2 Rais Kikwete akiongea na Viongozi wa CCM Mkoa Dsm Leo jijiniWatanzania, mabadiliko ni leo si kesho; mabadiliko ni wiki hii si wiki ijayo; ni mwezi huu si ujao, mabadiliko ni mwaka huu si mwakani.
Kesho hujaiona na hujui itakuaje, lakini uamuzi wako wa leo unaweza kuharibu kesho yako au unaweza kujenga kesho yako. Jenga leo yako vizuri ili kesho yako iwe nzuri.


Ninawahamasisha Watanzania wa kada zote — wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee — kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura. Mtanzania ni haki yako kujiandikisha, jiandikishe ili tukizike Chama Cha Mapinduzi (CCM), Oktoba, mwaka huu.
Mwaka huu ni mwaka wa kuwaondoa makaburu walioshindwa kuijenga Tanzania yetu. Mjadala huu ninaokwenda kuzungumza ni mtazamo binafsi. Nitashukuru kama mjadala huu utagonganisha fikra na mitazamo ya Watanzania wengi, binafsi ninaamini falsafa ya mgongano wa kifikra kwani inazaa mawazo mapya na ambayo hayakuwapo.


 Mwandishi wa Marekani, Anthony Tony Robbin, alipata kuandika, “Kila tatizo ni zawadi, bila matatizo tusingekuwa.” Kumbe matatizo ni fursa. Hata biashara yako inapoyumba usalalamike, hiyo ni fursa ya kufahamu ulikosea wapi na kujirekebisha.
Matatizo katika ndoa yako ni fursa ya kumpenda mwenzako. Si nia yangu kujadili masuala ya ndoa na uhusiano bali najenga hoja na kukukaribisha katika mjadala huu. Taifa letu kuja kuitwa Taifa linalojitegemea lilipitia mikikimikiki mbalimbali, wapo waliomwaga damu zao kwa ajili ya Taifa hili, wapo waliofia gerezani kwa ajili ya Taifa hili.


Ninawaombea kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, awajaalie pumziko la milele wapendwa wetu hawa ambao walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Taifa hili linatoka mikononi mwa wakoloni.
Naungana na gwiji wa fasihi Tanzania, Shaaban Robert, kuamini kwamba; “Watu wafao kwa ajili ya matendo bora kama vile kupigania uhuru wa taifa au wa ulimwengu, kusaidia watu wenye shida wanaodhulumiwa na kudhalilishwa, hufa kifo kitukufu.’’


  Siku moja rafiki yangu mmoja alinitembelea nyumbani. Alipofika tulizungumza mambo mengi, lakini alinikumbusha maneno ya busara ya mwanafalsafa na mpembuzi wa masuala ya kisiasa ndani ya muktadha wa demokrasia, Alex de Tocqueville [1805-1859].
Huyu ni Mfaransa aliyefanya utafiti juu ya siri ya mafanikio ya taifa la Marekani, alihitimisha utafiti wake kwa maneno yafuatayo, “America is great because she is good, if America ceases to be good America will cease to be great.’’
Kwa tafsri isiyo rasmi, anamaanisha hivi, “Marekani ni taifa kubwa kwa sababu lina maadili, litakapokoma kuwa na maadili, litakoma kuwa taifa kubwa.’’


 Maneno haya yalisisimua ufahamu wangu na kunifanya nitafakari mustakabali wa Tanzania kama taifa. Nukuu hii ilinifanya pia niyakumbuke maneno ya mpigania uhuru wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwalimu Nyerere katika dakika zake za lala salama alitamka maneno haya, “Najua ugonjwa huu sitapona, Watanzania watapata shida, lakini nitawaombea kwa Mungu.” Maneno haya ya Mwalimu yameonekana kutimia kwa muda mfupi tu tangu alipotutoka.
Kifo cha Mwalimu imekuwa fahari ya mashangingi, yaani ni taabu juu ya taabu. Watawala ambao ni viongozi wetu wanawatumia Watanzania kama daraja la kufanikisha mipango na malengo yao.


