Chadema Yakanusha Kuhusu John Mnyika Kujivua Ngwamba

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekanusha taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kuwa Mbunge wa Kibamba, John Mnyika amejivua uanachama wa chama hicho.

Disemba 3 kuanzia majira ya alasiri zilianza kusambaa taarifa zinazodai kuwa mbunge huyo amekihama chama hicho na kujiunga Chama cha Mapinduzi (CCM). Taarifa hiyo ilikuja ambapo kwa siku za hivi karibuni tumeshuhudia wimbi kubwa la watu wakihama kutokana chama kimoja kwenda kingine, kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa chama walichotoka.

Kupitia kurasa zao zi mitandao ya kijamii, CHADEMA wamewataka wananchama wao na wananchi kwa ujumla kupuuza madai hayo na kwamba waliokosa majibu kuhusu hali ya watanzania, ndio wanaosambaza taarifa hizo za uongo.

“Kuna taarifa zinasambazwa mitandaoni ya kuwa Mhe. John Mnyika, Mbunge wa Kibamba amejivua uanachama wa CHADEMA. Taarifa hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote, ni za kupuuzwa, wanaozisambaza ni wale walioishiwa hoja na majibu juu ya hali ya maisha ya Watanzania.”

Wakati huo huo, kambi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif imezungumzia kitendo cha Mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) kujiunga CCM na kusema kuwa bado wabunge wengine wawili wa CUF wataondoka.

Wakati kambi ya Seif ikisema hayo, Mwenyekiti wa CUF, Prof. Lipumba amebainisha kuwa Kamati ya Utendaji itakutana karibuni ili kujadili uamuzi wa mbunge wa chama hicho kutimkia CCM.