Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) limetangaza kuhamia rasmi katika mfumo wa malipo wa serikali (GePG).

Hatua hii imekuja baada ya kumalizika kwa mkataba na kampuni mbili za malipo ya kidijitali za Selcom na Maxcom waliokuwa wakikusanya malipo kwa niaba ya Dawasco.

Kwa mujibu wa Dawasco, mfumo huo utaokoa jumla ya shilingi 2.4 bilioni iliyokuwa inalipwa kwa wakala kila mwaka kama gharama za huduma mtandaoni.

Inakadiriwa kuwa DAWASCO hukusanya kiasi cha shilingi 1 bilioni kila mwezi kama gharama ya utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi, ambayo ni sawa na shilingi 12 bilioni kila mwaka.

“Tumeufurahia mfumo huu wa malipo wa serikali kwani utaongeza ufanisi na malipo yatakuwa yanafika moja kwa moja kwetu, tofauti na awali ambapo iliweza kuchukua hadi wiki moja kwa malipo kutufikia,” alisema Mkurugenzi wa Dawasco, Cyprian Luhemeja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kwua katika mfumo huu, malipo yatalipwa kwa kutumia namba 12 maalumu ambazo wateja wake watapewa.

Ameongeza kuwa kupitia mfumo huu, gharama ya utoaji wa huduma ambayo ni asilimi 1, italipwa na mteja mwenyewe.

Alidai kuwa malipo yatafanyika kupitia mitandao ya simu na kuongeza wanatarajia kuwepo kwa changamoto lakini mambo yatakuwa sawa kadiri siku zitakavyokwenda.

2189 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!