Wiki iliyopita Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, amewasilisha bajeti ya wizara yake kwenye mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma. Si nia yangu kujadili bajeti hii inayofikia wastani wa Sh bilioni 19. Na wala sitajadili danadana ilizopigwa bajeti hii, ambayo awali ilikuwa iwasilishwe Julai 18, lakini kwa mshangao ikasogezwa ghafla hadi Agosti 7, kisha kinyemela ikarejeshwa Julai 24.

Inawezekana ilikuwapo ajenda ya wazi iliyojikita katika kuvipiga chenga vyombo vya habari ambavyo wakuu wake wengi walikuwa Dodoma. Lakini pia, inawezekana kabisa kwamba kubabaika huko kulitokana na kuzama kwa mali ya MV Star Gate, ambayo wengi wanaiita MV Skagit. Yote haya yalizaa mkanganyiko ambao hatimaye ulivuruga si wanahabari tu, bali hata wahariri.

Kubwa zaidi na lililonisukuma kuandika mahala haya ni kuhoji nia njema ya Serikali. Kwa muda wa karibu miaka 11 umekuwapo mchakato wa kudai sheria mpya ya Uhuru wa Habari. Sheria hii mchakato wake ulianza mwaka 2002. Wadau wakiongozwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) waliitaka Serikali kupiga moyo konde ikawafikiria kwa kuhakikisha inaleta muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari, lakini si kwa sura ya hisani bali muswada huu uletwe kama haki.

Mwaka 2003 Serikali iliwaelewa wadau na kupitisha Sera ya Habari. Sera hii pamoja na mambo mengine inazitaja Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1973 na Sheria ya Utangazani ya Mwaka 1993 kuwa ni sheria mbaya. Kilichotokea walau ilielekeza kila wizara iwe na Afisa Habari. Rais Benjamin Mkapa aliifanya kazi hii kwa kuhakikisha maafisa habari wanateuliwa kwa kila wizara.

Mwaka 2006 Serikali ilileta ilichokiita Muswada wa Sheria ya Uhuru wa Habari (Freedom of Information Act). Muswada huu ulikataliwa na wadau kwa kuwa ulichanganya masuala mengi. Ndani ya Seria ya Habari yalijumuisha masuala ya watoto na mengine yasiyo na uhusiano na upatikanaji wa habari. Hapa wadau waliomba muswada huu utenganishwe.

Walitaka sheria hii itenganishwe iwepo Sheria ya Haki ya Kupata Habari na Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari. Sheria hizi mbili zinalenga katika kupambanua kati ya upataji wa Taarifa na Habari. Kwa kawaida taarifa si lazima ziwe habari. Hii inaweza kuwa ni utaratibu wa jinsi ya kuendesha mambo ndani ya Serikali watu kufahamishwa kwa mfano kiasi cha fedha za maendeleo zilizotengwa kwa ajili ya kata au vijiji vyao.

Tunapozungumzia habari, suala hili ni zaidi ya kutoa taarifa. Inaelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa kitaaluma katika kukusanya, kuchakata na kuchapisha taarifa. Kwamba hapa unahitajika weledi wa kufanya kazi hii. Si sawa na ile ya mwanzo ambayo mwananchi anakwenda kwenye mamlaka husika kuomba na kupatiwa taarifa zenye kugusa maisha yao tu.

Kwa huu muswada wa Sheria ya Huduma kwa Vyombo vya Habari, unalenga kuwapa fursa watu waliosomea kazi hii ya kukusanya, kuchakata na kuchapisha habari kuweza kuifanya. Hawa wanaitwa waandishi wa habari. Si kila mtu anaweza kufanya kazi hii. Kwa maana inalenga katika majukumu ya msingi matatu ya kukusanya, kuchakata na kuchapishwa. Mtu akienda kwenye halmashauri ya wilaya kujua Serikali Kuu imetoa fedha kiasi gani, taarifa hizi zinakuwa ni kwa ajili yake na si kuchapisha kwenye vyombo vya habari.

Mwaka 2007 Serikali ilitangaza kusikia kilio cha wanahabari na kuamua kuzigawa sheria hizi kwenye miswada miwili. Wazo la wadau ni kama nilivyoeleza hapo juu kupata Sheria ya Haki ya Kupata Habari na Huduma kwa Vyombo vya Habari. Badala yake Serikali iligawa muswada huu katika sheria mbili bila kubadili maudhui, bali kutenganisha tu walengwa.

Wadau wanachodai ni pamoja kuondokana na utaratibu wa sasa. Utaratibu wa sasa vyombo vya habari vinafanya kazi kwa hisani na huruma ya Rais Jakaya Kikwete, kwani sheria nilizozitaja bado zipo na ni mbaya. Sheria hizi zikimpata Rais dikiteta, anaweza kufunga vyombo vya habari karibu vyote hapa nchini.

Kwa mfano, Sheria ya Magazeti inampa haki na mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya Habari kulionya, kulifungia na au kulifuta kabisa kutoka kwenye orodha ya magazeti, gazeti lolote ambayo kwa maoni yake ni la uchochezi. Hakuna kigezo halali na kilichodadavuliwa juu ya nini maana ya uchochezi. Kuruhusu sheria ya aina hii kuendelea kuwapo ni sawa na kujenga nyumba katikati ya mbuga ya wanyama iliyosheheni simba wazee wasio na uwezo wa kuwinda digidigi kisha ukalala milango na madirisha yakiwa wazi.

