Mwaka 2015 si mbali, na kwa mara nyingine tena Watanzania tutapata fursa ya kutumia haki yetu ya kikatiba kumchagua mtu mmoja, ambaye tunaamini kwamba ndiye atakayefaa kutuongoza kama Taifa, katika hiki kipindi kigumu cha uchumi kinachotuathiri kwa miaka zaidi ya 50 sasa.

Nimelenga zaidi kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani ni jambo lililo dhahiri kwamba iwapo upinzani utashinda kiti cha urais mwaka 2015, basi kwa kiasi kikubwa itatokana na kutumia vyema udhaifu na upungufu wa CCM. Vinginevyo CCM bado ina nafasi kubwa ya kurekebisha mambo kadhaa muhimu na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuendelea kutawala nchi mwaka 2015.


Hii ni kwa sababu CCM kama chama, imefanikiwa sana kuepuka siasa za ukabila katika ngazi ya urais tofauti na nchi kama Kenya ambako suala la ukabila ndiyo kigezo kikubwa, huku vigezo vingine vikija baadaye. Ni mafanikio ya CCM katika kudumisha amani, utulivu na umoja ndiyo yanayoilinda CCM nyakati hizi, hasa kwenye uchaguzi wa Rais. Bado kuna imani kubwa katika jamii kwamba ni sawa kwa upinzani kuchukua majimbo, lakini si ngazi ya urais.


Kama ilivyo ada, kampeni za urais huambatana na matangazo mbalimbali juu ya wasifu wa wagombea, ushindani wa hoja, na ushindani wa maneno (ambao mara nyingine huwa ni fitina). Kwa mtazamo wangu ambao nadhani pia unafanana na wa Watanzania wengine wengi, katika uchaguzi wa mwaka 2015 CCM itakuwa na aina kuu saba za wagombea ambazo nitazijadili kama ifuatavyo:


1. Kundi la kwanza ni lile linaloendesha siasa za kupambana na ufisadi ndani ya CCM.

 

2. Kundi la pili ni lile ambao tumeshuhudia kupitia vyombo vya habari likipigwa vita na kundi la kwanza kwamba ndilo linaloigharimu CCM kimvuto katika siasa za ushindani nyakati hizi.


Kundi hili kinara wake mkuu ni Edward Lowassa ingawa si lazima yeye kugombea moja kwa moja. Kundi hili litakuwa na mgombea angalau mmoja ingawa kama ilivyokuwa kwa kundi la kwanza, ni mapema bado kubaini nani hasa atasimamsishwa na kundi hili.

 

Kitu muhimu hapa pia ni kwamba kuna uwezekano mkubwa Lowassa akashinda vita dhidi yake ndani ya chama, kwani CCM kama chama imeshindwa kumalizia “the last mile” katika azma yake ya kummaliza Lowassa kisiasa na kuna hisia nyingi inayozidi kujengeka ndani ya jamii kwamba pengine kinachoendelea ni fitina na minyukano ya masilahi kuliko ukweli.

Jamii bado inasubiri ukweli juu ya hili, vinginevyo kwa sasa the verdict is equally divided.3. Kundi la tatu ni lile linalopambana kuhakikisha kwamba linampokea Rais wa sasa mwaka 2015. Kama ilivyokuwa kwa makundi mengine hapo juu, hapa pia ni mapema mno kuja na majina ya uhakika mbali ya kutaja yale yanayovumishwa na vyombo vya habari bila ushahidi wa maana.


4. Kundi la nne ni lile lenye msimamo na mtazamo wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Vinara wa kundi hili ni kina mzee Joseph Butiku, Jaji Joseph Warioba, Dk. Salim Ahmed Salim, Dk. Hassy Kitine, Ibrahim Kaduma, n.k. Kwa vile wazee wote hawa umri wao umeshakwenda, watamsimamisha mtu wao, lakini kama ilivyokuwa kwa makundi mengie hapo juu, ni mapema mno kuja na jina au majina ya watu hao.


