa ndipo unakuja umuhimu mkubwa kwa viongozi wetu kutafuta ukweli wa jambo hili haraka ili kuwaondolea wananchi hofu ikiwa zitabainika kuwa si habari za kweli. Kukaa kimya viongozi wetu wajue kuwa kwa kazi zilizokwisha kufanywa na D’Andrea hapa kwetu na wao hawatabaki salama.

535 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!