CWT kwawaka

Fukuto limezidi kuwa kubwa ndani ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) baada ya gazeti hili kuchapisha taarifa za kuwapo ufujaji wa mali za walimu wiki iliyopita, JAMHURI linathibitisha.

Wiki iliyopita JAMHURI lilichapisha orodha ya wafanyakazi waliopewa ajira kwa njia ya upendeleo ndani ya CWT, hali inayotajwa kuwa imefungua ‘kabrasha la madudu’ yanayofanyika ndani ya CWT.

Haraka baada ya habari hiyo kuchapishwa uongozi wa CWT uliitisha kikao cha dharura na kukubaliana kuitisha mkutano wa waandishi wa habari kukanusha habari hizo kwa kufahamu kitakachoendelea kutokana na utamaduni wa Gazeti hili la JAMHURI la uchunguzi, hasa baada ya kuelezwa kuwa lingechapisha masuala mazito.

Taarifa za ndani ya CWT zinaeleza kuwa kikao hicho hakikufikia mwafaka, ingawa walikubaliana kuwa wakakanushe, Rais wa CWT Mwalimu Leah Ulaya, inaelezwa aliwaambia viongozi wenzake kuwa hakuna cha kukanusha katika kilichoandikwa na JAMHURI.

“Hatuna cha kukanusha. Tena JAMHURI wanapaswa kupongezwa kwa kazi iliyotukuka. Kwani ni kipi cha uongo walichoandika JAMHURI?” Mwalimu Ulaya aliyetarajiwa kushiriki mkutano na waandishi alikaririwa akimwambia Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif. Hadi tunakwenda mitamboni mkutano huo ulikuwa haujafanyika.

Majengo, TDCL, Benki ya Mwalimu si mali ya walimu

Uchunguzi uliofanywa na vyombo viwili huru; ambavyo ni Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati Maalumu ya Kuchunguza ya Kampuni ya Maendeleo ya Mwalimu (TDCL) iliyoanzishwa Aprili 4, 2003 si mali ya walimu.

Wamebaini kuwa kampuni hii kwa mujibu wa Katiba yake (MEMART) ilipaswa kuwa na mtaji wa Sh milioni 10, zilizogawanywa kwenye hisa moja moja yenye thamani ya Sh 100,000 kila moja.

“Kinachosikitisha zaidi ni kuwa hao waliohisi wana mali nao hawakujali sana kusimamia kampuni hii na ndiyo maana hawakuona umuhimu wa aina yoyote ya kufuatilia ama kuisimamia kwa karibu kampuni hii.

“Kibaya zaidi Chama cha Walimu kilijenga jengo kwa gharama ya shilingi 5,943,000,000.00 na kutolikabidhi kwa TDCL [kisheria],” inasema sehemu ya taarifa ya kamati hiyo iliyokuwa na wajumbe Hamisi Lissu (Mwenyekiti), Nuru B. E. Shenkalwa (Katibu), Amina Kisenge (Mjumbe), Abubakar Allawi (Mjumbe) na Moses Mnyazi (Mjumbe aliyejitoa).

Uchunguzi unaonyesha kuwa pamoja na TDCL ambayo ni kampuni ya walimu iliyoanzishwa mahususi kuendesha miradi ya walimu, bado kampuni hii iliingia mkataba na Kampuni ya GIMCO Africa inayoendesha jengo la Kitegauchumi cha Mwalimu kilichopo Ilala, jijini Dar es Salaam.

Wamiliki wa Kampuni ya TDCL

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, wamiliki wa TDCL waliosajiliwa na Msajili wa Makampuni ni Justinian Rwehumbiza anayemiliki asilimia 50 ya hisa alizozilipia mtaji wa Sh milioni 5, na (marehemu) Juma Abdallah anayemiliki hisa 1, aliyoilipia Sh 100,000 kama mtaji.

“Katika vikao vyote vya chama na viongozi waliaminishwa na hata bodi zote zilizopita kuwa Kampuni ya Maendeleo ya Walimu ni ya wanachama wa Chama cha Walimu ambapo Katibu Mkuu ana hisa (01) na Chama cha Walimu kina hisa 99.

“Baada ya kuteuliwa Bodi mwaka 2014 nayo Bodi ilituaminisha kuwa chama kina hisa 70 na Katibu Mkuu ana hisa (01). Kwa mujibu wa Katiba ya kampuni na kanuni zake kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Na. 12 ya Mwaka 2002 maelezo yote hayo hayakuwa sahihi.

“Tume hii mpaka imeundwa, kampuni iko chini ya umiliki wa wanahisa wawili ambao ni Justinian Rwehumbiza na Juma Abdallah na Katibu wa Kampuni ni Ndugu Riyaz Takin ambaye hakuna kiongozi hata mmoja anayemfahamu.

“Katika uchunguzi tulibaini kuwa hakuna mahali popote katika Katiba ya kampuni inatamka kukitambua Chama cha Walimu na tulishindwa kubaini kwa nini wanahisa hawaendeshi kampuni yao au kuna jambo wanalisubiria ndipo waje kuiendesha kampuni yao,” inasema sehemu ya taarifa hiyo ya uchunguzi uliofanywa na CWT.

Umiliki wa Kampuni hii ya Maendeleo ya Walimu unaonyesha mkanganyiko mkubwa wa umiliki. Wakati Brela ikionekana wamiliki ni Rwehumbiza na Abdallah, Taarifa ya Mwaka 2005 ya TDL inaonyesha wanahisa wafuatao:-

“Justinian Rwehumbiza hisa (50), Magreth Sitta (10), Yahaya Msulwa (10) na Juma Abdallah hisa (1). Na katika certificate ambayo chama (CWT) kilipewa na TIC inaonekana kuwa wanahisa wa TDCL ni registered trustees wa Chama cha Walimu wenye hisa (50) na wengine wanabaki, isipokuwa Justinian Rwehumbiza ambaye ametolewa katika certificate hiyo,” inasema sehemu ya taarifa ya uchunguzi.

