Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh ametoboa siri kwamba utendaji kazi wa ofisi yake umekuwa ukikwazwa na sheria za nchi.

Kwamba mgongano wa kisheria umekuwa ukisababisha baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi wanaotajwa katika ripoti zake kutofunguliwa mashitaka mahakamani.

 

Utouh ameeleza hayo jijini Mwanza hivi karibuni, wakati akijibu swali la mwandishi wa habari hizi aliyetaka kujua jinsi CAG huyo anavyojisikia pale ripoti yake ya ukaguzi inapotupiliwa mbali na DPP kisha watuhumiwa wa ufisadi kuachiwa huru.


Hata hivyo, Otouh amesema anaheshimu kila uamuzi unaotolewa na ofisi ya DPP kwa kuwa sheria za nchi ndizo zinazompa mamlaka hayo.


“Aah mimi kama CAG sheria za nchi zinanilazimu kupeleka ripoti yangu ya ukaguzi kwa DPP, TAKUKURU na sehemu nyingine. Suala la kwamba najisikiaje pale ripoti yangu inapotupwa, mimi naheshimu uamuzi wowote unaotolewa na ofisi hii ya DPP, hakuna jinsi maana ndivyo sheria zetu zilivyo,” amesema.


Kwa kawaida ofisi yake hutakiwa kuwasilisha ripoti zake za ukaguzi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na idara nyingine za kiintelejensia.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya nchini (TUGHE), Ali Kiwenge ameeleza kushangazwa na kitendo cha Serikali kuonekana kulegea katika kuiboresha ofisi ya CAG kiutendaji.


Ametahadharisha kuwa ofisi ya CAG inaweza kukosa ufanisi kama Serikali haitaiboresha ikiwa ni pamoja na kuongeza mishahara ya watumishi kuwaepushia mazingira ya kushawishika kupokea ‘kitu kidogo’ wanapokwenda kuwakagua viongozi wanaowazidi mishahara.


By Jamhuri