Umepata kujiuliza vipi utamtambua Muislamu anayeutekeleza Uislamu? Unamtambua Muislamu kwa kuvaa kanzu na kofia? Yumkini, lakini kuvaa kanzu na kofia si sifa bainifu ya kumtambua Muislamu kwa kuwa kanzu na kofia ni vazi tu lenye asili ya jamii mbalimbali kwa mitindo mbalimbali na kwa hakika halina uhusiano na dini.

Unamtambua Muislamu kwa kuitwa majina kama vile Abdallah, Twariq, Abbas, Khamis, Jumaa, na kadhalika? Inawezekana, lakini majina haya si sifa bainifu ya kumtambua Muislamu kwa kuwa majina haya ni majina yatokanayo na lugha ya Kiarabu tu na hayana uhusiano wowote na dini ya Uislamu. Majina wanayopewa watu ni utambulisho unaotokana na vilivyomo katika mazingira ya watu hao kwa kutumia lugha zao.

Isingewezekana kabla ya mwingiliano mpana baina ya jamii mbalimbali duniani kwa mzungu kumpa mwanawe jina ‘Achimwene’ wakati neno hilo halipo katika lugha yake; Mhindi kumwita mwanawe ‘Livingstone’ wakati neno hilo halimo katika lugha yake; Muarabu kumwita mwanawe ‘Ghandi’ wakati neno hilo halimo katika lugha yake; na ndivyo hivyo hivyo ingekuwa muhali kwa Mmakonde kumwita mwanawe ‘Twariq Aziz’ wakati si katika msamiati wa lugha ya Kimakonde.

Utamtambuaje Muislamu anayeutekeleza Uislamu? Sifa pekee bainifu ya kumtambua Muislamu ni kule kujipamba kwake kwa tabia njema. Uislamu ni tabia njema, si mavazi maalumu wala majina ya Kiarabu.

Tabia njema ni miongoni mwa makusudio muhimu ya kuletwa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) na ndio maana hata Mwenyeezi Mungu amethibitisha ndani ya Qur’aan Tukufu kiwango cha juu cha tabia njema alichokuwa nacho Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani).

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 68 (Surat Al-Qalam) Aya ya 4 kuwa: “Hakika wewe (Muhammad) una tabia njema mno (tabia tukufu)”.

Mwenyeezi Mungu Mtukufu anaelezea neema zake kwa waumini kwamba amemtuma Mtume wake ili awafundishe Qur`ani na awawafundishe kuzitakasa nafsi zao. Kutakasa nafsi kuna maana ya kuusafisha moyo usiwe na ushirikina  na tabia mbaya, kama vile chuki, husda, hiyana, choyo, unafiki na pia kujisafisha na kujiweka mbali na desturi na tabia mbaya kwa kauli na vitendo.

Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema kuwa: “Hakika, si vingine nimetumwa (nimepewa utume) kuja kutimiza tabia njema”.Hivyo, tunaona hapa kuwa mojawapo ya sababu muhimu sana za kuletwa kwa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) ni kuboresha na kuendeleza tabia njema na maadili bora ya mtu mmoja mmoja na jamii. 

Tabianjema ni sehemu muhimu ya Imani na Itikadi ya Muislamu. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alipoulizwa kwamba: “Ni muumini gani aliye bora zaidi katika imani?” Alijibu kuwa: “Ni yule mwenye tabia nzuri sana miongoni mwao”.

Mwanadamu katika maisha yake ana uhusiano wa aina mbili: uhusiano kati yake na Mola wake Muumba na uhusiano kati yake na viumbe alivyoviumba Mola wake Muumba wakiwamo wanaadamu. Tabia njema ina nafasi kuwa katika huu uhusiano wa mwanaadamu na viumbe wengine wakiwamo wanaadamu wenzake na kwa hakika kufanya vibaya katika uhusiano huu wa kati yake na viumbe wenzake kunahatarisha na kuharibu mafanikio yake katika uhusiano wake na Mola wake.

Ndipo utakapoona hata ibada azifanyazo Muislamu zinakusanya namna ya kumtengeneza katika kujipamba na tabia njema na kuziepuka tabia mbaya.

Unapoiangalia kwa mazingatio ibada yoyote katika Uislamu utakuta kuwa makusudio yake yanagusa tabia na maadili au athari ya ibada hiyo kitabia na kimaadili kwa mtu mmoja mmoja na kwa jamii. Tuangazie mifano michache: 

(1) Swala: Ibada hii ya Swala inamtengeneza Muislamu kukatazika na mambo machafu na maovu kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 29 (Surat Al-Ankabuut) Aya ya 45 kuwa: “Na simamisha swala. Kwa yakini, swala inakataza mambo machafu na maovu”.

Hivyo, ikiwa Muislamu anatekeleza ibada ya Swala Tano, lakini hajakatazika na kuyaepuka mambo machafu na maovu, basi huyo Swala haina athari chanya kwake.