Hapo katikati taarifa zilipoanza kuvuja kuwa TDCL si mali ya CWT, viongozi wajanja wamekwenda Brela kujaribu kubadili umiliki wa kampuni kutoka TDCL, ila wamekwama kutokana na hofu ya uongozi wa Rais Magufuli.

Akiwa jijini Dodoma katika mkutano wa CWT, Desemba, 2017 Rais John Magufuli aliwaambia miradi mingi ya CWT ni hewa, kwani hata Benki ya Mwalimu (MCB) ni mali ya watu wengine wasio walimu, suala lililothibitika kutokana na muundo wa umiliki wa MCB. Inamilikiwa na TDCL na wanahisa wengine.

Maoni ya Tume ya Uchunguzi

Tunaamini kuwa hakuna taasisi isiyokuwa na matatizo duniani ila hutofautiana kwa viwango na yanapokithiri wenye mali hutafuta namna ya kujikwamua na matatizo hayo. Hivyo maoni haya ni kwa ajili ya kujenga na wala si kubomoa misingi iliyowekwa na ni kuimarisha ili nia njema iweze kutimia na matunda ya kuanzisha chama yaweze kumfikia kila mmoja.

Hivyo mkutano huu wa wanahisa ili uweze kufanya maamuzi sahihi ni lazima ujigeuze kuwa baraza la Taifa ili mapendekezo yaliyotolewa yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa baraza la Taifa. Hivyo kamati inaweka mapendekezo haya kwa baraza la Taifa kwa sababu ya kukwepa utata wa kisheria ambao umejengwa katika Katiba na Kanuni za kampuni hii ambayo siyo mali ya chama kisheria japo kihisia ni ya Chama cha Walimu.

I.  Utaratibu wa kisheria ufanyike ili wale wanahisa wanaotamkwa katika katiba na kanuni warejeshe umiliki wao kwa Chama cha Walimu na washirkishwe kwa uwazi na kufuata utaratibu wa kisheria ili kusiwe na suala la kuwasemea wale ambao wako hai. Waitwe kwenye kikao maalumu waandike azimio lao la kuuza haki yao katika kampuni na wale wanaozichukua wakubali kuzipokea na kodi stahiki za serikal zilipwe.

II.  Katiba ya kampuni na kanuni zake zipitiwe na wataalamu wa ndani ya Chama cha Walimu chenyewe kwa kupitia mstari kwa mstari ili kujiridhisha kama yaliyoandikwa yanakidhi mahitaji ya chama pasipo kuathiri sheria na kuongeza kinachostahili na kuhakikisha chochote kilichobadilishwa kinapelekwa kwenye vikao vya maamuzi na hatimaye kusajiliwa BRELA.

III.  Wakurugenzi wa Kampuni wawe ni Katibu Mkuu, wadhamini mmoja kwa mzunguko na wajumbe watatu wateuliwe miongoni mwa wajumbe wa baraza ikiwezekana kwa kuzingatia taaluma zao kama zinagusa mambo ya biashara na kila mwaka wabadilike japo wanaweza kuchaguliwa tena. Bodi ya sasa ivunjwe kwa haraka iwezekanavyo ili kampuni irudishwe kwa wenye mali wanaostahili ambao ni Katibu Mkuu na wadhamini.

IV.   Iwapo itakubalika kampuni kufanywa ya Chama cha Walimu mpango wa kibiashara (business plan) na sera (policy) viandaliwe ili kubaini biashara zipi zifanywe na kampuni kwa niaba ya Chama cha Walimu.

V.    Kwa kuwa lengo la kampuni ilikuwa kumkomboa mwalimu na walimu ni wengi, kampuni hii kuwa ya binafsi haiendani na wingi wa walimu. Tunaweza kuendelea na hali ya sasa kama hatua ya mpito ya maandalizi ya kuwa kampuni ya kijamii (public) ili walimu wanunue hisa kwenye kampuni kwa ajili ya kuendesha biashara kubwa zaidi na kuongeza umakini katika usimamizi wake, hivyo itagusa walimu wengi.

VI.   Jengo la Mwalimu House lisimamiwe na TDCL kwa mkataba maalumu utakaosaidia wao kulitambua kama mali ili wakati wa kuandaa taarifa za fedha waweze kujumuisha uchakavu wa jengo na kupunguza kiwango kikubwa cha kodi inayolipwa na fedha zitakazotengwa kwenye uchakavu zitumike kufidia katika ukarabati wa jengo.

VII.  Mtaji wa kampuni urekebishwe kwani ilivyo sasa ni kama TDCL inafanya biashara haramu kwa kuwa ina mtaji uliolipiwa wa shilingi 5,100,000.00 na wala haina mkopo wa aina yoyote bali inafanya biashara ya mabilioni ya fedha. Hili linaweza kuchukuliwa kuwa kampuni hii inatakatisha fedha, jambo ambalo si la kweli, ila huwezi kuwa na shilingi 5,100,000.00 halafu uzalishe shilingi bilioni moja kwa mwaka.

VIII. Kampuni ya TDC iajiri watumishi wake wenyewe watakaowajibika kwenye bodi iliyo chini ya mtendaji mkuu wa chama ili akishindwa kuisimamia awajibishwe yeye mwenyewe bila ya kuwa na mwanya wa kukwepa.

