Nazungumzia daladala za Dar es Salaam. Kihistoria mpaka mwaka 1983 hakukuwa na mabasi ya abiria yaliyokuwa yakiitwa ‘daladala.’ Jina hili ‘daladala’ lilianza kutumika mwaka 1983.

Mwaka 1983 Dar es Salaam ilikuwa na magari machache ya abiria. Watu wengi wakawa wanachelewa kufika sehemu zao za kazi. Wakati ule magari hayo machache ya abiria yaliyokuwa yakitumika Dar es Salaam yalikuwa ya Kampuni ya Shirila la Umma la Usafiri Dar es Salaam (UDA).

Mwaka 1983 Waziri Mkuu wa Pili wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, alipoona wafanyakazi wanachelewa sehemu zao za kazi aliruhusu magari ya watu binafsi kuchukua abiria. Nauli ilikuwa shilingi tano ambayo enzi hizo iliitwa ‘dala.’ Mabasi nayo yakaitwa ‘daladala.’

Hakuna asiyekubali kwamba mabasi ya watu binafsi yamesaidia sana kupunguza tatizo la usafiri Dar es Salaam, lakini pia wakati huo huo mabasi haya binafsi mara nyingi yamesumbua wananchi kwa kukatisha safari. Hali hii inaendelea mpaka leo.

Mambo mawili hutokea mabasi yanayokatisha njia. Kwanza, abiria analazimika kupanda gari jingine na kulipa nauli zaidi. Pili, kama anakokwenda ni mbali na hana fedha za ziada mtu huyo analazimika kuendelea na safari yake kwa miguu.

Huko nyuma, askari wa Usalama Barabarani walifuatilia kwa karibu sana safari za mabasi. Mabasi yalipokatisha safari yalikamatwa, yakaadhibiwa.

Leo hali ni tofauti. Mabasi yanakatisha safari yapendavyo na hakuna anayejali. Hii ni kwa sababu askari wa Usalama Barabarani wameacha kudhibiti daladala. 

Leo daladala zinatangaza mwanzoni mwa safari zitaishia wapi! Utasikia pale Kariakoo, kondakta wa gari la Mwananyamala akitangaza wazi kabisa kwamba safari yao itaishia Ujiji au kwa Mama Zakaria na kwamba hawatafika Makumbusho.

Kwa kweli kuna shida. Asubuhi daladala za Mwananyamala zinazokwenda Posta na Stesheni zikifika huko zinageuza mpaka Ujiji au kwa Mama Zakaria. Hapo abiria atalazimika kutoa nauli nyingine anapopanda gari jingine ama asafiri kwa miguu mpaka Makumbusho.

Ikifika saa tisa alasiri, daladala za Mwananyamala zinazotoka Kariakoo huishia Ujiji ili kuwahi abiria wengine wa Kariakoo. Ninaamini kwamba hali hii mbaya haiko Mwananyamala tu bali pia ipo maeneo mengine ya Dar es Salaam.

Sababu yake moja kubwa ni kwamba leo askari wa Usalama Barabarani wanashughulika na magari madogo tu. Utakuta wapo hadi wanne eneo moja wakishughulika na magari madogo ya watu binafsi kando ya barabara kuu.

Wameacha kabisa kushughulika na daladala, kwa hiyo ni wazi hawatapata kwenda maeneo korofi mfano Mwananyamala, ili kujionea wenyewe jinsi wananchi wanavyosumbuliwa na daladala zinazokatisha safari.

Inatisha kuona kwamba daladala zinasumbua wananchi katikati ya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo haitaki kuona wananchi wakisumbuliwa.

Ni matarajio ya wananchi kuwa adha hii itaondolewa na kupatiwa huduma zinazowastahiki katika awamu hii ya Rais aliyejipambanua kupambana na unyanyasaji wa wananchi wa kipato cha chini. Askari nao watatimiza wajibu wao na kupambana na daladala hizi korofi.

By Jamhuri