Naamini inawezekana mpendwa msomaji unajiuliza sheria hii mpya itavisaidiaje vyombo vya habari kufanya kazi zake kwa uwazi na manufaa kwa jamii zaidi? Hapa nataka nitoe mifano michache kati ya mingi yanayoendelea hapa nchini.

Watanzania hatujapoteza kumbukumbu ya fedha za EPA. Kama si vyombo vya habari kupigia kelele suala hili, wakubwa hawa kina Farijali Maranda wasingekuwa gerezani.

Tumeshuhudia mkataba tata wa Richmond. Tumehudia kashifa ya Dowans. Tulishuhudia kashifa ya wabunge kupokea posho mbili. Tumeshuhudia kashfa ya rada. Tumeshuhudia Dk. Stephen Ulimboka akitekwa na kuumizwa vibaya. Tumeshuhudia mgomo wa madaktari. Tunashuhudia sasa mgomo wa walimu unaonukia. Tunashuhdia pia wafanyakazi wa sekta ya migodi wakiwa katika maandamano makubwa kupinga Sheria ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuzuia watu kuchukua mafao yao kabla ya kufikisha umri wa miaka 55.

Haya na mengine yanafanyika kwa hisani. Ikitokea wahusika wakakomaa mahakamani kwa sheria zilizopo magazeti yote yatalipishwa faini mpaka yafilisike. Radio na Televisheni wanaambiwa wasirushe matangazo zaidi ya asilimia 25 ya nchi, wakati teknolojia imekwishaifanya ipitwe na wakati.

Sitanii, kuna usemi usemao “Si aibu kutenda mambo ya aibu ila ni aibu kufahamika kuwa unatenda mambo ya aibu.” Kwa habari chache nilizozitaja kati ya nyingi zilizochapishwa na vyombo vya habari kama zisingechapishwa nchi hii ingekuwa inaendelea kutafunwa tu.

Ni kwa mantiki hiyo, tunasema ije sheria mpya ambayo kwanza itafuta mamlaka yaliyopitiliza mipaka aliyokasimiwa Waziri. Si hilo tu, sheria hii mpya tunayoidai inavilazimisha vyanzo ya habari kutoa taarifa pasi kificho wala kuzizuia. Kwa mfano, Afisa au Mkurugenzi ambaye nyaraka za EPA ziko mikononi mwake, sheria hii itamlazimisha kuzitoa kwa wanahabari kuzitangaza kwa masilahi ya jamii.

Afisa au Mkurugenzi husika asipofanya hivyo, atakuwa anahatarisha nafasi yake ya kuendelea kushikilia wadhifa huo na mwisho wa siku anaweza kufunguliwa mashitaka na mwanahabari anayetafuta habari husika. Hili nadhani ndilo wakubwa hawalipendi. Hawaipendi kwa maana itamwaga mboga.

Sitanii, sheria hizi zina masilahi zaidi kwa jamii kuliko kutokuwapo kwake. Dhana finyu inayotolewa kuwa heunda sheria hizi zikaathiri uhuru binafsi wa watu na usalama wa taifa. Mimi nasema wanahabari si vichaa. Na hata watunga sheria si vichaa pia. Haiwezekani tukafika mahala tukaandika kila kitu ikiwamo serikali ina risasi ngapi, bunduki ngapi au Waziri Mkuu akienda kuoga bafuni anaoga na nguo ua la!

Nimelisikia jibu la Waziri Mukangara anayesema muswada umefikia hatua nzuri kwa maana ya kuwa katika Kamati ya Baraza la Mawaziri. Hata hivyo, ingawa sitaki kutilia shaka maneno haya, tumeyasikia mara nyingi na siku nyingi zilizopita. Aliyekuwa Waziri wa Habari, Kapteni George Mkuchika, alipata kusema kuwa muswada huo anao kwenye mkoba mwaka 2007.

Mkuchika aliondoka, akaja Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye naye ameondoka akaja Mukangara, na sitashangaa hadithi ikibaki ile ile. Katika hili Rais Kikwete anapaswa kusimama kidege na kujenga historia isiyofutika. Kama alivyoamua kuingia kwenye vitabu ya historia kwa kuandika Katiba mpya, hii ni fursa pia kwa yeye kuandika historia nyingine kuwa ndiye aliyeruhusu Uhuru wa Habari nchini.

Sitanii, zimeanza kuibuka dhana hapa kwamba inaandikwa Katiba mpya hivyo Sheria ya Haki ya Kupata Habari na Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari nazo zitakuwa zimepata jibu. Nasema ndiyo, ila inahitajika Sheria kwani Katiba inatoa mwongozo na Sheria zinaelekeza jinsi ya kutenda mambo. Hata ikija Katiba mpya, bado tutawajibika kuwa na sheria yenye kutuongoza jinsi ya kutenda katika uandishi.

Napenda kuamini fursa hii haitapita. Wakati wa kutunga sheria mpya umewadia. Tunasema serikali yetu ni sikivu na imesaini mkataba wa kuwa wazi, hivyo sitarajii tumalize mwaka huu bila sheria mpya ya Haki ya Kupata Habari. Tunataka iitwe hivyo kwani haki ni rahisi kuidai kuliko uhuru.

1263 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!