(2) Zakah: Unapoiangalia ibada ya Zakah utaona kuwa pamoja na kwamba uhalisia wa Zakah ni kuwafanyia hisani watu na kuwasaidia, lakini pia inamrekebisha mtu na kumtakasa asiwe na tabia mbaya. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 9 (Surat At-Tawbah) Aya ya 103 kuwa: “Chukua kutoka katika mali zao Zakah, uwasafishe na uwatakase kwa Zakah hiyo”.

(3) Swaumu: Ibada ya Swaumu inalenga kumfikisha Muislamu katika kumcha (kumuogopa) Mwenyeezi Mungu kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 2 (Surat Al- Baqarah) Aya ya 183 kuwa: “Enyi mlio amini, mmeandikiwa kufunga swaumu, kama ilivyoandikwa kwa wale walio kuwepo kabla yenu, ili mpate kuwa wenye kumcha (kumuogopa) Allah”.  

Lengo ni kumcha Allah kwa kutekeleza maamrisho yake na kuepuka makatazo yake. Kwa sababu hiyo, Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Mtu ambaye hakuacha uongo na kuufanyia kazi uongo, Allah hana haja kwa mtu huyo kuacha chakula chake na kinywaji chake”.

Mtu ambaye funga yake haikumuathiri yeye mwenyewe na tabia zake katika kuishi na watu wengine, hakulifikia lengo la kufunga swaumu.

Utaona hapa kuwa ibada unayoifanya kama haikutengenezi kuwa mtu mwenye tabia njema na uliye mbali na kila aina ya tabia mbaya, basi huna sababu ya kujifakharisha kwa Uislamu wa aina fulani ya mavazi au majina yadhaniwayo kuwa majina ya Kiislamu wakati Uislamu hauna majina maalumu ya lugha fulani, bali umesisitiza majina mazuri. Yaani si vyema mtoto ukamwita majanga, shida, matatizo na kadhalika.

Ni vyema tuzingatie kuwa uhusiano wa Muislamu na viumbe wengine wakiwamo wanaadamu wenzake, nasisitiza, binaadamu wenzake, una nafasi muhimu katika kujenga au kubomoa mafanikio ya uhusiano wake na Mola Muumba wake. Yaani, malipo mema yatokanayo na ibada za Swala, Zakkah, Swaumu na nyinginezo hayatamsaidia mwanadamu kumpeleka peponi endapo alikuwa ni mtu mwenye tabia mbaya zilizoharibu uhusiano wake na wanaadamu wenzake kama anavyotufundisha Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) katika hadithi ifuatayo:

Imaam Muslim amepokea kwamba Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alisema (kuwaambia maswahaba wake): “Je mnamjua aliyefilisika (muflisi)?” Walijibu: “Muflisi miongoni mwetu ni yule ambaye hana pesa wala mali.” Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akasema:“Muflisi ndani ya ummah wangu ni yule anayekuja siku ya Qiyaamah akiwa na Swalah (thawabu za Swala), Zakah (thawabu za Zakah) na Swaumu (thawabu za Swaumu), hata hivyo anakuja hali ya kuwa amemtukana huyu, amemsingizia huyu, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya huyu, na amempiga huyu. Hivyo, atalipwa (mdai huyu) kutokana na mema yake (mdaiwa) na atalipwa (mdai huyu) kutokana na mema yake (mdaiwa) na pale mema yake (mdaiwa) yatakapomalizika kabla ya kumalizika madai ya wanaomdai, anaadhibiwa kwa matendo yao maovu hadi pale anapotupwa motoni.”

Hivyo, utaona hapa huyu ambaye Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amemtangaza kuwa ni mwenye kufilisika si kwamba hakuwa akifanya ibada zilizo katika uhusiano wake yeye na Mola wake Muumba, alifanya ibada hizo za Swala, Swaumu, Zakkah na nyinginezo kwa ukamilifu kiasi cha kumpatia thawabu alizokwenda nazo kwa Mola wake, lakini msingi wa kufilisika kwake na kuikosa Pepo na kuingizwa Motoni (Tunamuomba Mwenyeezi Mungu Atuepushe na Adhabu ya Moto) ni kule kutofanya vizuri katika upande wa uhusiano wake na wanaadamu wenzake. Kwamba anaswali Swala Tano, anafunga Swaumu ya Ramadhani, anatoa Zakkah, lakini hana tabia njema: anatukana watu, anavunja heshima za watu, anawadhulumu watu, anawasingizia watu, anaua watu, anapiga watu kwa dhuluma. Ibada zake alizozifanya vyema hazimsaidii kwa kukosa tabia njema.

Hivyo basi, tuzingatie kuwa Uislamu si mavazi maalumu wala majina maalumu, bali Uislamu ni kukiri kwa moyo na kubaini kwa ulimi kwamba hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Mtume wake; kisha kutekeleza uliyoamrishwa na ukaacha uliyokatazwa na ukajipamba na tabia njema. Kufanya ibada bila ya kujipamba na tabia njema ni kujiorodhesha katika orodha ya watakaotangazwa kufilisiwa Siku ya Qiyama.

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Mwandishi wa makala hii, Sheikh Khamis Mataka, ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu Baraza Kuula Waislamu Tanzania (BAKWATA). Anapatikana kwa namba: 0713 603050, na 0784 603050.

221 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!