LICHA ya Tanzania kumudu kulibakiza nyumbani Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati – maarufu zaidi kwa jina la Kagame – mshambuliaji wa Simba Sports Club, Felix Mumba Sunzu ameibuka kuwa galasa huku mashabiki wakijiuliza kuhusu sifa zinazofanya timu hiyo iendelee kumng’ang’ania.

Wakati Sunzu akigeuka galasa Mshambuliaji wa Yanga aliyeibuka msimu huu Bahanuzi yeye ameibuka shujaa kwa kupachika magoli wavuni katika mazingira yasiyotarajiwa na hivyo kuiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa CECAFA kwa mara ya pili mfululizo.

Goli alilofunga Saidi Bahanuzi kipindi cha pili liliiwezesha yanga kuizamisha Azamu FC 2 kwa 0 na hivyo kufuta ndoto za watengeneza lambaramba kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza katika historia yao, Mbali na Simba au Wekundu wa Msimbazi, timu nyingine za Tanzania zilizoshiriki michuano hiyo ni Mafunzo ya Zanzibar, na pia ilikuwepo Dar es Salaam Young Africans (Yanga) iliyofika fainali na kupambana na Azam Footbal Club, zote za Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita.

Timu nyingine zilizoshiriki michuano hiyo ukiziondoa Yanga, Simba, Azam FC na Mafunzo ni Wau al Salaam ya Sudan Kusini, Ports ya Djibouti, APR ya Rwanda, Atletico ya Burundi, URA ya Uganda, Tusker ya Kenya na AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) iliyoshiriki kama mwalikwa.

Katika mechi ya kwanza, Simba inayonolewa na kocha Milovan Cirkovic kutoka Serbia, ilichapwa mabao 2 – 0 na kikosi cha wakusanyaji wa kodi wa serikali ya Uganda, URA, huku Sunzu akipiga shuti moja tu la maana langoni mwa wapinzani wao katika dakika ya tano, lakini likapanguliwa kwa ufundi mkubwa na kipa Yassin Mugabi. Kuanzia hapo, mshambuliaji huyo wa kulipwa kutoka Zambia alidhibitiwa kisawasawa na beki aliyetemwa na Simba ileile, mwaka jana, Derrick Walulya na kushindwa kuonekana uwanjani kwa muda wote uliobaki na mechi zote zilizobaki pia alishindwa kuwa lolote au chochote dimbani.

Wachezaji pekee wa Simba walionyesha uhai siku hiyo ya kwanza ni Nkanu Mbiyavanga na Abdallah Juma. Hali hiyo ilimfanya hata Cirkovic akiri kuwa kukosekana kwa mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, Mganda Emmanuel Okwi ilikuwa ni simanzi, kilio kilichoungwa mkono na mashabiki mbalimbali, hasa baada ya kikosi hicho kuishia robo ya fainali baada ya kuchapwa na Azam FC kwa mabao 3 – 1.

Kabla ya kuanza kwa michuano hiyo Julai 14, Simba ilikuwa ikielezwa kwamba imefanya usajili wa watandazaji wakali wa kandanda kama vile Abdallah Juma, Nkanu Mbiyavanga, Danny Mrwanda, Mussa Mudde, Jonas Mkude, Masombo Lino, Kigi Makasi Kigi na Salum Kinje, lakini timu hiyo imekuja kuwachefua wengi na kutaka ifumuliwe yote. Kocha wake msaidizi ambaye pia ni kiungo wa zamani wa timu hiyo, Selemani Matola, anakiri wazi kwamba kutokuwepo kwa Kelvin Yondani aliyekwenda Yanga, ni tatizo lililoacha pengo kubwa katika safu nzima ya ulinzi.

“Nadhani hapa ipo haja ya kuisuka upya beki yetu na hii ni kazi hasa ya kocha mwenyewe”, anasema Matola na kukiri pia kuwa safu ya ushambuliaji nayo ni butu na ilikuwa ikiendelea kuonyesha udhaifu mkubwa kadri inavyocheza mechi zake, jambo ambalo linakubaliwa na watu wengine.  Hao ni pamoja na wale ambao wanaungana na kocha Cirkovic kumlilia Okwi, Yondani na marehemu Patrick Mafisango aliyefariki kwa ajali ya gari jijini Dar es Salaam, miezi michache iliyopita na kusema ni lazima zifanyike jitihada za makusudi kuziba mapengo hayo yote.

Pamoja na upungufu huo, Haruna Moshi ‘Boban’ ambaye ni kiungo mchezeshaji wa Simba, ndiye pekee aliyeng’ara kwa kiwango kikubwa zaidi. Karibu makocha wote kutoka nje waliokuwepo na timu zao jijini Dar es Salaam kusaka ubingwa wa Kombe la Kagame wanakiri kuwa mchezaji huyo ni bora.

Mwingine ni mchezaji bora wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Shomari Kapombe ambaye ndiye alifunga bao la kufutia machozi la Simba, Jumanne ya wiki iliyopita ilipofungashiwa virago na Azam katika mechi ya robo fainali. Ugalasa wa Sunzu dimbani, ulithibitika pia siku Simba ilipopambana na Ports iliyokuwa moja kati ya timu mbili dhaifu kuliko zote, nyingine ikiwa ni Wau al Salaam.