 Ni watoto tu wa watawala ndiyo wanaopata elimu stahiki, ndiyo wanaopenyeza katika sekta nyeti katika Taifa hili, ndiyo wanaopewa vipaumbele stahiki. Ni ukweli usiohitaji hoja ya kina kwamba misingi imara aliyoiacha Mwalimu imetoweshwa kutokana na viongozi dhaifu na walafi wa madaraka.
Taifa limegeuzwa kuwa taifa giza kwa Watanzania. Taifa limegeuzwa kuwa la kifisadi. Taifa limegeuzwa kuwa danguro la uovu. Mwalimu alihimiza kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi, afanye kazi, hakuhimiza kila mtu anayebahatika kupata uongozi awe fisadi na mroho.
Kaulimbiu inayotumiwa na viongozi wetu ni hii; ‘Nunua siasa, siasa ikununulie utajiri.’


 Kuna mtoto aliyetembelea familia moja. Alipofika alipikiwa nzi. Wanafamilia hao waliofanya jambo hilo baya walitaka kufuta historia hiyo kwenye kichwa cha mtoto. Walimuuliza, “Ukienda nyumbani utasemaje?’’ Mtoto alijibu, “Nitawaambia mlinipikia nzi.’’ Wakampa pipi. Wakamuuliza tena atakavyosema akifika nyumbani.  Akawajibu, “Nitawaambia walinipikia nzi na kunipa pipi.’’


Walioona hajasahau wakamnunulia nguo nzuri. Wakamuuliza tena atasema nini akienda nyumbani.  Alijibu. “Nitawaambia mlinipikia nzi, mlinipa pipi na mlininunulia nguo nzuri.” Mtoto huyu hakusahau ubaya aliotendewa na ile familia. Watanzania tumepikiwa nzi na chama tawala, hivyo hatuwezi kusahau ‘nzi’ hawa tuliopikiwa na CCM. Ukosefu wa ajira ni nzi ambao tumepikiwa na chama tawala.


Ukosefu wa elimu bora ni nzi ambao tumepikiwa na chama tawala. Rushwa katika Taifa hili ni nzi ambao tumepikiwa na chama tawala. Uongozi dhaifu katika Taifa hili ni nzi ambao tumepikiwa na chama tawala.
Ni kweli tuna matatizo mengi — kuanzia ukosefu wa ajira, elimu duni, kilimo duni, huduma duni za afya, miundombinu duni, ukosefu wa maji safi na salama kwa watu wetu, demokrasia changa, utawala dhaifu na kumomonyoka kwa maadili ndani ya viongozi wenye madaraka.
Ufike wakati sasa wasomi wetu, wanaharakati wetu na wanasiasa mbalimbali watafakari hatima ya vizazi vijavyo. Binafsi najiuliza mchango wenu wasomi uko wapi? Mchango wenu wanaharakati uko wapi? Mchango wa wanasiasa wetu uko wapi?


Wasomi wetu wanakimbilia kujiunga na chama tawala ambacho kwa kiasi kikubwa kimekwisha kuacha njia ya kuwapeleka wananchi kwenye nchi ya maziwa na asali, bali kinajenga tabaka la wakubwa na watwana, walionacho na wasionacho, watawala na watawaliwa na wenye haki na wasio na haki.


Balozi Juma Mwapachu amepata kuandika yafuatayo katika Jarida la ‘Change’, Vol.4 la 1996.  Balozi aliandika hivi, “Haipingiki kwamba Tanzania kwa sasa iko katika hali mbaya kiuchumi na kaulimbiu inayopaswa kutumika ni uokozi wa kiuchumi. Isipokuwa bila kuwa na mfumo wa kikatiba na kisheria ambao si tu unaokubalika kwa mapana bali pia unaoweka mwelekeo wa wazi wa Taifa –kijamii, kisiasa na kiuchumi. Tanzania inaweza isitatue na kukabili kwa mafanikio ya kuridhisha maadui wakubwa wa maendeleo, ambao ni umasikini, ujinga na maradhi.”
Sisi raia wa Tanzania, tunatamani tuendelee kuwa Taifa linaloongozwa na utu, umoja, heshima, uzalendo na maendeleo ya wote pasipo kuwa na ubaguzi wa kukusudia au kutokukusudia.