Vivyo hivyo ili kukidhi matakwa ya kisheria, Katiba ya Chama cha Walimu itambue kuwa kila kampuni iliyoanzishwa na Chama cha Walimu iwe na siku moja ya kuja kutoa taarifa ya maendeleo na changamoto mbele ya Baraza la Taifa ili waweze kujua hali ilivyo kabla ya kwenda kwenye mikutano yao mikuu wawe tayari wameshapata mawazo ya chama.

Iwapo hili halikutazamwa kwa kina, chama kitakuwa kinawaanzishia watu makampuni na chenyewe kinabaki kilivyo na huku kikijivunia makampuni ambayo hayamsaidii mwalimu na wala chenyewe hakinufaiki.

IX.   Chama cha Walimu kifanye tafiti za kina kabla ya kuanzisha makampuni ambayo yanakuwa vichaka vya baadhi ya watu kuficha maovu yao. Hakuna faida yakinifu ambayo imepatikana kutoka mwaka 2007-2015 katika jengo ambalo tulilijenga kwa kujinyima halafu wenzetu wachache ndani ya chama wanajimilikisha kwa kufanya mambo yasiyo na tija.

X.  Katika kipindi cha 2007-2014 zaidi ya shilingi milioni elfu tano (5,000,800,000) zimekusanywa, lakini hakuna kiongozi hata mmoja mwenye ujasiri wa kusema fedha hizo zimefanya nini zaidi ya watu kujichumia kwa kuingia mikataba isiyo na tija, kuzitumia pasipo uwazi na chama chote kimeshikwa ganzi kusema ziko wapi au nani amezitumia.

XI.   Kamati ya Utendaji ya Taifa bila kuchelewa ichukue hatua stahiki kwa wale wote ambao kwa namna moja ama nyingine wametumia nafasi zao kuhujumu kampuni hii, ya walimu na hivyo kukiweka chama njia panda kutokana na hasira walizo nazo juu ya Mwalimu House. Tumesoma kwenye magazeti au kuulizwa kwenye mikutano.

XII.  Baraza la Taifa lichukue hatua stahiki kuielekeza Kamati ya Utendaji juu ya hatua za kuchukua dhidi ya bodi zilizofanya maamuzi yasiyofaa na kukishauri chama ipasvyo wakati walikuwa wanajua kuna udhaifu na huku wakiendelea kutumia fedha au chama kukopa na kutumia pasipo hata kuonyesha fedha hizo zinakwenda wapi baada ya chama kupata fedha zake.

Mfano kama kulikuwa na upungufu wa mishahara chama kikakopa si jambo baya, ila mara baada ya fedha za ada kupatikana zilipaswa kurudishwa na badala yake zikapelekwa ambako hazijulikani na ndiyo maana hazionekani kwenye taarifa za fedha za chama.

XIII. Malengo ya chama na kampuni yahuishwe pamoja ili kuwe na muonekano bayana wa chama kuwa na uhusiano na makampuni yanayoanzishwa na chama kwa manufaa ya wanachama. Malengo yalivyo sasa huwezi kuyapima kama yanaendana na hali halisi ya TDCL.

XIV. Kampuni iendeshwe kwa mujibu wa sheria na ikumbukwe kuwa hata kama itachelewa kufuatiliwa ipo siku serikali itafuatilia juu ya udhaifu ambao ulifumbiwa macho huko nyuma. Kama taarifa za mrejesho wa kampuni zinatakiwa zifanyike kila mwaka na iwapo hukufanya hivyo kuna faini.

Companies Act No 12 of 2002 Section 128(3) state that, if a company fails to deliver annual return in accordance with this chapter within twenty eight days of the return date, the company and every officer of the company who is in default shall be liable to a fine and, in case of a continued failure to deliver an annual return, to default fine.

Kwa kuwa Kampuni ya TDCL haikutimiza wajibu huu, tujiandae kisaikolojia wakati Msajili wa Makampuni atakapochukua hatua ya kuiwajibisha TDCL.

XV.  Kwa kuwa kampuni inakusanya fedha za kodi na kwa kuwa muda wa tume ulikuwa mdogo tunapendekeza ufanyike ukaguzi maalumu kubaini ubadilishaji wa fedha za kigeni zinazokusanywa na viwango vya ubadilishaji kama ni halali.

Mkaguzi huyu atoke nje ya mfumo wa chama na ikiwezekana apendekezwe na Baraza na taarifa yake iletwe kwenye Baraza moja kwa moja. Kampuni hii ikague ankara za umeme, maji, malipo ya watoa huduma kwa kina na ijiridhishe na eneo la jengo linalostahili kupangishwa, yaani jengo lipimwe ili kubaini ukubwa halisi wa eneo linalopangwa. (Kampuni ya Ernest and Young inaweza kupewa kazi hii).

XVI. Mkaguzi wa hesabu wa awali arudishwe na kama ni kuondolewa basi taratibu za kisheria zifuatwe kwa kuwa vitu alivyokuwa anahoji ni vya msingi ila wenye mali walikuwa hawachukui hatua kwa sababu zisizojulikana na hiyo ndiyo pengine kulikuwa na sababu ya kumuondoa.

Kwa kuwa umewekwa utaratbu wa kumuingiza kwenye ukaguzi wa kampuni kwa mujibu wa sheria, ni vema utaratibu huu usomwe kwenye sheria ya makampuni namba 12 ya mwaka 2012, section (170-179) zinaelekeza namna ya kumuweka na kumuondoa mkaguzi wa hesabu.

