Na Deodatus Balile, Bukoba

Mwezi mmoja uliopita niliandika makala iliyoamsha hisia katika viunga vingi vya nchi hii. Nilizungumzia ukuaji wa deni la taifa. 

Nilitumia takwimu za Benki Kuu kukokotoa ukuaji wa deni na kuonyesha kuwa limefikia Sh trilioni 78 sasa. 

Mada hii imekuwa moto mno. Imejadiliwa hadi bungeni. Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, akatoa mchango wake bungeni na kutaka ufanyike uchunguzi katika akaunti ya deni la taifa.

Sitanii, hoja ya msingi katika makala ile ilikuwa ni kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ilikopa mikopo ya kibiashara ambayo inaiva kabla ya miradi iliyokopewa kuanza kufanya kazi. 

Makala hii imenionyesha sura halisi za Watanzania. Ni bahati mbaya kuwa Watanzania walio wengi hawauishi ukweli, bali wanaishi kama mianzi.  

Upepo ukivuma kutoka kaskazini kwenda kusini wanainama kufuata mkondo wa upepo. Ukitoka mashariki kwenda magharibi, hali kadhalika!

Kuna shida kadhaa nimepata jinsi mjadala ulivyokuwa unaendelea. Wapo wayumbaji ambao walishinda kwenye mitandao wakitetea uongozi wa Rais John Magufuli si kwa hoja, bali kutetea heshima. 

Ila ninajua walichokuwa wanatetea mno. Aliwateua, hivyo lazima ikibidi waufumbie macho ukweli. Tena wengine wakafanya mbinu za kutenganisha deni la taifa na deni la serikali. Wengine wakaona ni fursa ya kunishushia matusi mimi na taaluma ya uandishi.

Nikasikitika kuona hata baadhi ya makandarasi wanaojenga madaraja na barabara zikabomoka ndani ya miezi mitatu, wakaonyesha hamu ya kufanya kazi ya uandishi wa habari. Wakiamini wanaweza kuandika vizuri habari kuliko waandishi. 

Wengine wakanishushia rungu kuwa kwa “elimu yangu ya kujua kusoma na kuandika tu” sina ujuzi wa kuchambua uchumi.

Sitanii, nimepitia fikra na mtazamo wa wengi waliochangia wakiwamo madaktari wa falsafa, nilichobaini ni kuwa badala ya kujadili hoja, waliiona hiyo kuwa na fursa ya kujipendekeza. Kumhakikishia Rais Samia kuwa deni ni himilivu na mtangulizi wake hakukopa sana. Lakini hao hao ndio wanahoji kwa nini Rais Samia ametangaza hadharani matumizi ya mkopo wa Sh trilioni 1.3 alizokopa IMF, kitu ambacho hakijawahi kuwapo tangu Uhuru. 

Rais Hussein Mwinyi naye ametangaza hadharani matumizi ya dola milioni 200 ilizokopa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Ninamshukuru Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba, kuwa wakati anahitimisha hoja ya Nape, alisema serikali ya Rais Samia haijakopa mkopo wa kibiashara hata mmoja. 

Akaongeza kuwa kwa mikopo ya kibiashara iliyoiva na yenye masharti yanayoleta ugumu kidogo, serikali itaangalia na kufanya utaratibu wa ‘refinancing’, kwa maana kuwa itakopa mkopo wa masharti nafuu (concessional loans), kisha ilipe hiyo yenye masharti magumu, na maisha yaendelee. 

Ninafurahi amethibitisha hoja yangu niliyoiibua baadhi wakaipotosha. Mikopo itaendelea kuwapo, ila serikali haipaswi kukopa mikopo ya kibiashara kama ilivyofanya serikali iliyopita. Ni hatari.

Kuna jambo hapa ninaomba niliseme. Hapa duniani kuna taaluma mbili tu, ambazo kila anayepata tatizo huzikimbilia kupata ufumbuzi; Uandishi wa Habari na Uanasheria. 

Taaluma hizi zimetamkwa hadi kwenye maandiko matakatifu. Baadhi ya watu nchini kushindwa kuzithamini na kuzidharau kwa kiburi cha kada walizosomea, ni bahati mbaya ya aina yake. Kinachonipa shida zaidi, wanatamani kuifanya kazi ya uandishi, ila hawaonyeshi taaluma   walizosomea ‘wamezitendea haki’ kwa ufanisi wa kiwango gani.

Sitanii, kwa sasa tuna mjadala wa mgawo wa maji, huku mgawo wa umeme ukinukia kutokana na ukame ulioikumba nchi. 

