DC ampa ardhi aliyechoma  moto nyumba za wananchi

*Mwenyewe adai alipewa eneo hilo na Sokoine mwaka 1983

KIBAHA

Na Mwandishi Wetu 

Wananchi wa Lupunga, Kibaha mkoani Pwani wamepigwa butwaa baada ya mwekezaji aliyewachomea moto makazi yao kuthibitishwa kuwa ndiye mmiliki halali wa eneo hilo.

Wakazi hao, wengine wakiwa ni vikongwe wenye umri wa zaidi ya miaka 80, walikuwa wakiishi eneo hilo tangu kabla ya Uhuru hadi walipofukuzwa na nyumba zao kutiwa kiberiti na anayejiita mwekezaji, Tariq Ahmed, aliyeongozana na askari pamoja na vijana wake.

Sakata hilo sasa limechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri, kuelekeza kuwa eneo lililokuwa likidhaniwa kuwa mali ya wanakijiji ni mali ya Tariq.

Sara anasema amejiridhisha baada ya kupitia nyaraka kadhaa zilizotolewa na Tariq mbele ya wanakijiji, ikiwamo hati ya kumiliki eneo linalodaiwa kuwa na ukubwa wa ekari zaidi ya 1,000.

Akizungumza katika mkutano na wanakijiji wa Lupunga, awali Sara alisema yupo pale kuwasalimia na kusikiliza kero zao, likiwamo suala la Tariq kudaiwa kuvamia eneo la kijiji na kufanya uharibifu wa mali.

“Tariq, kama ni wananchi (vijana) wako wamechoma moto nyumba, mashamba au kuchoma nini sijui, haijalishi. Uhalali ni wako.

“Kuchoma nyumba au shamba au kufyeka mazao si jukumu lako kama mwekezaji. Ukivamiwa toa taarifa kwangu. Vipo vyombo vya sheria. Kuchoma au kuharibu mali ni kosa kisheria,” anasema Sara akimwelekeza Tariq aliyekuwapo kwenye mkutano huo.

Hati aliyoionyesha DC inadaiwa kuwa Tariq alimilikishwa eneo mwaka 1983 wakati wa nguvu kazi na kulisajili mwaka 1986 kwa jina la Lupunga Farm Limited, kwa ajili ya kilimo na ufugaji.

Sara ametoa maagizo kwa viongozi wa kata kushirikiana na wananchi kukagua shamba la Tariq kuona iwapo ameliendeleza kama alivyoomba, kisha wampelekee taarifa.

Viongozi wengine wamshangaa Tariq 

Tariq, ambaye amekuwa akikaidi wito wa viongozi wa kata na kijiji mara kwa mara, amewashangaza wengi baada ya kuibuka kwenye mkutano wa DC akiwa na nyaraka.

Akizungumza mkutanoni hapo, mwekezaji huyo anasema amefuata taratibu zote za kumiliki eneo hilo analodai kupewa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine. 

“Sikuliendeleza kwa kuwa nilikuwa nje ya nchi. Nilirudi mwaka 1996 na kuanzisha Lupunga Farm Limited pamoja na ndugu yangu.

“Mwaka huu watoto wa ndugu yangu walitaka kugawiwa ardhi ndipo tulipokuja hapa,” anasema Tariq mbele ya DC. 

Akizungumzia mgogoro huo, Diwani wa Kikongo, Asha Jongo (Viti Maalumu), anasema umedumu kwa muda mrefu huku Tariq akigoma kuitikia wito wa viongozi mbalimbali waliotaka kuusuluhisha.

“Akiambiwa alete nyaraka ofisini au kwenye mikutano ya wananchi ili wanakijiji wajiridhishe, hataki. Leo wananchi wanashangaa kumuona akileta hizo nyaraka,” anasema Asha.

Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Brown Nziku, anasema nyaraka alizonazo ni halali na zilitolewa na wizara kama ofa mwaka 1986.

Anasema awali alitakiwa kufanya kilimo cha mkonge lakini baadaye mwaka 1987 akapata hati kwa ajili ya matumizi ya kilimo na mifugo.

“Ana hati ya umiliki ya miaka 99, yupo kwenye nyaraka zetu wilayani na kwenye mifumo ya walipa kodi. Analipa kodi kila mwaka,” anasema Nziku.

Anasema kwa mujibu wa sheria, kijiji hutoa ardhi yenye ukubwa wa ekari 50, na ikizidi hapo (eneo la Tariq lina ekari 850) mamlaka yanahamishiwa halmashauri ya wilaya na kwamba katika suala hilo, ilibidi kamati ya kugawa ardhi ya kitaifa ndiyo itoe uamuzi.

“Kuna hati ya Kamishna wa Ardhi na sasa nyaraka zote zipo kwenye majalada yetu japokuwa haikufuata utaratibu,” anahitimisha Nziku kwa kauli yenye utata kwa wanakijiji.

Kamishna wa Ardhi anasemaje?

JAMHURI limemtafuta Kamishna wa Ardhi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia kwa Ofisa Habari wa wizara hiyo, Lusajo Mwakabuku.

Mwakabuku ameliambia JAMHURI kuwa suala la ardhi ya Lupunga ameliwasilisha kwa Kamishna wa Ardhi na kuongeza:

“Mamlaka ya upangaji ardhi yapo chini ya manispaa au halmashauri husika. Ni wao ndio hupanga matumizi na si wizara wala kamishna. 

“Mchakato wa utoaji hati huanzia halmashauri. Wizara inapelekewa mapendekezo na kusimamia utekelezaji.”