XVII.        Kampuni hii kwa kuwa ilikosewa katika misingi ya uanzishwaji haina mali zake hasa zile za msingi ambazo zingetumika kufanya biashara yake ya kujitegemea. Chama cha Walimu kiamue kama kinahitaji kampuni hii ifanye nini na ipewe mtaji stahiki kufanya biashara iliyolengwa. Kama haja ni kufanya biashara ya real estate, basi iwezeshwe na ifanye kazi hiyo kwa malengo ya kuinua kampuni kwani kwa sasa haina kitu cha maana.

XVIII.    Ni kawaida kwa kampuni kudaiwa na kudai kwa kuwa ndio utaratibu wa wakati na biashara nyingi duniani kote. Japo Kampuni ya TDCL haikuwa na mali, lakini ilikuwa imejipa dhamana ya kusimamia ukusanyaji kodi wa jengo la Mwalimu House. Hivyo kampuni inadaiwa na pia inadai. Uwezo wa kampuni hupimwa kwa uwezo wake wa kulipa madeni kwa wakati na kukusanya madeni yake.

Kampuni ya TDCL inaidawa pasipo sababu ya msingi na inashindwa kukusanya madeni pasipo sababu zinazoeleweka bayana, kwani wapangaji wote hawana mikataba. Jitihada zifanyike kama kampuni hii itaendelea.

XIX. Mikataba yote ni ya kupitiwa upya na ikishaandaliwa ikapitiwe na Kamati ya Utendaji ya Taifa kabla ya kuanza kutumika au Bodi kabla ya kuanza kutumika kwa wapangaji na makampuni yanayotoa huduma katika jengo la Mwalimu House.

XX.  Mwanasheria wa kampuni aliyepo haisaidii Kampuni ya TDCL na tayari Chama cha Walimu kina wanasheria ambao wangeweza kutoa huduma hizo. Ila ni vema Chama cha Walimu kikawatambua wanasheria waliopo na kuanzisha idara ya utetezi na sheria ili chama kiwe na mwanasheria wa chama anayetambuliwa na wote.

XXI. Kambalau (lift) ni vema ikanunuliwa kwa sababu kwa muda mrefu ni mbovu na watakaohusika na manunuzi hayo wafanye utafiti wa kutosha ili wanunue kambalau itakayodumu kwa muda mrefu na ikiwezekana wasinunue Kampuni ya OTIS.

XXII. Ununuzi wa viwanja vya Morogoro unatia shaka kubwa ambayo haiwezi kumalizwa na tume. Kamati ya Utendaji ishughulikie jambo hilo na kuhakikisha kuwa fedha za TDCL zinarudishwa.

Tunaweza kutumia uwezo wetu kujipatia viwanja kwa sababu sisi ni sisi, na tuna pesa na tunaweza hata kuielekeza sheria kile tunachotaka ila hatutaweza kubadililisha ukweli ambao siku moja utathibitika kama si duniani, basi hata kule ambako kila mwandamu siku moja atakwenda.

XXIII.   Mali zote za Kampuni ya TDCL ziwe chini ya Chama cha Walimu mpaka pale usajili wa hisa za kampuni utakapokuwa umekamilika na kuwa miliki halisi ya Chama cha Walimu.

XXIV.    Hisa za TDCL kwa MCBL zithibitishwe kwa maandishi kwani MoU haitoshi na MBCL wathibitishe kwa maandishi na TDCL wapewe hati ya hisa hizo.

XXV.   Kampuni ya TDCL ifanye utafiti na kuona ni maeneo yapi yanafaa kuwekeza mfano kujenga hosteli maeneo yenye vyuo vikuu ili kusaidia taifa na wanafunzi kusoma vizuri zaidi kwa kuwa na mahali penye uhakika pa kukaa.

Hitimisho

Tukumbuke cheo ni dhamana na siku moja wenye dhamana wanaweza kuchukua. Umefika wakati kila mjumbe wa Baraza ajiulize, hivi ni kwa nini Kampuni ya Maendeleo ya Walimu iko hivi tulivyo leo?

Yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika ndani ya chama na kampuni hayampendezi Mungu. Kila mmoja ajitafakari na ajihoji ni kwa nini tulianzisha Chama cha Walimu.

Yatosha kusema yatosha na wenye mamlaka waamue kulinda uovu ili chama kife au kuchukua hatua kukiokoa chama. Mwenye macho haambiwi tazama, tupo katika wakati mgumu.

Mwaka 2016 uongozi wa CWT uliwafahamisha wanachama kuwa umefanya mabadiliko katika umiliki wa kampuni na hisa zimerejeshwa kwa walimu, lakini uhalisia taarifa bado zinaonyesha udanganyifu huo unaendelea.

Ukaguzi maalumu wa CAG

Sehemu hii inaeleza kwa muhtasari mambo muhimu yaliyojitokeza katika uchunguzi tuliofanya kwenye Chama cha Walimu Tanzania – uchunguzi huu tulifanya katika Mkoa wa Dar es Salaam na tumebaini dosari / mapungufu mbalimbali katika Chama cha Walimu Tanzania ambayo maelezo ya kina yametolewa katika Sura ya Pili, Aya ya Tano ya ripoti hii inahusika. Masuala na mambo muhimu yanayohusiana na mapungufu hayo ni kama ifuatavyo:

1. Katiba ya Chama haijaweka bayana ushirikishwaji wa kila mwanachama katika ngazi mbalimbali za uongozi kwenye kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha Katiba ya Chama. Hivyo  tumeshindwa kuthibitisha kama wanachama wa CWT walitoa mawazo yao katika kuboresha Katiba ya Chama ya mwaka 2014 ambayo imeonekana kuwa na mapungufu.