Ninasikitika kuwa ninaposoma mijadala mingi inayoendelea, hakuna mjadala unaojielekeza katika kupata ufumbuzi wa tatizo. 

Tunaishia kusikia watu wakilaani kuwa ilikatwa miti milioni 1.5 kujenga Bwawa la Nyerere na kwa kushangilia wanasema tunavuna tulichopanda.

Wanasema miti iliyokatwa utengenezaji wa mawingu umekuwa tabu na sasa mvua hazinyeshi na kama kushangilia vile, wanasema mito itakauka na bwawa lenyewe halitajaa maji ili kuzalisha hizo Megawati 2,115 za Stiegler’s Gorge. 

Mimi ninadhani kama Watanzania tunapaswa kuwaza na kuamua kipi tunataka, iwapo tunataka maendeleo ya kweli. Na tukumbuke kuwa mradi huu umekwisha kutumia fedha zetu nyingi. Iwe mtu uliuunga mkono au la, ni lazima tumalizie. Tukiuacha hapa ulipo, tutabaki kuwa kichekesho cha mwaka duniani. Mungu apishe mbali.

Maendeleo ni gharama. Hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana kirahisi. Kama nchi tunapaswa kufanya uchaguzi, kati ya kuhifadhi miti ambayo tunaandikiwa majina yake na Wazungu kwa Kilatini, tukaelezwa kuwa kitaaluma unaitwa… Wazungu ambao kwao katika majiji kama London, New York, Nice, Tokyo, Beijing hakuna msitu hata mmoja, kwani walikata miti yote wakatengeneza faida na sasa wanakula gawio. Tuchague kati ya misitu na kupata umeme wa bei rahisi.

Inawezekana tunaliangalia hili kwa mtazamo upi. Kupanga ni kuchagua. Ni kweli wakati wa ukame umeme wa maji unaingia katika msukosuko, lakini wakati wa masika, nchi inavuna umeme wa bei rahisi mno. 

Kwa hiyo, mimi ninawaza kuwa tuwekeze tu katika umeme wa gesi, upepo, makaa ya mawe na vyanzo vingine, ambao utatumika wakati wa kiangazi.

Jambo jingine, tunapaswa kufahamu kuwa nchi zilizoendelea zinatumia umeme kuanzia megawati 30,000 kwenda juu. 

Kwa mantiki hiyo, kila chanzo kinachoweza kuongeza umeme katika gridi ya taifa, tunapaswa kukipa nafasi. 

Hatuwezi kumiliki viwanda na mitambo mikubwa ya kuzalisha bidhaa zitokanazo na chuma kwa kuendelea kuwa na umeme wa megawati 1,500.

Suala la maji, huko nako mimi sitaki kulalamika. Rais Samia kama alivyokopa Sh trilioni 1.3 za miradi inayotikisa nchi kwa sasa, ninaamini ni suala la kujenga hoja. 

Hawezi kushindwa kuandika hii historia. Kama nchi tuseme vipaumbele vyetu. Mfano tuseme tunajenga bwawa kubwa la maji litakalotupatia ufumbuzi wa kudumu. Kuna hili Bwawa la Kidunda, ninaendelea kulifanyia kazi kufahamu gharama halisi na faida yake.

Sitanii, ifike mahala kama nchi tuwe tunasema sasa tunamaliza tatizo la umeme, basi tulimalize milele. Tuseme tunahama kutoka kusafirisha mizigo kwa barabara na kwenda kwenye reli, tujenge reli iishe bila kupigia debe madalali. 

Tusema tunajenga hifadhi ya maji, tulimalize kama Rais Samia alivyoona mahitaji ya madarasa ni 11,000 nchi nzima kwa sasa, akaamua tujenge madarasa 15,000 ya sekondari.

Ninahitimisha makala hii kwa kusema, maendeleo hayajawahi kuja kwa lelemama. Ni lazima tufanye uamuzi mgumu. Tusikubali kuendelea na maandiko yanayotokana na utafiti uliofanywa na Wazungu pekee. 

Wazungu waliotwambia Tanzania haina gesi ya kuzalisha kibiashara miaka ya 1960 na sasa tunajua wingi wa gesi iliyopo. 

Wazungu wanaotufadhili mashimo ya vyoo shuleni, wakatukataza miradi mikubwa kama kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe na vyanzo vingine, huku sisi tukitumia misitu yetu kusafisha gesi ya ukaa chini ya Kyoto Protocol. Akili ya kuambiwa, changanya na ya kwako.

361 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!