5. Kundi la tano ni lile ambao litapendekezwa baada ya busara ya watu kama Mzee Benjamin Mkapa, Mzea Ali Hassan Mwinyi na Abdulrahaman Kinana kutumika katika kuokoa kuvunjika kwa chama. Ni vigumu kwa sasa kubaini ni kina nani ambao wanaweza kuteuliwa na ambao makundi yote yatakayokuwa yanahasimiana wakati huo yatajihisi yapo salama hivyo kumuunga mkono mgombea huyo.


6. Kundi la sita ni lile la wale walioshindwa kuingia katika tatu bora mwaka 2015. Tatu bora ya wakati ule – Profesa Mark Mwandosya na Dk. Salim tayari wana majina makubwa hivyo uwezo wa kujitegemea ikifananisha na wagombea wengine kama Frederick Sumaye na Dk. Abdallah Kigoda ambao ili kufanikiwa itakuwa ni muhimu kujenga a coalition.

 

7. Na kundi la mwisho ni lile litakalokuwa na mchanganyiko wa wagombea mbalimbali ambao hawatakuwa na uhusiano ya moja kwa moja na makundi mengine hapo juu na ambao hawajawahi kuwania nafasi ya urais. Wagombea hawa watajaribu bahati zao kutokana na nafasi zitakazojitokeza wakati huo, hasa kutokana na upepo wa kisiasa ndani ya CCM, lakini muhimu zaidi, kutokana na nguvu ya mgombea wa Chadema mwaka 2015.

 

Humu watakuwamo watu kama Dk. John Magufuli, mawaziri wengine waandamizi katika awamu hii na awamu iliyopita ambao hawajawahi kuwania nafasi hiyo, lakini pia kina mama na vijana iwapo itatokea CCM ikahitaji mgombea wa namna hiyo. Kundi hili linaweza kutumiwa na kundi la tano (rejea hapo juu) kama nia itakuwa ni kuzuia CCM isivunjike kutokana na minyukano ambayo ni dhahiri itajitokeza.


Mara nyingi, Watanzania wengi huwa na tabia ya kuchagua viongozi kwa misukumo mikuu mitatu:

1. Mazoea.

2. Mkumbo.

3. Hisia na mapenzi binafsi juu ya wagombea.


*Tukianza na mazoea; mara nyingi CCM imekuwa na utamaduni wa kumsimamisha mgombea ambaye chama (si lazima wanachama au mvuto wake kwa umma) kina amini ndiye anayefaa. Na mara nyingi mgombea wa namna hii hupitishwa na wananchi kwani wapigakura wengi, hasa wa vijijini huchagua CCM kutokana na mazoea.


* Tukija kwenye suala la mkumbo; Watanzania wengi hupigia kura mgombea urais kutokana na mkumbo; kwa mfano, kama upepo wa siasa ya wakati huo unapeperusha UJANA, basi mgombea mwenye haiba ya ujana atakuwa na nafasi kubwa ya kupigiwa kura; kama upepo wa siasa unapeperusha UWEZO WA KIFEDHA, basi wananchi wengi watampigia kura mgombea mwenye uwezo kwa imani kwamba huyo hatakuwa na tamaa ya kuponda mali ya umma; na kama upepo utakuwa unapeperusha bendera ya UADILIFU, basi mgombea mwadilifu atakuwa na nafasi kubwa, n.k.


Pamoja na haya yote, kutumia vigezo kama hivi – kijana, au mwenye uwezo kifedha au uadilifu haina maana ndiye atakuwa Rais bora kwani kuna vigezo vingine vingi na muhimu vya kutazama kama nia ni kupata Rais atakayetufaa.


* Na mwisho tukija kwenye suala la hisia na mapenzi binafsi juu ya mgombea; hili tumeliona sana katika siasa za nchi yetu. Ni kawaida Watanzania wengi kujenga hoja kwamba fulani ana mvuto na mwonekano wa kuwa rais, au ana uwezo wa kujenga hoja n.k, lakini mara nyingi wanaotoa hoja hizi ni wale ambao aidha, wanafanana na wagombea husika in terms of socio-economic class, au wanatoka kanda au kabila moja na mgombea, na kadhalika.


Kwa ufupi, hawajengi hoja zao kwa masilahi ya Taifa. Watu wa namna hii ugeuka kuwa wapambe wa wagombea husika, na kutokana na nguvu na ushawishi wao mkubwa katika jamii, wapambe hawa hufanikiwa kuaminisha umma, hasa ule jamii ambayo haifanani kabisa na class ya mgombea na wapambe wake.