2. Katiba ya CWT na Kanuni zake zinakinzana juu ya majukumu ya Bodi ya Wadhamini katika usimamizi wa mali za chama; kulingana na Katiba ya Chama, Ibara ya 35(b) Wadhamini ni waangalizi na wadhibiti wa mali za chama wakati Kanuni ya Chama Na. 37(a) inasema mali zote za chama zitaandikishwa kwa jina la Wadhamini wa Chama. Hii inaleta mkanganyiko juu ya majukumu halisi ya Bodi ya Wadhamini katika mali za chama na pia inaweza kuleta mgongano wa kimasilahi katika mali za chama.

3. Uchunguzi umebaini kuwa mali za CWT hazijasajiliwa kwenye daftari/rejesta ya Mali za kudumu ikiwemo magari, majengo, kompyuta, samani na kadhalika.

4. Katiba ya CWT ina mapungufu katika ukomo na unufaikaji kwa mwanachama aliyefariki au kustaafu kwani Ibara ya 9.2 imeeleza ya kwamba mwanachama akikoma kuwa mwanachama hatarudishiwa ada zake, lakini wakati huo huo Kanuni ya CWT Na. 29 imeelezea kuwa mwanachama akistaafu akiwa amechangia CWT miaka 15 mfululizo atapewa mkono wa kwaheri, lakini mkono huo haukuwekwa bayana kuwa ni wa kitu gani au kiasi gani cha fedha. Hali hii inaweza kuleta upendeleo au migogoro katika chama.

5. Uchunguzi haukuweza kujiridhisha kwenye mchakato uliofanywa na CWT pamoja na vigezo vilivyotumiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo na Ufundi. Kwenye utoaji wa mkataba wa kukitambua Chama cha Walimu Tanzania kama chama kinachotetea haki na masilahi ya walimu wote Tanzania Bara pamoja na mkataba wa kutoa mamlaka kwa Chama cha Walimu juu ya utozaji wa Ada ya Uwakala kwa walimu wasio wanachama (Recognition and Agency Shop Agreements) ambapo mwaka 2014 mwezi Aprili chama kilionekana kuwa na wanachama zaidi ya 50% ya walimu wote Tanzania Bara hali iliyoipa chama haki ya kutoza 2% ya mshahara wa kila Mwalimu hata asiye mwanachama wa CWT. Taarifa hii iliombwa kwa Katibu Mkuu wa chama ili kujiridhisha uhalali wa taarifa hiyo lakini hatukuweza kupatiwa.

6. Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004, Kanuni za CWT za mwaka 2015 sehemu ya 4(C), Agency Shop na Recognition Agreements za mwaka 2014 zilihitaji chama kiwe na akaunti za benki tofauti za kuweka michango itokanayo na ada za wanachama na akaunti ya kuweka Ada ya Uwakala kwa walimu wasio wanachama ili kuweza kutofautisha kulingana na matumizi yatokanayo na shughuli zinazolenga wanachama na zile zinazolenga watoa Ada ya Uwakala. Kinyume na matakwa hayo, chama hakijaweza kutenganisha akaunti hizi.

7.  Hakuna ushahidi wa kisheria juu ya uwepo na umiliki wa Kampuni ya CWT iitwayo Teachers Development Company Limited (TDCL), ambayo ni kampuni yenye hati ya usajili namba 45719 na iliyoanzishwa na CWT kwa madhumuni ya kusimamia jengo la Mwalimu lililopo llala Boma, ikiwemo kupangisha, kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya pango na kufanya ukarabati wa jengo hilo. Lakini baada ya kufuatilia kampuni hii haijasajiliwa kisheria na BRELA kwani kampuni inayotambulika BRELA ni Teachers Development (T) Limited ambayo inatumia hati ya usajili namba 45719, lakini kumekuwa na utofauti wa majina yaliyotumika kwenye kuisajili kampuni hii wakati taarifa nyingi za Chama cha Walimu Tanzania hazijaonyesha kuwepo kwa Kampuni inayotumia jina la Teachers Development (T) Limited hivyo kuibua utata kama kweli hii ni kampuni halali ya CWT au kuna namna imefanyika kuondoa uhalali wa walimu kuwa na kampuni yao wanayoitambua kisheria.

Timu ya uchunguzi ilijaribu kuomba kama kuna nyaraka zozote ndani ya CWT, ambazo zimetumia jina la Teachers Development (T) Limited lakini liazikuwepo, hivyo kwa kutumia nyaraka zote za CWT na kutokuwepo kwa nyaraka zinazotumia Teachers Development (T) Limited ni dhahiri hii si kampuni ya CWT. Rejea Majibu ya BRELA kwa barua Na. MITM/RC/MISC/2017/21 ya BRELA ya tarehe 7/5/2017.

8. Hakuna ushahidi wa moja kwa moja juu ya masilahi (kwa kila mwanachama) yatokanayo na Kodi za Jengo la Mwalimu House lililopo katika Plot Na. 48 llala Boma, Dar es Salaam, lililojengwa kwa kutumia michango ya walimu ya kila mwezi iliyokuwa ikitolewa kwa Chama (CWT).

9.  Chama kimekuwa kikitoa taarifa ya uwekezaji kwenye vipande vya UTT kwa thamani ya soko (market value) kuwa ni Sh 50,000,0000 toka mwaka 2011 – 2016 lakini uchunguzi ulibaini kuwa mpaka 2017 vipande hivyo vilikuwa na thamani ya Sh 350,000,000 ambapo ni dhahiri ya kwamba katika kila mwaka kulikuwa na mabadiliko ya thamani ya vipande hivyo.

10.  Malipo yenye thamani ya Sh 10,272,952,014.83 yamefanyika bila kuambatanishwa na vielelezo vya uthibitisho kwenye Hati ya Malipo kinyume cha Kanuni za Fedha Toleo la Pili la Mwaka 2011 (b) (v).

