Baada ya danadana ya muda mrefu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoendelea kukwamisha kumtangaza mgombea wao wa urais, sasa naamua kusema. Hii ni kwa sababu ni mwanachama wa kawaida na sina nafasi ndani ya vikao vya Kamati Kuu wala Halmashauri Kuu.
Nimeona hivi kwa sababu hata ikitengenezwa mizengwe na majungu ya kila namna, bila ya kumsimamisha Edward Lowassa au Bernard Membe kugombea urais, basi ieleweke wazi kwamba muungano wa Ukawa utashinda Uchaguzi Mkuu ujao, kwa sababu Watanzania wanataka mabadiliko.
Wapo watu wanasema, “Eti Lowassa anatumia pesa nyingi…” Kuna wanaodai “Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alimkataa” wakisema Ikulu pahali patakatifu wasipelekwe matajiri.” Kauli hii si ya kweli na yenye kukosa mashiko; hebu tumuogope Mungu.


Ukweli ni kuwa hakuna asiyetumia fedha katika harakati zake za kisiasa, katika chaguzi za serikali za mitaa hadi ngazi za juu, tusidanganyane, huo ndiyo ukweli wenyewe!
Nichukue nafasi hii kuwauliza ninyi ndugu zetu mliopewa ama kuwa na nafasi za uteuzi wa wagombea  ndani ya chama, hivi Mwalimu Julius Nyerere anafaa sana kipindi hiki cha uchaguzi? Hasa huu wa Oktoba? Hivi ni mabaya mangapi aliyakataa, lakini ninyi mnayakumbatia?      Niwaulize, je, hajakataa rushwa? Hajakataa ufisadi? Je, hayo hayapo hivi sasa? Mbona mnashindwa kuwawajibisha mafisadi na mnawaogopa?


Mbona pesa za Lowassa na za wengine msiowapenda mwaka 2010 zilikuwa nzuri na niwaulize kwani za sasa zina picha yake? Hivi nyinyi tukifanya upekuzi kila mtu aangaliwe vyema mali zake alizozitangaza wakati anapata madaraka, na tukiainisha alizo nazo sasa kuna atakayesalimika? Tena tukiuliza amezipataje?
Hebu msilitumie jina la Nyerere kwa kutimiza azma zenu tata! Hasa kwa wale wote wenye roho za kwanini, kwani wapo baadhi ya wanaojifanya wasafi na maadili tele walitoroka vikao vya Bunge kabla ya kufikia kikomo kwenda Nachingwea, huko siyo jimbo lao wala siyo wa kutoka mikoa ya Kusini. Mmoja mzee mzima na mwingine kijana, wote hawa wanautaka urais, ninawauliza kule mlikwenda kufuata nini? na Mlifanya nini? Kwa sababu ninakijua mlichokifanya na wote ni wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC).


 Na huyu kaka Membe naye anafanyiwa mizengwe, je, ana ‘mihela gani’? Au na yeye alikataliwa na Mwalimu Julius Nyerere? Kwani wapo watu walichukia pale aliposema kwa utani na masihara kuwa hakuna kosa kwa Tanzania kujiunga na OIC na fedha hata ikitoka kwa shetani tutazipokea! Kumpinga huko kwa nguvu hakuna mashiko kwani wapo watu wanatumia fedha za ajabu bila hata ya kujijua, watoto wa mjini wanaziita za ‘freemason’, na wengine wanafanya ushirikina wa hali ya juu, mfano kutumia viungo vya albino na mambo mengi ya kumchusha Mungu muumba!


Niwaombe hao wa vikao vya uamuzi watupatie wawili hawa niliowataja hapo mwanzo. Jamani hebu tupatieni tuanze kampeni maana mnatuchelewesha. Kwani mwaka huu hatutaki chaguo la Mungu, tunataka chaguo la watu na Mungu muumba athibitishe na kutia saini tu. Huu ndiyo mtazamo wangu na ninawatakia kila la heri, Mungu awabariki mtuteulie chaguo la watu.

0773-402133

2051 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!