Asili ya mgogoro na utata wa Tariq

Septemba 27, mwaka huu, Tariq akiandamana na askari Polisi wamechoma moto nyumba na mashamba ya wanakijiji, wakachukua na kuondoka na mali mbalimbali na kuwasababishia hasara kubwa.

Mkazi mmoja, mzaliwa wa Lupunga, Saidi Pazi (80), anasema maisha yake yote ameishi hapo na familia yake kabla ya ‘uvamizi’ wa Tariq.

“Mwaka 1983 alikuja mtu mmoja anaitwa Abdallah mwenye asili ya Kiarabu, akaomba sehemu ya kufanya makazi. Wanakijiji tukaridhia ugeni huo na wala yeye hakuwa mtu wa kwanza kuomba sehemu ya kufanya makazi,” anasema.

Eneo hilo kuna Watanzania wengi wenye asili ya Kiarabu wanaoishi pamoja na wazawa kama ndugu.

Mzee Pazi anasema Abdallah alilima eneo alilopewa bila kupanda kitu.

“Baada ya Abdallah kufariki dunia, akaja mtu mmoja (Tariq) na kujitambulisha kama mdogo wa marehemu. Akataka aonyeshwe mipaka ya eneo la kaka yake. Tukamwonyesha. 

“Lakini sasa amebadilika na anakuja kwa dhuluma, akitumia nguvu kutunyang’anya maeneo yetu tofauti na eneo ambalo kaka yake alipewa na kijiji. Anachofanya sasa ni dhuluma kwa wananchi,” anasema mzee Pazi.

Akizungumza na JAMHURI, Shomari Msasalo, ambaye pia ni mwenyeji wa kijijini hapo, anasema eneo linalogombewa ni mali ya babu yake, anayemtaja kwa jina la Msasalo.

“Hatujawahi kumuuzia mtu na humu kuna makaburi ya asili. Ni eneo letu la maziko.

“Alipokuja hapa Abdallah, kaka yake Tariq mwaka 1983 kuomba eneo la kuishi, tulimpa ekari nne tu,” anasema Shomari, aliyezaliwa mwaka 1942.

Anasema wazazi wake na mababu wote wamezaliwa hapo na kuzikwa hapo hapo, akisema mipaka ya eneo asilia la Abdallah ipo wazi na inafahamika.

Shomari anasema ujio wa Abdallah kijijini hapo ulipokewa kwa furaha na wanakijiji kiasi cha hata kufanya sherehe za kumkaribisha.

Anasema mambo yalibadilika baada ya kifo cha Abdallah na ujio wa mdogo wake aliyeamua kwa makusudi kutotambua mipaka ya eneo la kaka yake.

“Ameingia katika mashamba ya wanavijiji na kuyapora, akisema maeneo yote ni yake! Hii si kweli. Na bahati mbaya akiitwa alete nyaraka kuhalalisha umiliki wake, hataki!

“Haiwezekani hata makaburi ambayo mimi nimezaliwa na kuyakuta kuwa leo yapo kwenye eneo lake. Ndiyo maana tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie kwa sababu hakuna hata kiongozi mmoja aliyewahi kuja kusikiliza matatizo yetu,” anasema Shomari.

Sasa wanakijiji wanaomba uongozi wa wilaya au mkuu wa wilaya wa zamani (wanamtaja jina) waende kuthibitisha mauzo ya eneo hilo kwa Tariq.

Tatu Mbegu, mwanamke na mkazi wa kijiji hicho, anasema: “Mimi ni mmoja wa wanawake walioathiriwa na kutiwa umaskini na Tariq.

“Siku ya tukio (la mashamba na nyumba kuchomwa moto) Tariq alikuja na askari wenye bunduki pamoja na vijana wake, wakabomoa na kuiba kuku wangu, magodoro na vitu vingine vingi. 

“Kwa kweli menitia umaskini mkubwa na sasa watoto wa shule hawana vitabu! Tunalala kwenye vibanda kama wakimbizi.”

Anasema siku ya pili, Tariq akiwa na wajukuu wake alikwenda tena kijini hapo kuwaonyesha wajukuu wake eneo analodai ni la kwao.

“Wakati sisi na watoto wetu tunataabika, yeye akawa anawaambia wajukuu wake; ‘mmeona eneo lenu? Ni hili lote.’ Kisha akaja kwetu na kutamba akitutaka kuondoka katika eneo lake.

“Tunaomba serikali ije kusawazisha mgogoro huu vinginevyo atakapokuja tena kuvunja nyumba zetu tutalazimika kujipanga na kumzuia,” anasema Tatu.

Polisi Pwani haina taarifa

JAMHURI limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, kutaka kufahamu iwapo jeshi hilo lina taarifa za kuwapo kwa suala hilo.

Afande Nyigesa anasema hana taarifa zozote kuhusu tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Butamo Ndalahwa, anasema wakati taarifa zikifikishwa ofisini kwake, hakuwapo.

“Hata hivyo mimi na timu yangu tutakwenda huko kumaliza suala hilo,” anaahidi Ndalahwa.

Umiliki wa Tariq eneo hilo pia unakanwa na Mtendaji wa Kata, Palekege Jailos, akisema ofisini kwake hakuna taarifa za Tariq kumiliki eneo hilo.

“Nilipozungumza naye aliniambia eneo hilo alipewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati hakukuwa na uongozi wa serikali,” anasema Palekege.

Palekege anasema baada ya uharibifu wa mali za wananchi kufanyika, aliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya lakini hadi alipozungumza na JAMHURI hakuwa amepata majibu.