11.   Malipo yenye thamani ya Sh 3,646,550,820 yamefanyika kwa ajili ya vikao vya kamati mbalimbali na mikutano mbalimbali ya CWT bila uthibitisho wa aliyelipwa, na kiasi alicholipwa, pia hayana taarifa ya kazi iliyofanyika (Ripoti za vikao, Kamati na Mikutano). Vilevile, uchunguzi umebaini kuwa malipo yenye jumla ya Sh 26,857,334,119 yamelipwa zaidi ya bajeti iliyokuwa imeidhinishwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2011 hadi 2016.

12.   Manunuzi ya viwanja na nyumba zenye jumla ya thamani ya Sh 1,575,661,678 hayakuonyeshwa kwenye Taarifa za Fedha za CWT hata hivyo kulikuwa na ukiukwaji wa mchakato mzima wa manunuzi kwani hakukuwa na vikao halali vilivyoidhinisha manunuzi hayo. Pia uchunguzi ulibaini kuwa viwanja viwili (2) vilivyopo Bunju na Magomeni Kagera vyenye thamani ya Sh. 1,201,861,678 havikuwa na hatimiliki.

13.   Malipo ya takriban Sh 3,287,708,358 yalifanyika bila kuidhinishwa (unthorized payments) hayakupitishwa na kusainiwa na Katibu Mkuu pamoja na Mweka Hazina kama Kanuni za Fedha za CWT zinavyotaka.

14.     Kodi ya Mapato yenye jumla ya Sh 882,995,642 haikulipwa TRA (withholding Tax 5%) kwa malipo yanayotokana na mikataba mikubwa kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za CWT mikoani.

15.    Hakuna uthibitisho wa nyaraka na utaratibu maalumu uliotumika wakati wa kulipa malipo ya walimu wenye matatizo/shida mbalimbali ikiwa ni pamoja na ugonjwa kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2011 mpaka 2016 kwa takriban Sh 1,651,298,605.70.

16.   Mikataba yenye thamani ya Sh 17,668,812,881 ikiwemo mikataba ya ujenzi haikuorodheshwa kwenye Rejesta ya mikataba, kinyume cha Kanuni za Manunuzi pamoja na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ya Mwaka 2004 inayohitaji kuainisha vizuri Daftari (Register) la Mikataba linalopaswa kuonyesha kumbukumbu zote za mikataba zinazojumuisha gharama ya mkataba, tarehe ya kuanza kazi na kukamilisha kazi, mabadiliko yoyote yaliyofanyika pamoja na malipo yaliyofanyika, hali iliyoleta ugumu kwa timu ya uchunguzi kuweza kujiridhisha na uhalali wa mikataba iliyoingiwa na Chama cha Walimu Tanzania. Vilevile, kuna mapungufu kwenye mikataba ya wakandarasi, kwani hakuna nyaraka za zabuni kiasi cha takriban Sh 3,536,569,600 na Dola za Kimarekani (USD) 2,284,968 zilizowasilishwa wakati wa uchunguzi.

17.      Katiba ya CWT imeshindwa kwa kiasi kikubwa kuweka mfumo mzuri wa kiutawala na kiusimamizi, kwakuwa hakuna ukomo wa madaraka kwa viongozi wa kuchaguliwa kama Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Mweka Hazina Mkuu. Mfumo uliopo unawaruhusu viongozi waliopo kukaa madarakani mpaka ukomo wa utumishi wao ilimradi tu wawe wamepigiwa kura na wanachama, hali hii inasababisha kuathiri utendaji wa kazi kwa imani kuwa wataendelea kuwepo na inaweza kusababisha mgongano wa masilahi ndani au nje ya CWT kama ilivyo sasa.

18.   Taarifa za maamuzi ya uongozi wa CWT haziwafikii wanachama kabisa au kwa wakati; hii imechangiwa na kuwepo kwa mfumo hafifu wa utoaji wa taarifa za maamuzi yanayofanyika katika ngazi za Sekretariati ya CWT, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Chama.

Hali hii imedhihirika kupitia madodoso yaliyojazwa na baadhi ya wanachama na wachangiaji wa CWT katika baadhi ya shule/matawi, ambapo 82% ya wanachama waliohojiwa kwa njia ya madodoso walionyesha kutokuwa na taarifa za miradi inayoanzishwa na kutekelezwa na CWT kwa mfano TDCL, MCB na Mwalimu House, misaada inayotolewa na CWT makao makuu kwa walimu wenye shida na taarifa za mabadiliko ya Katiba ya CWT.

Maoni ya CAG

1)    Katiba na kanuni zote za CWT zihuishwe/kupitiwa upya ili kupata mapendekezo ya uendeshaji wa chama kutoka kwa kila mwanachama na baada ya kuhuishwa, kila mwanachama anapaswa apate nakala ya Katiba na kanuni hizo ili aweze kujua haki na wajibu wake katika uendeshaji wa chama kwa manufaa yake na manufaa ya chama kwa ujumla.

2)    Hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe kwa wote waliopewa dhamana ya kuongoza Chama cha Walimu na hawakutekeleza kwa matakwa ya wanachama na kanuni za chama.

3)    Viongozi waliotumikia chama kwa muda mrefu waachie nafasi zao ili kuweza kuwapa fursa wanachama wengine kuongoza chama kama sehemu ya kuonyesha uwajibikaji.

4)    Mikataba  yote iliyoingiwa na Chama cha Walimu ipitiwe upya ili kuona kama ina tija kwa wanachama na chama.

