Waliouza nyumba ya Serikali namba 162, kiwanja namba 1103 iliyoko Kitalu ‘S’ eneo la Mafiati jijini Mbeya kwa gharama ya Sh milioni 250 kwa mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, Saul Henry Amon, wamelalamikiwa kwa Waziri Mkuu.

Nyumba hiyo ambayo kwa sasa ina hatimiliki mbili, moja ikiwa imetolewa kwa mtumishi wa umma aliyeuziwa nyumba na Serikali ikiwa namba 11443-MBYLR iliyotolewa Oktoba 2007 baada ya kumaliza kulipa deni la nyumba hiyo na nyingine inayodaiwa kutolewa kwa mnunuzi huyo kwa njia ya mnada.

Simbonea Kileo amemweleza Waziri Mkuu kwamba nyumba yake aliyokopeshwa na Serikali kupitia Wakala wa Majengo (TBA) kwa mkataba namba 1531, lakini iliuzwa kiujanja na mazingira ya rushwa kwa mfanyabiashara huyo Julai 5, 2012 kwa amri ya Mahakama ya Mbeya Mjini baada ya ndoa yake kuvunjika mwaka 2007 kutokana na kutelekezwa na mkewe, Gladness Kimaro na watoto wake watatu tangu Januari 2001.

Kileo anasema kabla ya nyumba hiyo kupigwa mnada, alimjulisha Meneja wa TBA Mkoa wa Mbeya, ambaye alimshauri apeleke nyaraka zote zinazohusiana na kesi hiyo makao makuu ya Wakala wa Majengo jijini Dar es Salaam na kwamba baada ya kukabidhi nyaraka hizo Juni 2012 hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hadi nyumba hiyo inaporwa.

Anasema baada ya kuona hakuna hatua zozote zinazochukuliwa, aliomba ushauri kwa Mwanasheria wa Serikali ambaye alimshauri kupitia mwanasheria wa TBA kwamba afungue kesi dhidi ya mnunuzi wa nyumba ya Serikali kupinga uuzwaji wa nyumba hiyo.

Hata hivyo, kwa kuwa muda wa kukata rufaa ulikuwa umepita, alishauriwa na Mwanasheria wa Serikali kupitia Meneja wa TBA Mkoa wa Mbeya, aombe marejeo (revision) ya hukumu kujibu upungufu wa Mahakama kutotambua mkataba.

“Kwa upande wangu nilikuwa tayari nimefungua kesi ya kupinga mnada huo pamoja na kuomba marejeo. Kesi ya kupinga mnada huo ilimalizika kwa kufutwa kwa mnada huo na kuamriwa mnunuzi arudishiwe fedha zake.

“TBA hawajatekeleza ushauri waliopewa na Mwanasheria wa Serikali hadi sasa na sielewi kuna tatizo gani ingawa nilionana na mtendaji mkuu na kumfahamisha kila kilichojiri mahakamani yeye na meneja wa Wakala huo Mkoa wa Mbeya pamoja na kumpa nakala za hukumu.

“Nachelea kusema uongozi wa TBA unahusika katika uuzwaji wa nyumba hii kinyemela, kwani wamekaa kimya kama hakuna kilichotokea,” anaeleza Kileo katika barua aliyomwandikia Waziri Mkuu yenye kumbukumbu namba SGK/MBY/2016/01 ya Februari 27, mwaka huu.

Kileo anasema akiwa safarini alishangazwa na shauri hilo kuendeshwa kwa kasi ya ajabu ndani ya siku nane tu huku Wakili wake (Shitambala) akishindwa kuhudhuria mahakamani hata mara moja licha ya kumlipa gharama zote za kesi hiyo na hivyo kutolewa hukumu ya upande mmoja.

Pamoja na hilo anaeleza kwamba mawakili wake wanne akiwamo Shitambala, Mkumbe, Lwambano na Mary Mgaya kwa nyakati tofauti walijiondoa kwenye kesi hiyo bila taarifa huku akiwa amewalipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.