Mwanafalsafa George Gordon Byron [1788-1824] alipata kushauri hivi; “Tone moja la wino wa kalamu linaweza kuwafanya mamilioni ya watu kufikiri.” Muda umefika wa kufikiri tulipotoka, tulipo na tuendako. Muda umefika wa kuwachagua viongozi wa kuturudisha katika misingi ya utaifa wetu.
 Mshairi mmoja alipata kunena hivi; “Kwenye kila jamii, ipo kazi ya kufanya. Kwenye kila taifa, yapo majeraha ya kutibu.” Taifa letu lina majeraha ya kutibu. Tunadaiwa na Benki ya Dunia, hayo ni majeraha yanayohitaji kutibiwa. Kuna vifo vya akina mama wajawazito, hayo ni majeraha yanayohitaji kutibiwa. Kuna wazee waliopiginia Uhuru katika Taifa hili, lakini Serikali haiwakumbuki wala kuwatunza kwa malezi stahiki, hayo ni majeraha yanayohitaji kutibiwa.


Walimu wanadai madeni yao kwa Serikali na hawajalipwa hadi sasa, hayo ni majeraha yanayohitaji kutibiwa. Kuna migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, hayo ni majeraha yanayohitaji kutibiwa.
Chama tawala kimeshindwa kutatua laana hii, badala yake kimebaki kutumia nguvu kubwa ya dola kuwadhibiti wapinzani na wafanyabiashara wadogowadogo yaani machinga. Muda umefika wa kuwachagua viongozi wanaotengeneza kesho njema, wenye kesho nyingi tumeona udhaifu wao, tumeona ufedhuli wao.


 Mwalimu Nyerere aliwahi kuandika kwa uchungu maneno haya, “Uongozi mbovu ni kama mzoga, una tabia ya kukaribisha mafisi na mainzi. Tusidhani kwa hulka ya siasa ya watu wengine, kwamba sisi tunaweza kuvumilia uongozi mbovu na tusivune matunda ya hulka ya uongozi mbovu.” Mwalimu Nyerere hakuishia hapo, anasema pia, “Chama legelege, huzaa serikali legelege.”


Hivi sasa chama tawala na serikali yake, vyote ni legelege kiutendaji, kiuadilifu na kiuzalendo. Hivi sasa chama tawala kimepoteza dira na vipaumbele vya Taifa hili. Kipima joto cha Taifa letu hivi sasa ni kumpata kiongozi mwenye itikadi, mtazamo, falsafa kama za mwasisi wa Taifa hili, Mwalimu Nyerere.
Mwanahabari mkongwe, Jenerali  Ulimwengu, katika makala yake ya ‘Elimu ijenge taswira ya Taifa, utambulisho wa watu wake’’ katika gazeti la Raia Mwema toleo Na. 391 anasema, “Ningeulizwa leo ni taifa gani ningependa tujenge, ningejibu; taifa la watu wapenda haki; watu wanaopendana na wanaowapenda watu wengine; watu wanaojali usawa miongoni mwao na kutendeana mema; watu wanaotetea haki kwa uwezo wao wote; watu wanaopenda kusema ukweli wakati wote; watu jasiri, wasioogopa kutetea haki kwa kumhofu mtawala au mkwasi; watu walio tayari wakati wote kutetea haki za wanyonge na watu wasio na uwezo.”


Tunataka kiongozi anayeamini katika haki, usawa na uwajibikaji. Tunataka kiongozi atakayetumia sifa ya maji kuwaunganisha Watanzania. Sifa ya maji ni hii.  Maji ukiyaweka kwenye beseni yanachukua umbo la beseni. Maji ukiyaweka kwenye bakuli yanachukua umbo la bakuli. Maji ukiyaweka kwenye bilauli yanachukua umbo la bilauli. Maji ukiyaweka kwenye ndoo yanachukua umbo la ndoo. Kiongozi atayetuunganisha kwa njia hii, katika Taifa letu atakuwa amefuta viashiria vya  udini, ukabila na ukanda. Tunataka kiongozi atakayeenzi itikadi za Mwalim Nyerere.
Oooh! Mungu tusaidie tumpate kiongozi mwenye sifa hizi. Tunataka mabadiliko katika Taifa letu. Tunataka kiongozi mweye fikra mpya. Tunataka kiongozi mjasiriamali atakayewainua  Watanzania waliokata tamaa kwa sababu ya ugumu wa maisha.