5)    Chama kifuate sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2014 ikiwemo kuweka taarifa kamili na sahihi kwa kila mwanachama na Katibu Mkuu wa chama aweke taratibu zenye kujitosheleza ili kuweza kudhibiti mapato ya chama yatokanayo na ada za wanachama, ikiwemo kuwa na taarifa zenye kujitosheleza kwa kila aina ya mwanachama kwenye daftari la kudumu la wanachama  hao.

6)    Chama na Wizara ya Elimu wapitie upya mkataba wa utozaji wa ada ya uwakala kwa walimu wasio wanachama ili iweze kutofautiana na ada inayotolewa na wanachama kwa kuwa walimu hawa hawafaidiki kwa kiwango sawa na wanatoa ada ya uanachama.

7)   Asilimia inayotozwa kama ada kwa wanachama ipunguzwe kutoka 2% mpaka asilimia 0.5% au 1% kama inavyopendekezwa na wanachama wengi, pia Baraza la Taifa la CWT lifanye upembuzi wa viwango vya asilimia vya matumizi ya chama ili kuhakikisha kila mwanachama anafaidika moja kwa moja na viwango hivyo na ufaidikaji huo uweze kuwiana na michango ya mwanachama aliyoitoa.

8)    Katibu Mkuu ahakikishe wanachama wote wanaotoa ada ya uwakala wanajulikana na taarifa zao zinaingizwa kwenye daftari lao maalumu, pia ifunguliwe akaunti itakayoweka fedha hizo na matumizi yake yaendane na lengo la fedha hizo za uwakala na zitolewe taarifa kila mwaka.

9)    Baraza la Taifa la CWT lisimamie miongozo ya chama upande wa uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa chama ikiwemo wadhamini wa chama kwa kuzingatia ukomo ulioainishwa kwenye katiba ya chama na lichague bodi nyingine ya wadhamini wa chama ili kufuata matakwa ya Katiba pamoja na kuondokana na viashiria vya mgongano wa kimasilahi kwa wadhamini hao.

10)  Kanuni za CWT zibadilishwe ili ziweze kuendana na Katiba ya CWT upande wa majukumu ya Bodi ya Wadhamini, chama kifanye upembuzi yakinifu kwenye mali zote za chama ili kuhakikisha mali hizo zipo kwenye jina la chama na si kwenye majina ya wanachama wake (wadhamini), kwa kuwa CWT kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004, hivyo kisheria ni mtu “Legal Person” ambaye anaweza kushitakiwa au kushitaki, kwa mantiki hiyo hata mali za chama zinatakiwa ziwe zimeandikishwa kwa jina la chama. Wadhamini wa chama wanatakiwa kuwa wasimamizi tu wa mali hizo.

11)  CWT kiweke bayana miradi yote ya chama ikiwemo taarifa za mapato na matumizi ya miradi hiyo na ni kwa jinsi gani faida itokanayo na miradi hiyo itagawanywa  (itakokotolewa)  kwa kila mwanachama katika uhai wake, uanachama wake au baada ya kustaafu kwake. Kipitie upya katiba na kanuni zake ili kuweka bayana viwango halisi au mfumo halisia utakaotumika kutoa mkono wa kwa heri kwa mwanachama aliyestaafu au pole kwa familia ya mwanachama atakayefariki na kipitie sababu zote za kukoma uanachama na kuainisha masilahi rejesho kwa mwanachama husika kulingana na sababu za ukomo wake ili kutokumfunga mwanachama kuwa mwanachama wa CWT kwa maisha yake yote, kwani sheria imetoa uhiari wa kujiunga na chama angalau kimojawapo cha wafanyakazi.

12)  Chama na Wizara ya Elimu zifanye mapitio upya ya leseni ya uwakala iliyotolewa ili kuweza kujiridhisha juu ya idadi kamili ya walimu waliopo na ambao ni wanachama kamili wa CWT (wale wenye kujaza TUF 6) na vithibitisho hivyo viweze kupatikana kiurahisi pindi vitakapohitajika. Chama pamoja na waajiri wote wafanye jitihada za kuwaelimisha walimu wasio wanachama na wanaokatwa ada ya uwakala juu ya ukatwaji huo na juu ya faida za kuwa mwanachama kamili wa CWT kwani mpaka hivi sasa hakuna tofauti kwenye ulipaji kati ya mwanachama kamili na mwenye kutoa ada ya uwakala licha ya mwalimu mwenye kutoa ada ya uwakala kutofaidika kama mwanachama kamili.

13)  Mhasibu wa chama anatakiwa kutoa taarifa halisi na sahihi za mali za chama kila mwisho wa mwaka wa fedha unapoisha kulingana na taratibu za utoaji taarifa za mali na madeni, ikizingatiwa ya kwamba thamani halisi ya vipande hivyo inapatikana UTT.

14)  Chama cha Walimu Tanzania kifanye haraka usajili wa Kampuni yake (TDCL) BRELA na kiwe na nyaraka za kisheria zenye kuonyesha umiliki wa kampuni hiyo kwa chama na si kwa wanachama wake au watu binafsi ili kuondoa shaka ya mgongano wa kimasilahi kwa watu ambao ndio wanaoonekana kumiliki kampuni hiyo na kiweze kupata faida stahiki kutokana na uwekezaji wake katika Benki ya Mwalimu.

15)  Chama kihakikishe kunakuwepo na mgawanyo  thabiti wa masilahi yanayotokana na vitega uchumi vyote vya chama ili kuondoa malalamiko yaliyodhahiri  kutoka kwa wanachama wake. Vile vile, chama kiwe kinafanya tathmini ya kina juu ya taarifa zinazotolewa na Kampuni yake (TDCL) ili kuweza kujiridhisha kama kweli hakuna faida yoyote itokanayo na jengo la walimu.