Kazi hii ya wapambe hufanikiwa kwa urahisi hasa pale suala la mkumbo na mazoea linapojipenyeza pole pole miongoni mwa Watanzania (umma), hasa wale wenye uelewa mdogo juu ya masuala ya demokrasia na maendeleo. Ndiyo maana kati ya masuala haya ya mazoea, mkumbo na hisia/mapenzi binafsi, hili la tatu – yani hisia/mapenzi binafsi huwa ni overriding factor.


Je, katika nyakati za sasa, hasa tunapoelekea uchaguzi mkuu wa tano wa vyama vingi, vigezo hivi vitatu vitakuwa na nafasi gani katika kutupatia mgombea kupitia tiketi ya CCM?

 

Ni dhahiri kwamba mchakato huu unaotumika kuaminisha Watanzania kwamba fulani na fulani ndiyo wanaotufaa katika nafasi ya urais, (hasa ule wa hisia/mapenzi binafsi) si wa kuaminika (it is not a reliable process) katika kutupatia viongozi/rais bora. Ipo mifano mingi kuhusu jinsi gani mchakato huu umezaa viongozi wabovu katika Taifa letu.


Kwa mtazamo wangu ambao unaweza pengine ukawa finyu, mgombea wa kweli atapatikana iwapo vigezo vikuu vitatu vitatumika katika mchakato wa kumpata mgombea ndani ya CCM:


1. Wasifu (hulka) ya mgombea – ni muhimu wahusika wakatazama morality of the person, kwa mfano, je, ana any moral failings in the past? Je, amewahi kuwa involved in any unethical decisions na kuna ushahidi katika hilo? Ni muhimu sana all skeletons za mgombea zikawekwa hadharani ili umma uweze ku- scrutinize, na ikiwezekana, kazi hiyo ianze sasa. Lakini pia muhimu hapa ni kwa Watanzania kuelewa tofauti ya ukweli na fitina katika mchakato huu.


2. Msimamo wa mgombea kwa masuala mbalimbali – hili ni suala muhimu sana; kwa mfano, iwapo mgombea urais kupitia CCM mwaka 2015 alikuwa kambi moja na alisimamia msimamo sawa katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kijamii, na kisiasa, na wenzake ambao nyakati hizi wanaonekana hawafai mbele ya jamii, umma usiwaache hawa bila kuwadadisi kwa undani kwani kuna uwezekano mkubwa wakashindwa kufanya uamuzi mgumu kutokana na kuwindwa na dhambi ya asili.


Pia katika suala la msimamo on issues – msimamo wa mgombea ni muhimu uwe compatible with available evidence, not just fiction or theories – kwa mfano, msimamo na imani yake katika masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, over and above ilani ya CCM ambayo ipo to vague.


3. Na tatu ni – Uzoefu wa mgombea katika masuala ya uongozi. Uzoefu hapa si lazima iwe katika siasa, bali katika uongozi hata kama ni kwenye NGO au sekta binafsi; kikubwa ni awe na uzoefu wa kutosha na pia track record ya mafanikio katika uongozi wake; Katiba yetu ya sasa ya Tanzania inaeleza kwamba moja ya sifa ya mgombea urais ni lazima awe na sifa za kuwa mbunge; nadhani hii imepitwa na wakati na tuondokane nayo kwani kuna wabunge wa CCM ambao kwa miaka zaidi ya 20 wamekuwa bungeni wakifanya madudu ambayo yanashangaza hata watoto wadogo wa chekechea.


Nia yangu ni kupendekeza vigezo vya ku- scrutinize wale wote ambao wataweka nia ya kugombea urais kupitia CCM. Inawezekana vigezo hivi vikawa havitoshi, na ndiyo maana ya kuwa na mjadala ili tusaidiane kuboresha mjadala huu. Tukifanikisha hilo, nina hakika kwamba kwa pamoja tutaweza kutokomeza desturi ya kuchagua rais kwa njia za mkumbo, mazoea na hisia/mapenzi binafsi, vigezo ambavyo tayari vimeshatugharimu sana kama Taifa.

3215 Total Views 13 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!