Mshambuliaji huyo aliongoza kukosa idadi kubwa ya mabao licha ya kushinda 3 – 0, mawili yakifungwa na Abdallah Juma huku straika huyo akizawadiwa kupiga penalti ili angalau kumpunguzia aibu.

Aidha, siku Simba ilipotoka sare ya bao 1 – 1 na AS Vita, Sunzu bado alionyesha udhaifu mkubwa kiasi cha kuwaudhi mashabiki waliokuwa wamelipa viingilio ili kuishangilia timu yao palepale uwanjani, na pia aliwakera hata waliokuwa wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni na redioni kutoka sehemu nyingine.

Katika mechi hiyo, ‘Boban’ aliyeingia kipindi cha pili akitokea benchi ndiye aliokoa jahazi la Simba lisizame. Alisawazisha bao kwa guu lake la kulia katika dakika ya 66, baada ya kuitumia kwa uhakika krosi iliyotumwa kwenda kwake kutoka kwa Mudde. Awali, timu hiyo ilikuwa nyuma kwa bao ililofungwa dakika ya 35 na Etikiama Taddy kwa penalti ya kuvutia. Beki Juma Nyosso alikuwa ameunawa mpira ndani ya eneo la hatari na kipa Juma Kaseja akashindwa kuonyesha umahiri wake wa kupangua mikwaju hiyo.

Ilipofika dakika ya 89, Simba ilipata nafasi ya dhahabu ya kushinda mechi hiyo. Mabeki wa AS Vita walijichanganya “ndani ya maguu 18” wakati wakijaribu kuokoa moja ya mashambulizi langoni kwao. Katika kufanya hivyo, mmoja wao aliuzuia mpira kwa mkono na mwamuzi akaona. Hapo ndipo Sunzu alipoitwa, akapewa jukumu la kupiga penalti hiyo ambayo hata hivyo ilipanguliwa kwa ujuzi mkubwa kabisa na kipa Lukong Nelson.

Madudu ya Sunzu pia yaliendelea hata siku ya robo fainali dhidi ya Azam iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa. Alishindwa kuonyesha kuwa kweli ni mchezaji wa kulipwa (professional footballer) kutoka nje ya nchi, hatua iliyosababisha baadhi ya mashabiki wahoji uhalali wake. Wengine walikwenda mbali zaidi kwa kuutaka uongozi wa Simba umtimue kama Yanga ilivyomtosa mshambuliaji mwingine kutoka Zambia, Davis Mwape.

Mathalani, mshambuliaji huyo alipewa mpira aliotakiwa auguse tu ili utumbukie wenyewe wavuni na kuiandikia Simba bao la pili katika dakika ya 70, lakini alishindwa kuunasa licha ya kuwa karibu nao mno. Aliteleza chini kama mtoto anayefanya mchezo wa kuigiza huku akiangukiana na kipa wa Azam, Deogratius Munishi ‘Dida’.  Kabla ya hapo, Sunzu alikuwa amekosa mabao ya wazi yasiyopungua matatu katika kipindi cha kwanza, yale ambayo kuna mengine alikuwa mzito kupiga mashuti au aliishia kuanguka.

Akabaki amekaa chini huku akihema utadhani kifaranga cha kuku kilichokoswakoswa na mwewe, kisha akatikisa kichwa chake na kujifanya kama mtu asiyeyaamini macho yake.  Ilipofika dakika ya 86, mshambuliaji huyo aliamua kuutumbukiza mpira wavuni ingawa tayari mwamuzi alishapiga filimbi ya kumwambia alikuwa kwamba ameotea, kisha akaenda mwenyewe kuuchukua ili ukapigwe kuelekea lango la timu yake ya Simba. Alizaliwa Mei 2, 1989 mjini Chingola, Zambia.

Kabla ya kusajiliwa Simba aliichezea kwa mkopo timu inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza kwa vilabu vya kulipwa nchini Tunisia, AS Marsa.  Kutoka huko alikwenda LB Chateauroux ya Daraja la Pili ya Ufaransa nako kwa mkopo, kisha akarudi AS Marta pia kwa mkopo. Ameichezea mechi 14 timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo), akaifungia mabao manane kabla hajatemwa kwa kushuka kiwango.

Julai 25, 2011 alisajiliwa Simba kwa dola 35,000 za Marekani, kiasi cha Sh 55,300,000 za Kitanzania akitokea Al Hilal ya Sudan, hivyo kuwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi zaidi na klabu hiyo.  Baba yake mzazi, Felix Sunzu Sr ni kipa wa zamani wa Konkola Blades na mdogo wake, Stophira Sunzu ni beki wa Chipolopolo na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa sasa. Kwa matokeo ya fainali ambapo Yanga ilishinda 2 bila, Inadhihirisha kuwa watani wao Simba wamekosa uhondo na pengine inaweza kusemwa kuwa wameanza vibaya msimu huu.

By Jamhuri