16)  Chama hakina Kamati ya Ukaguzi (Audit Committee), hivyo tunapendekeza kuanzishwa kwa Kamati ya Ukaguzi ambayo itahusika kumchagua Mkaguzi wa Nje wa Hesabu za Chama na kuishauri Menejimenti ya Chama juu ya usimamizi wa mali na fedha za chama.

Mapungufu yaliyobainika katika uchunguzi huu maalumu wa Chama cha Walimu Tanzania yamesababishwa na mapungufu yaliyopo kwenye Katiba, ikiwa ni pamoja na ukomo wa uongozi katika ngazi za chama pamoja na Bodi ya wadhamini kushindwa kutekeleza majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kufuatilia na kusimamia shughuli za chama kwa ukaribu na kushindwa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa mapato na matumizi ndani ya chama.

Walimu waandaa mkakati mzito, 700 wajiorodhesha

Taarifa za kina zilizolifikia JAMHURI zinaonyesha kuwa walimu 700 kati ya 1,200 ambao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CWT wamesaini azimio la kutaka uitishwe mkutano mkuu.

Walimu hao wanatoka mikoa 24 ya Tanzania Bara, ambapo mikoa miwili tu ndiyo imekataa kushiriki azimio hilo. Mikoa isiyoshiriki ni Arusha na Geita.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudai Mkutano Mkuu, Evodiuks M. Henerico, ameliambia JAMHURI kuwa mambo yanakaribia kuiva:

“Ni kweli movement ya petition ya kuomba yafanyike marekebisho ya Katiba ya CWT mwaka huu 2019 kama ilivyoazimiwa na Mkutano Mkuu wa 2017 ipo inaendelea. Kwa sasa bado tunalishughulikia katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CWT na mamlaka zinazosimamia Vyama vya Wafanyakazi Tanzania. Kwa sababu hiyo sitaweza kulizungumzia kwa sasa. Ila kamati inayoshughulikia movement hiyo italitolea ufafanuzi baada ya Juni 16, 2019 ikiwa hakuna kitakachokuwa kimetokea,” amesema.

JAMHURI linafahamu kuwa CWT tayari imetumia zaidi ya Sh bilioni 1.0 kukusanya maoni ya jinsi ya kurekebisha Katiba ya CWT na nini kiwemo kwenye katiba hiyo. Hili ndilo linaisukuma kamati kupingana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi ambaye awali aliwaelekeza CWT kuwa na mkutano wa dharura mwaka 2019, lakini baadaye akaufuta.

Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, D. Uiso, katika kinachotajwa kuwa shinikizo kutoka kwa mmoja wa vigogo hapa nchini kuwalinda baadhi ya viongozi wa CWT, Mei 9, mwaka huu aliandika barua yenye Kumb. Na. RTU/CWT/VOL. IV/12/92, ambayo kwa kutumia kigezo cha gharama ameelekeza Baraza la Taifa la CWT kufanya mkutano mkuu mwaka 2022, badala ya mwaka huu. Mwakani kuna uchaguzi wa CWT.

‘Mmiliki’ wa mali za walimu alonga, aeleza picha yote

Mtu anayetajwa kuwa mmiliki wa Kampuni ya Maendeleo ya Walimu, Rwehumbiza, amezungumza na JAMHURI na kusema:

“Kwanza mimi nakueleza hivi; By the time naachana na Chama cha Walimu, yaani nilipostaafu 2009 si ninaacha na mambo yote ya udhamini na mambo yanayohusiana na Chama cha Walimu?

“Kwanza, jengo lilipokuwa linazinduliwa na Kikwete sikualikwa. By the time limejegwa halafu linaanza kukodishwa nafikiri nilikuwa nje ya system… na wakaanza kupangisha watu kabla ya kuunda hiyo kampuni ambayo wanasema mimi ni mjumbe au nina 50%.”

Ameliambia JAMHURI kuwa wakati kampuni hiyo inaundwa alikuwa mdhamini wa CWT, hivyo aliitwa katikati ya mji akaambiwa atie saini andiko lililokwisha kuandaliwa tayari.

“Nakumbuka tulitoka wapi by then? Tulitoka kwenye Ofisi ya Chama cha Walimu wakamuita huyu bwana wakasema si lazima wawe wadhamini wote, mimi nilikuwa nimekwenda Dar es Salaam kwa shughuli fulani wakasema imekuwa bahati kwa hiyo ikawa kama coincidence.

“Ilala katikati ya mji. Katikati ya mji somewhere humo, yaani ndiyo kuna Msajili… Ndiyo wakatupeleka na Ilala kutuonyesha site ambako jengo litajengwa, sasa lilikuwa adjacent na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mahala ambapo Mwalimu House iliko sasa hivi, kalikuwa ni kakiwanja, sikujua nani, ramani ya jengo litakuwa la muda gani, lakini ikawa site.

“Na Mama Sitta alikuwemo, na mara nyingi vitu ambavyo nilikuwa ninasaini huwa ninahitaji nibaki na nakala, lakini basi bahati mbaya tu,” amesema.

Alipoulizwa mbona kampuni inafanya biashara kubwa na fedha zinatolewa pasipo utaratibu, akasema: “Sasa kama ninamiliki mbona sina kitu? Sasa mbona sina kitu. Niko kwenye magugu shambani. Sasa niwe na kampuni ndi omunkeke, ndi omubishambu (nipo kwenye kwekwe, nipo kwenye magugu?)

JAMHURI linaendelea kufuatilia kwa karibu umiliki wa Kampuni ya TDCL na Benki ya Mwalimu ambavyo inaonekana kuna dalili walimu wanaandaa jambo zito iwapo mkutano mkuu wa kurekebisha Katiba ambayo ingeondoa upungufu wote hautafanyika haraka.