Katika toleo lililopita la gazeti hili, miongoni mwa habari zilizoripotiwa kwa ukubwa wa pekee ilihusu kifo kinachoikabili Hifadhi ya Taifa Serengeti (Senapa).

Habari hiyo ilikuwa na picha zilizoonesha makundi ya ng’ombe wakiwa ndani ya Hifadhi; na alama za mipaka zilizo katikati ya mashamba. Kulikuwa na picha zikiwaonesha mbwa wanaoua kondoo baada ya kukosa wanyamapori; na picha za mabanda ya wafugaji jirani na mengine ndani ya Hifadhi hiyo maarufu duniani.

Kama ilivyotarajiwa, wanasiasa ni kundi lililobainika kuwa na mchango mkubwa katika kuiua Serengeti na maeneo mengine ya uhifadhi nchini mwetu.

Wanasiasa hao, ama wao wenyewe wamekuwa na mamia kwa maelfu ya mifugo, au wamekuwa wakiwatetea wananchi kama mbinu ya kutaka waendelee kupendwa na hivyo kuchaguliwa.

Tunaandika haya kwa uchungu kutokana na hatari inayoikabili Serengeti na maeneo mengine kama vile Pori Tengefu la Loliondo ambalo ni mhimili muhimu mno katika ikolojia ya Serengeti-Masai Mara.

Kwa miaka mingi utalii nchini mwetu umefanikiwa kutokana na wanyamapori na viumbe vingine kwenye maeneo yetu ya uhifadhi.

Ni jambo la kushangaza sasa kuona mapori yakivamiwa na kuharibiwa ilhali viongozi wetu wakiwa wanashuhudia.

Wakoloni waliotutawala walilinda kwa nguvu zote rasilimali hizi, hivyo ni jambo la ajabu kweli kweli kwa Watanzania wenyewe sasa kuwa chanzo cha kutoweka kwa urithi huu.

Wizara ya Maliasili na Utalii ishirikiane na wadau wengine kama vile Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, pamoja na TAMISEMI kuhakikisha kuwa watu wanaheshimu mipaka.

Suala la uhifadhi lisiwe la kumbembelezana. Liwe ni la kufa au kupona kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za uhifadhi vinazingatiwa.

Hiki kinachoendelea Serengeti ni aibu kwa taifa, hasa kwa viongozi wetu waliogeuka kuwa watetezi wa waharibifu wa mazingira na uhifadhi.

Kila mmoja wetu ajione ana wajibu wa kulinda rasilimali hii ili kizazi kijacho kiifaidi.

Siasa iwekwe mbali kwa sababu inawafanya watumishi waadilifu wa rasilimali hizi kukosa nguvu za kusimamia sheria na kanuni za uhifadhi.

Kwa pamoja tuamini kuwa kifo cha Serengeti na uhifadhi kwa jumla nchini mwetu, si tu ni fedheha na aibu kwetu, bali ni pigo kwa wapenda uhifadhi duniani kote. Tusichelewe, tuanze sasa kuyaokoa mapori na hifadhi zetu.

By Jamhuri