Siasa ni mchezo mchafu, kweli wana JAMHURI sasa naamini. Utata wa siasa hauna cha nchi kubwa wala ndogo, maana nchi kubwa kama Marekani au Uingereza zinaweza kuamua siasa, wakakaribia kugawanyika nusu kwa nusu. Uingereza walipopiga kura mara ya mwisho, walishindwa kuchagua chama kimoja kikae madarakani, kwa sababu wabunge waligawanyika.

Labour waliokuwa wamekamata serikali walipoteza na Conservative wakaunganisha nguvu na Liberal Democrats, wakatosheleza kilichokuwa kinatakiwa kikatiba. Hawa watu, chini ya Waziri Mkuu David Cameron, walikuwa na mambo mengi na ndoto kubwa, lakini bahati mbaya ni kwamba nyingine zinakanganya na kutaka kuivunja serikali ya mseto.

 

Hili akilikubali Cameron analikataa Naibu Waziri Mkuu, Nick Clegg; akilitaka Clegg basi Cameron haelewi, na hao wawili wakikubaliana, wanakataliwa na ama vigogo wa Conservative, au wabunge.

 

Moja ya mambo hayo ni hili la pombe au kilevi. Mimi ni mdau kwa sababu ni daktari wa wanadamu na najua athari ya pombe inapomzidi mwanadamu. Mwanzo walikubaliana kuweka vigezo kuzuia pombe kuuzwa kwa bei rahisi, kwa sababu watu wengi wanakunywa kupita kiasi, dawa ikawa ni kuongeza bei ya painti moja ili watu washindwe kununua.

 

Sheria za afya zinafuatwa sana hapa kwetu, hata chupa zao zimeelezwa kiasi cha juu anachotakiwa mwanamke au mwanamume kunywa, na tovuti ya wanaodhibiti unywaji inabandikwa kwenye chupa au kopo la kilauri chako. Siasa imebadilika na wale waliokuwa wamemuahidi waziri mkuu kumuunga mkono wamegeuka; kati ya wote ni mawaziri waandamizi, Theresa May wa Mambo ya Ndani na wengineo.

Waziri mkuu aliahidi kuweka bei ya chini ya kuuza pombe, lakini baada ya kugeukwa na washirika wake wa karibu, naye ameufyata. Katika kipindi cha maswali kwa waziri mkuu bungeni, aliishia kuzungumza kisiasa, akasisitiza kwamba atadhibiti vileo vinavyouzwa bei rahisi katika ‘supermarkets’ na maduka, lakini akakataa kuahidi kuweka bei ya chini.

 

Habari ni kwamba baada ya wale wanaomzunguka kuamua kuachana na mpango huo, naye mwenyewe anaona hataweza kwenda nao mwenyewe. Sasa Cameron anasema serikali bado inafanya tathmini ya matokeo ya mashauriano juu ya sera husika.

 

Imeshauriwa kwamba pombe isiuzwe chini ya pence (senti ya paundi) 45 (paundi moja ni shilingi 2,600). Madaktari tumekuwa tukimtumia Cameron na serikali yake ujumbe ili wawe wajasiri kutekeleza hicho walichoamua.

 

Uzuri wa kitu kama hiki ni kwamba kikianza hapa, haitachukua muda kusambaa dunia nzima, maana hakuna ubishi hawa ndiyo wakubwa. Kama kweli lojiki inaonesha kwamba bei ikipanda unywaji utapungua, basi ni kwamba itasaidia sana afya za watu wengi.


974 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!