Ushahidi wa kuambiwa ni nini?

Ushahidi wa kuambiwa ni ule unaotolewa na mtu ambaye hakuona tukio likitendeka, hakusikia tukio likitendeka, hakuhisi wala kuonja, wala kunusa jambo lililo mbele ya Mahakama kama kosa isipokuwa aliambiwa na mtu mwingine aliyeona, kusikia, kuhisi, kunusa au kuonja.
Hapa kuna watu wawili – kwanza aliyeona au kusikia na pili yule aliyeambiwa na huyu aliyeona au kusikia. Kwa hiyo, katika maana yetu huyu wa pili aliyeambiwa na wa kwanza aliyeona au kusikia, ndiye mwenye ushahidi wa kuambiwa.


Ni kwa maana hii tunasema huyu wa pili aliyeambiwa akienda kutoa ushahidi wake mahakamani utaitwa ushahidi wa kuambiwa.
Kwa mfano, A alimuona B akimuua C. Baada ya A baada ya kuona tukio lile akamwambia rafiki yake – D. Ina maana D hakuona lolote isipokuwa ameambiwa na rafiki yake – A aliyeona.


Kwa maana hii ushahidi wa D ni ushahidi wa kuambiwa. Ameambiwa na nani, ameambiwa na A aliyeona tukio. Hii ndiyo maana ya ushahidi wa kuambiwa. Kwa jina la kitaalamu ushahidi huu huitwa ‘hearsay evidence’. Na kwa jina jingine la mtaani huitwa “ushahidi wa nilimsikia akisema….”
Sababu nne kwanini ushahidi huu haukubaliki/
Sheria ya ushahidi kifungu cha 61 na 62 kinauweka ushahidi wa kuambiwa katika ushahidi wa maneno (oral evidence). Na kanuni za ushahidi wa maneno ni kuwa ili uweze kukubalika kama ushahidi sahihi, ni lazima kama swali ni nani aliyeona tukio likitendeka basi jibu awe nalo mtu aliyeona tukio likitendeka, na kama swali ni nani aliyesikia tukio likitendeka, basi jibu awe nalo aliyesikia tukio likitendeka, na kama swali ni nani aliyehisi au kuonja kitu fulani, basi jibu awe nalo  mwenyewe kabisa aliyehisi au kuonja kitu hicho. Na kama swali ni mtaalamu yupi alipima na kugundua kuwa jambo fulani lilisababishwa na kadha wa kadha, basi jibu awe nalo mtaalamu huyo huyo na si vinginevyo. Hii ndiyo kanuni inayoongoza ushahidi wote wa maneno (oral evidence).


Kwa hiyo, kwa kuwa ushahidi wa kuambiwa nao ni ushahidi wa maneno, lakini uliokosa sifa hii, basi mtu aliyesikia kutoka kwa mtu aliyeona ushahidi wake hauwezi kukubalika kwa kuwa atapingana na kanuni hii inayotaka mwenyewe kabisa aliyeona au kusikia kuwa ndiye awe shahidi. Hii ni sababu ya kwanza ya kutokubalika ushahidi wa kuambiwa au ushahidi ‘anilimsikia akisema. Pili, ushahidi wa kuambiwa hautolewi kwa kiapo. Kawaida shahidi hutakiwa kuapa mahakamani kabla ya kutoa ushahidi, na kiapo ndiyo kitu pekee ambacho huthibitisha kuwa mtu anachosema ni kweli na kweli tupu. Ikiwa mtu atatoa ushahidi bila kuapa basi ushahidi huo hauwezi kuitwa ‘kweli na kweli tupu’. Kwa mujibu wa sheria ya ushahidi, mtu anayetakiwa kuapa ni yule aliyeona tukio, kusikia, kuhisi, kuonja au kuthibitisha kitaaluma.


Huyu ndiye anayetakiwa kuapa. Kwa maana hii aliyeambiwa anaweza kutoa ushahidi lakini bila kuapa kwa sababu hairuhusiwi kwake kuapa. Na kama haapi basi ushahidi wake kuanzia hapo huwa sawa na bure, usio na maana yoyote hali kadhalika usiokubalika.
Pia haukubaliki kwa kuwa ni ushahidi ambao ni mwepesi kuharibiwa. Hii ni kwa sababu aliyeona au kusikia ni  tofauti na aliyeambiwa. Aliyeona au kusikia si rahisi kusahau alichokiona au kukisika, lakini aliyeambiwa ni rahisi kusahau chote alichoambiwa au sehemu yake au nukta kadhaa za alichoambiwa.
Hali hii ya kuwapo kwa uwezekano wa kusahau, huwa inamtoa nje mtu huyu aliyeambiwa kwa kuwa muda wowote anaweza kuharibu ushahidi kwa kusahau nukta kadhaa kwa kuongeza au kupunguza na hivyo kuathiri uhalisi.


Hii ni kawaida hata wewe ukitumwa ukampe maagizo mtu fulani hutatoa maagizo yaleyale na kwa maneno yaleyale kama aliyekuagiza alivyosema. Utaongeza au kupunguza.
Mwisho, ushahidi wa kuambiwa haukubaliki kwa kuwa ni ushahidi unaoacha kiu. Ushahidi mzuri ni ule unaomaliza kiu ya Mahakama na ya kila mtu. Hii ni kwa sababu ushahidi wa kuambiwa mpaka mtu aliyeambiwa anapomaliza kutoa ushahidi wake, bado kila mtu katika Mahakama hubaki akiwa na hamu ya kumuona au kumsikia aliyeona tukio kwa macho yake, na akamsimulia huyu aliyetoa ushahidi.


Kila mtu hubaki na swali la ‘sijui huyu jamaa aliyeshuhudia yuko wapi’. Hii ndiyo kiu inayobaki na kuufanya ushahidi huu kutojitosheleza.
Ni sawa na wewe uambiwe na mtu aitwaye Patrick kuwa alimsikia Aloys akisema alimuona Samuel akichoma moto nyumba yako. Bila shaka, utapenda zaidi kumuona Aloys ili akwambie kilichotokea kuliko Patrick anayekusimulia wakati hakuwapo.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, ndoa, kampuni tembelea sheriayakub.blogspot.com

 

3773 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!