Kwa haraka aliyokuwa nayo Hakimu Seif Kulita, aliamuru nyumba iuzwe huku akijua hakuna nakala (Notice of Execution) iliyokuwa imetolewa na hivyo Mahakama ya Wilaya iliamuru watoto wagawiwe asilimia 45 ya mauzo na ndani ya jalada hilo kukiwa na hukumu ya Mahakama ya Mwanzo ambayo haijawahi kupingwa popote iliyoeleza kwamba watoto wote watatu wataendelea kuishi na baba yao.

Anasema alikata rufaa mara mbili kupinga hukumu ya upande mmoja na pia marejeo Mahakama Kuu kwa hati ya dharura kabla ya mnada Julai 5, 2012. Maombi hayo hayakufanyiwa kazi hadi Aprili 2015 yalipotupiliwa mbali na Jaji Mfawidhi Chocha na kuamuriwa alipe gharama.

Licha ya kupewa amri ya zuio na Baraza la Ardhi na barua kutoka TBA Mkoa wa Mbeya zikimtaka dalali Japhet Kandonga asiuze nyumba hiyo, yeye aliendelea na mnada uliozua mashaka kwani haukutangazwa.

“Nilipata ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu muda mfupi kabla ya mnada kwamba nyumba yangu itabadilika jina na kuwa Landmark, na baada ya ujumbe huo nilielezwa imeuzwa kwa Amon kwa Sh milioni 250,” inaeleza sehemu ya barua aliyomwandikia Waziri Mkuu.

Dalali wa Mahakama, Japhet Kandonga, alizuiwa na Meneja wa TBA mkoani Mbeya asiuze nyumba ya Serikali kwa kuwa ni kinyume cha taratibu na masharti ya nyumba zilizouzwa na Serikali kwa watumishi wake kwa barua ya Julai 4, 2012, lakini alikaidi maelekezo hayo.

Katika barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Meneja wa TBA, Mkoa wa Mbeya, Jaffari Kiyonga, inaeleza kwamba mkataba wa mauziano kifungu Na. 9 na 10 vinaeleza kuwa mtumishi yeyote aliyeuziwa nyumba za Serikali au mrithi wake hawaruhusiwi kuuza nyumba hadi hapo itapotimia miaka 25 kuanzia tarehe aliyopewa hatimiliki.

Pia barua nyingine ya TBA kwenda kwa Kileo iliyoeleza kuhusu ukiukwaji wa taratibu na masharti juu ya kuuzwa kwa nyumba za Serikali zilizouzwa kwa watumishi wake, inaeleza kwamba Wakala umepokea ushauri kutoka kwa Mwanasheria wa Serikali wakati hatua za kisheria kwa waliokiuka amri ya Mahakama zikifanyika kwamba ifungue kesi dhidi ya mnunuzi wa nyumba hiyo kupinga uuzwaji wake.

 

Dalali Kandonga

Kandonga alipohojiwa na JAMHURI kuhusu uuzwaji wa nyumba ya Serikali bila kuzingatia taratibu za mnada, anasema matangazo yalikuwa ya wazi na hakukuwapo na vificho kama inavyodaiwa kwamba aliwatafuta wanunuzi wanne tu.

“Kesi ilikuwa mahakamani na Mahakama ndiyo iliyotoa amri kwamba  nyumba hiyo iuzwe, hivyo nikaenda kuikamata na kuiuza na fedha zilipelekwa mahakamani na kugawanywa kwa wahusika kwa maelekezo yaliyotolewa,” anasema.

Anasema Saul alikuwa mnunuzi wa kwanza lakini alishindwa kulipa fedha hizo hivyo kwa maelekezo ya Mahakama aliuziwa mtu aliyeshika nafasi ya pili katika mnada huo. 

Alipoulizwa jina la mnunuzi wa pili wa nyumba hiyo alishindwa kumtaja na kukata simu. Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno uliomtaka ataje jina la mnunuzi huyo hakutoa jibu lolote.

Madai ya dalali huyo kwamba mnunuzi wa kwanza alishindwa kutoa fedha yanaibua mashaka makubwa katika uuzaji wa nyumba hiyo na kuibua maswali mengi, kwani hakuna kielelezo kinachomtaja kwa jina mnunuzi wa pili wa nyumba hiyo huku ikielezwa kuwa hakukuwa na mnada wowote uliotangazwa.

1175 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!