Mila za Wazanaki: Mwitongo na Muhunda

Baada ya makala ya juma lililopita juu ya lugha ya Kizanaki, naendeleza makala inayofafanua mila na tamaduni za kabila la Wazanaki.
Eneo la Butiama linalojulikana kama “Mwitongo” linatokana na neno la Kizanaki lenye kumaanisha “mahame”, eneo ambalo lilikuwa na wakazi ambao walihamia sehemu nyingine.


Kwa desturi chanzo kikuu kilichosababisha watu kuhama eneo moja kilikuwa kifo cha mkuu wa kaya na kwa kawaida siku hizo mkuu wa kaya alikuwa ni mwanaume. Mke au wake wa marehemu walirithiwa na mrithi alihama nao na kuwapeleka kwake. Kwa kawaida ni wapwa wa kiume waliorithi mali ikiwa ni pamoja na mifugo. Katika kipindi kifupi tu na mara baada ya kuzikwa marehemu eneo lake lilibaki tupu.


Kwenye baadhi ya makabila kifo kilisababisha watu kuhama eneo kwa sababu ya woga uliojengeka katika mila za jamii hizo juu ya umauti na hivyo kulazimu kuhama eneo. Kwa Wazanaki ni suala la kurithi mali ya marehemu ndiyo lilisababisha eneo kuwa mahame; wale waliorithi walihamisha urithi wao kuupeleka kwenye makazi yao.
Kwa Butiama mahame (Mwitongo) yanayojulikana zaidi ni alipoishi na alipozikwa mwaka 1942 Mtemi Nyerere Burito, baba mzazi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ni pale tu ilipojengwa nyumba ya wageni katika eneo hilo kwenye miaka ya mwanzo ya sabini ndiyo watu walianza kurudi kuishi katika eneo hilo.


Katika jitihada za kugeuza eneo hilo la Mwitongo kuwa kivutio cha urithi wa kabila la Wazanaki wa eneo la Butiama, uongozi wa Kijiji cha Butiama ulijenga upya nyumba ya Mtemi Nyerere Burito pale pale ilipokuwa nyumba yake enzi hizo. Leo hii ni eneo ambalo linatembelewa na wageni wa ndani na wa nje na limeanza kujulikana kama kivutio cha utalii.


Kwenye miaka ya 1970 chama cha TANU kilipoamua kumjengea nyumba Mwalimu Nyerere alichagua ajengewe nyumba hiyo kwenye eneo la Mwitongo, jirani na nyumba ya baba yake. Baada ya Vita ya Kagera kumalizika mwaka 1979, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) liliamua kumjengea nyumba Amiri Jeshi Mkuu kama zawadi ya kuongoza vyema Tanzania katika vita hiyo na Mwalimu Nyerere alichagua eneo hilo hilo la Mwitongo kujengewa nyumba ambayo ilikamilika mwaka 1999.


Kwa namna fulani historia ya zamani imejirudia kwenye jengo hilo katika miaka ya karibuni. Mwaka 2008 nilikubali kushiriki kwenye programu ya vipindi vya redio na televisheni vilivyoandaliwa na Idhaa ya Kiswahili la Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) katika kuadhimisha miaka 30 vya Vita ya Kagera. Kwa upande wa Uganda walimshirikisha Jaffar Amin, mtoto wa kiume wa Idi Amin Dada, kiongozi wa kijeshi aliyeongoza vita dhidi ya Tanzania. Kilele cha vipindi hivyo vya redio na televisheni kilifanyika Mwitongo na kuhudhuriwa na Jaffar kwenye nyumba ambayo inabeba sehemu muhimu ya historia ya Tanzania.


Mwalimu Nyerere aliishi kwa siku 17 tu ndani ya nyumba hiyo kabla ya kwenda kwenye matibabu na kufariki dunia Oktoba 14, 1999. Alizikwa Mwitongo tarehe 23 Oktoba 1999.
Hali ya kubaki mahame kwa muda mrefu tangu mwaka 1942 kumefanya eneo la Mwitongo kuwa eneo la wanyama na viumbe mbalimbali, ikiwa ni pamoja na pimbi, tumbili, na nyoka. Mara moja moja hata nyani huonekana Mwitongo. Milio ya fisi nayo husikika mara moja moja.


Siyo jambo la ajabu kwa mkazi wa Butiama kuona nyoka, na wakati mwingine nyoka hupatikana hata ndani ya nyumba ingawa hii huwa ni nadra. Na hao nyoka wapo wa sampuli za kila aina, wengine wenye sumu kali za kuua binadamu.
Kwa mujibu wa mila na desturi za Wazanaki kila eneo la sehemu mbalimbali za Uzanaki huwa na mizimu inayolinda maeneo hayo. Muhunda ndiyo mzimu wa eneo la Wazanaki wa Butiama. Huaminika kuwa Muhunda huishi ndani ya msitu wenye jina hilo hilo uliyopo jirani na Mwitongo.


Anapoonekana nyani mkubwa, nyoka mkubwa, au chui inaaminika kuwa huyo ni Muhunda. Kwa kawaida, hao wanyama huachwa bila kudhuriwa na binadamu. Anapoonekana nyani mkubwa wazee wa kimila wanaojulikana kama abanyikura huchagua wawakilishi miongoni mwao ambao hutumwa kwa mpiga ramli ili ipigwe ramli kufafanua sababu ya kujitokeza huko. Napenda kuamini kuwa mpiga ramli wa aina hii siyo wale wa siku hizi wanaotumia viungo vya wanadamu katika kazi yao.


Wazee wanaporudi huingia ndani ya msitu wa Muhunda na kufanya matambiko halafu maisha yanaendelea kama kawaida.
Matumizi ya msitu wa Muhunda yanaambatana na masharti kadhaa. Mbali na abanyikura ni watu wachache wenye ruhusa ya kuingia kwenye msitu wa Muhunda.


Inaruhusiwa kusenya kuni ndani ya msitu ila ni yale matawi makavu ambayo yameanguka chini. Hairuhisiwi kukata miti wala matawi yake. Upo uzio wenye urefu mfupi unaozunguka eneo lote la ekari 15 la msitu wa Muhunda lakini, pamoja na kuwa uzio ule ni mfupi na mtu anaweza kuuruka kuuvuka, wazee wale wanapotaka kuingia humo hukata ule uzio ili kupata njia ya kupita; mila haziwaruhusu kuruka uzio. Usiulize kwa nini, mila nyingine hazina maelezo.


Baadhi ya wakazi wa Butiama wanazungumzia kisa cha chui aliyejitokeza kwenye eneo la Mwitongo ilipoanguka ndege vita ya JWTZ wakati wa Vita ya Kagera na akabaki kulinda eneo hilo mpaka wanajeshi walipofika na kuondoa mabaki ya hiyo ndege. Kwa watu walioshuhudia tukio lile kwao ilikuwa ishara kutoka kwa Muhunda kwamba Tanzania itashinda vita dhidi ya majeshi ya Idi Amin.
Hizi ndiyo simulizi zinazobainisha baadhi ya mila na tamaduni za Wazanaki wa Butiama.