Chanjo ya corona kufufua utalii

DODOMA

Na Mwandishi Wetu

Serikali imepongezwa kwa kuruhusu chanjo ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19), hatua itakayofungua milango katika sekta ya utalii nchini.

Sekta hiyo ambayo ni moja ya vyanzo vikuu vya mapato nchini, imeathirika zaidi kutokana na ugonjwa huo.

Akizungumza na JAMHURI, Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii (TATO), Wilbrod Chambulo, anasema kuanza kutumika chanjo ya corona ni faraja kwa wadau wa utalii.

“Tumejipanga kupokea chanjo hiyo na sasa tupo tayari kupokea watalii. Corona imeyumbisha utalii lakini sasa sekta hii inafufuka,” anasema Chambulo.

Anasema hatua hiyo muhimu itawafanya watu wa mataifa mengine kufahamu kwamba Tanzania inajali wananchi wake pamoja na wageni wanaokuja kutalii.

“Kwamba, chanjo imekwisha kuingia nchini, kwetu hii ni taarifa njema sana. Sisi wadau wa utalii tunasubiri zamu yetu ifike tukachanjwe. Tunasuburi maelekezo na taratibu za nchi kujua jinsi ya kupata chanjo,” anasema.

Kuanza kutumika kwa chanjo ya COVID-19 nchini ni kielelezo kwamba serikali imejipanga kufufua utalii uliodumaa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Chambulo anasema kwa kulitambua hilo, watoa huduma wote wa utalii ni muhimu kupata chanjo, ingawa mwongozo wa serikali ni kwamba chanjo hiyo ni ya hiari.

Anasema wao hupokea wageni ambao kwa namna yoyote watakuwa wamekwisha kuchanjwa na watakuwa na imani iwapo wenyeji wao nao wana chanjo.

“Asilimia 90 ya wadau wa utalii wapo Kanda ya Kaskazini. Huku suala la chanjo tumeshaliweka sawa kwamba wafanyakazi wote wanaowahuduhumia watalii wapate chanjo ili kukidhi vigezo vya kuwahudumia wageni hao,” anasema.

Anahoji akitoa mfano wa ndege yenye watalii kutoka Marekani au Uingereza ambayo wote waliomo, kuanzia rubani, wamechanjwa, kwa nini wanaowapokea hapa nchini wasiwe wamechanjwa?

Chambuso anasema watu anaowasiliana nao nje ya nchi wamefurahishwa sana na uamuzi wa serikali kuruhusu chanjo ya corona.

“Tunatarajia kupata mafuriko ya watalii wakati wowote kuanzia sasa,” anasema.

Mwongozo wa serikali unaonyesha kwamba watakaopewa kipaumbele ni vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya utalii.

Watakaopewa nafasi ya kwanza kupata chanjo katika sekta ya utalii ni wanaohusika moja kwa moja na wageni kama maofisa wa uhamiaji, madereva, wapokea wageni, wapishi, wahudumu wa kawaida hotelini, mameneja na wakurugenzi.

Mmoja wa wadau wa utalii, Cosmas Hale wa Arusha, anasema jitihada hizo za serikali ni za kupongezwa kwa kuwa inaonyesha ni namna gani inawajali Watanzania kwa kuwapa chanjo bure na kwa hiari.

“Serikali hii ni makini. Mimi maoni yangu, ingawa serikali imesema chanjo ni ya hiari, Watanzania kuchangamkia fursa hii ni kuifanya chanjo kwetu kuwa ni ya lazima,” anasema.

Serikali pia inapanga kuanza kuanzisha mchakato wa kujenga kiwanda chake cha kutengeneza chanjo ya corona.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi, anasema tayari hatua madhubuti zinachukuliwa kupamba na wimbi la tatu la corona, ikiwamo ujenzi wa kiwanda cha chanjo.

Tayari chanjo imeanza kutolewa.