Tunataka Tanzania yetu ifungue ukurasa mpya, ukurasa wa ajira kwa vijana wetu, ukurasa wa uongozi bora. Ukurasa wa kutumia vizuri rasilimali zetu. Ukurasa wa siasa bora. Ukurasa wa umoja wa Watanzania. Ukurasa wa undugu na ujamaa.
Ni ukweli kwamba Taifa letu liko njia panda, Taifa letu limepoteza dira na mwelekeo stahiki, tuliyodhamiria kuyaboresha kwa miaka 53 iliyopita hatujayafikia hata kwa nusu yake. Hii ni aibu kwa taifa kama la Tanzania ambalo  Mwenyezi Mungu amelijaalia rasilimali lukuki na wasomi lukuki.


Mwanaharakati Martin Luther King Jr alipata kusema hivi, “Maisha yetu yanaanza kufikia mwisho siku tunaponyamazia mambo muhimu.’’ Pengine ukimya wa Watanzania umechangia kwa watawala wetu kutumia rasilimali zetu hovyo. Hii ni tahadhari na pia ni fundisho kwetu Watanzania.
Kwa muda mrefu Watanzania tumenyamazia ufedhuli unaofanywa na Serikali ya CCM. Sasa ni wakati wa kusema imetosha. Ni wakati wa kuamini kwamba hata nje ya CCM kuna maendeleo na mabadiliko makubwa na ya kutisha. Ni wakati wa kutambua kwamba Tanzania siyo CCM, Tanzania ni Watanzania.


Askofu Mkuu Fulton J. Sheen alipata kuwaasa waamini wake kwa maneno haya, ‘’Misalaba mingi tunayobeba ni ya kujitengenezea wenyewe, tumeitengeneza kwa dhambi zetu.’’ Watanzania tujilaumu wenyewe kwa kuendelea kukichagua chama tawala. Chama tawala kimewatengenezea Watanzania misalaba mingi, tujiulize maswali haya, iweje leo mwekezaji athaminiwe kuliko Mtanzania?
Je, Watanzania hatuoni kwamba huo ni msalaba? Iweje leo matajiri ndiyo wamiliki mashamba makubwa? Iweje leo wakulima wahamishwe kwa sababu ya mwekezaji? Waafrika na Watanzania kwa ujumla, kwa wawekezaji tunaonekana kama mambumbu ambao hatuna akili na wala hatujui tupo wapi au tunataka kwenda wapi.


Kinachofanyika sasa ni kutoa ardhi mikononi mwa wananchi kinyemela na kuwapa wageni. Huu ni ukoloni wa kisasa unaofanywa na viongozi wetu, viongozi wamegeuka kuwa mawakala [agents] wa wageni na hili viongozi wetu wanalifanya kwa ufahamu wao wote.
Ooo! Hi ni aibu. Watanzania tumeendelea kulia hali ya maisha kuwa ngumu, huu ni msalaba tena mzito, ni kwa sababu tumekuwa tukiwapa ridhaa baadhi ya watu wasiotufaa. Umefika wakati sasa tuache kujitengenezea misalaba. Misalaba ya kujitengenezea ni dhambi. Tuamke. Tushituke. Tujanjaruke. Porojo za wanasiasa uchwara zimetuchosha.


Huu ni muda wa umma wa Watanzania kufikiri. Huu ni muda wa umma wa Watanzania kuamua kuitengeneza Tanzania mpya, Tanzania yenye neema kwa wananchi wote. Hatujachelewa kuamua. Hatujachelewa kufikiri.
Historia ni mwalimu mzuri na ni shahidi bora katika nyanja za kujifunza, basi tujiulize tulipotoka, tulipo na tuendako. Kuna matumaini au kuna giza. Kuna faraja au kuna majonzi. Miaka inavyoendelea kukatika ndivyo tunavyozidi kushuhudia roho ya utaifa ikipotea kwa kasi kubwa, viongozi wanakiuka maadili ya uongozi.


