“Nina karibia kustaafu na kutoka mjini nirudi kijijini nikaungane kimawazo na kivitendo na wananchi wenzangu kuikomboa Kata ya Kabilizi katika Jimbo la Muleba Kusini.’’

Hayo ni maneno ya Jackson Butoto, Mkurugenzi Masoko wa Chuo cha Lugha mbalimbali za Kimataifa kinachojulikana kama Ciros, alipiozungumza na JAMHURI jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.


Mbunge wa Jimbo la Muleba ni Profesa Anna Tibaijuka (CCM), ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.


“Nimebaini katika kata yangu hakuna uongozi bali kuna watawala wasiojua shida za wananchi kwa kuwa si wabunifu wa miradi ya kuwaingizia vijana kipato, wamewaacha maskini, ninataka kwenda kuwaunganisha vijana wenzangu kupitia vikundi vya ujasiriamali.


“Nitaanzisha vikundi vya fani mbalimbali  kama kufyatua tofali, kufungua mashamba madogo na makubwa, hivyo kupitia miradi hiyo watajipatia fedha za kujenga nyumba bora na kusomesha watoto wao.


“Kupitia miradi hiyo pia watakuwa na uwezo wakuchangia utekelezaji wa miradi maendeleo kuiwezesha kata yetu kupiga hatua ya maendeleo ya kiuchumi.


“Nimefanya mengi katika kata hiyo lakini bado sijafikia lengo langu la kuwafanya vijana wajitegmee, sasa nimeona nahitaji kukaa katika kata hiyo kwa mawazo na kimatendo,” anasema Butoto.


Anataja matatizo mengine yanayoikabilia Kata ya Kabalizi yenye vijiji vya Kiwera, Kabalizi Mkale na Kashanga huduma duni za barabara, umeme, afya, maji na elimu, licha ya kata hiyo kuwa maarufu kwa kilimo cha migomba, mihogo, viazi vitamu, kunde, uwele, karanga, njugu mawe, kahawa na mahindi.


“Tatizo la ubovuu wa barabara unasababisha wananchi kushindwa kusafirisha mazao yao kwenda sokoni. Wengi wanatumia usafiri wa baiskeli. Hali hii huwatufanya wakulima kuuza mazao kwa hasara, lakini kama barabara zingekuwa nzuri tungetumia gari na kufika sokoni kirahisi,” anasema.


Ukosefu wa huduma bora za kijamii katika Kata ya Kabilizi imesababisha kupanda kwa gharama za huduma na bidhaa mbalimbali, hivyo kuongeza ugumu wa maisha kkwa wananchi katani hapo.


Butoto anasema tayari ameaanza kuandaa utaratibu wa kuwakutanisha wananchi wasomi wazawa wa kata hiyo wanaoishi jijini Dar es Salaam ili kupeana mawazo ya kuchangia maendeleo ya kata hiyo.


Anaongeza kuwa amejiandaa pia kuanzisha shule ya katika Kata ya Kabilizi kama hatua ya kuchangia kuboresha elimu katani hapo.


“Kupitia Shirika langu la Butoto’s Education Fund na mwanasheria wetu tumenunua kiwanja katika Kijiji cha Kiwera ili tujenge shule ya watoto wadogo, duka la vitabu na duka la dawa kurahisisha upatikanaji wa dawa katani,” anasema Butoto.


Anasema anaamini kupitia miradi huo watazalisha ajira kwa vijana wa kata hiyo waliomaliza kidato cha nne kwa kuwapeleka katika kozi fupi ya ualimu waweze kufundisha katika shule hiyo.


‘Tutafundisha bure watoto yatima na wa mazingira magumu, wenye uwezo watachangia gharama za masomo katika shule hiyo,” anasema Butoto.

1030 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!