Kuna mpasuko katika Taifa letu, mpasuko wa aliyenacho na asiyenacho. Mpasuko wa udini. Mpasuko huu umetengenezwa na chama tawala. Ipo methali ya watu wa Kenya inayosema hivi, “Ukitaka kwenda kwa kasi, tembea peke yako. Ukitaka kufika mbali, tembea pamoja na watu wengine.’’
Je, ni kweli kwamba Watanzania tunatembea pamoja kimaono? Kifikra? Au tunatembea kivyama, kidini, kiukabila na kikanda? Hii ni changamoto kwetu. Watanzania tumegawanywa na tumegawanyika. Tumeyumbishwa na tumeyumbika. Leo hii hatupigani vita na ukoloni mkongwe. Lakini tuna vita vigumu. Vita ya ukombozi wa kifikra, vita ya kujilimbikizia mabilioni kwa watu wanaotumia uongozi kama vitanda wanavyolalia, vita ya umasikini, vita ya udini, vita ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kadhalika.
Watanzania, tuna wasomi wa kutosha lakini kwa sababu ya kuhofiwa kunyang’anywa madaraka na wasomi, kumekuwapo na migongano ya kifikra na kimaslahi. Viongozi wasio wasomi hawako tayari kupokea mashauri ya wasomi wetu. Hii ni shida, naomba Watanzania tuitatue Oktoba, mwaka huu.


Kwa mtazamo makini, kwa vigezo makini na kwa historia makini nashawishika kusema hivi, Taifa hili liko hivi lilivyo kwa sababu ya uongozi dhaifu wa chama tawala, tazama leo hii mafisadi wanavyokumbatiwa kama wafalme, wawekezaji wanavyothaminiwa na kulindwa kama mboni ya jicho. Haya ni matusi kwa Watanzania.


Leo hii katika Taifa letu rushwa ndiyo ada kwa watawala na watawaliwa. Wapinzani wanapenda wapate ushindi lakini chama tawala kinamwaga mapesa kwa mawakala wa kuhesabu kura na mawakala wanauza kura kwa wenye mapesa.
Kwa sababu ya rushwa mawakala wanazimisha ndoto za Watanzania walio wengi. Eee! Mungu tuhurumie. Rushwa inarusha hata wapigakura. Falsafa iliyopo katika Taifa hili, ni kwamba asiyetoa anashindwa na anayetoa anashinda.


Aliyenacho anathaminiwa asiyenacho anatazamwa kama kinyago. Fedha zimekuwa kigezo kipya cha kutafutia uongozi. Kauli ya Mwalimu Nyerere kwamba wanaogawa fedha hizo walizitoa wapi, na kwamba watazirejesha vipi imewekwa kapuni na viongozi wetu.
Matendo safi yanachafuliwa na rushwa. Viongozi mahiri na wenye weledi makini wanashindwa kupata madaraka kwa sababu ya rushwa. Mmh! Ni kwa sababu ya uongozi dhaifu wa chama tawala. Kupotea njia ndiko kujua njia.


Kwa miaka kadha wa kadha Watanzania tuliithamini CCM tukaipa ridhaa ya kutuongoza, kumbe tulitoa mwanya wa kunyonywa rasilimali zetu. Huu ni mwaka wa Pasaka kwa Watanzania. Ni mwaka wa kwenda kwenye nchi ya ahadi. Misri ya CCM tumeichoka. Ni mwaka wa kufufuka na kushinda longolongo za wanasiasa uchwara. Ni mwaka wa kushinda kwa kuwachagua viongozi wenye moyo wa uzalendo kwa Taifa hili.


Mjadala huu nautamatisha kwa maneno ya Padre, Dk. Faustine Kamugisha, yanayosema hivi; “Unapofundishwa, fundishika. Unapopewa, toa. Unapofarijiwa, fariji. Unapofurahishwa, furahisha. Unapoelimishwa, elimisha. Unaposaidiwa, saidia. Unaposikilizwa, sikiliza. Unapotembelewa, tembelea. Unapopendwa, penda. Unaposamehewa, samehe’’.
Taifa hili hatuwezi kukata tamaa kwa yaliyojiri chini ya uongozi CCM. Huu ni mwanzo mpya na huu ni mwaka wa kuizika CCM. Mwisho wa sura si mwisho wa kitabu. Kuna sura nyingine zinaendelea tena zenye mada tamu kama asali. Nakubaliana na Libba Bray, kwamba ‘’Hatuwezi kurudi nyuma. Tunaweza tu kwenda mbele’’. Mungu ibariki Tanzania.

0757 852377/0783 994403

3134 Total Views 4 Views Today
||||| 5 I Like It! |||||
Sambaza!