Nilipowapokea vijana kadhaa wa Kitanzania hapa London, miaka karibu mitano iliyopita, mmoja wao alikuwa amesomea diplomasia.

Sikuwa na hakika kama diplomasia yake ilikuwa ya kiwango gani, lakini uhakika ni kwamba alisomea hapa uchumi kwa ngazi ya shahada ya uzamili (masters).

Kwa sasa kijana huyo ameshavuka umri wa miaka 40 na anachapa kazi kama farasi hapo Tanzania, akiwa ni meneja.


Haya yamenijia wakati nikiangalia gharama inazoingia Serikali ya Uingereza kwa ajili ya kusubiri kumkamata Julian Assange, aliyejificha kwenye Ubalozi wa Ecuador, jijini hapa.

 

Niliwasikia jamaa wa ‘ofisi kubwa’ wakisema wamepigwa ‘changa la macho’ na sasa wamepatwa na kigugumizi, wakikaa usiku na mchana, jua likiwaka na mvua ikinyesha nje ya ubalozi huo.


Assange ni jamaa aliyechapisha siri za wakubwa kupitia mtandao wa Wikileaks, akijiita mwanaharakati wa kuweka wazi ukweli.

 

Ecuador, kati ya nchi zote duniani, ilisimama kidete kumtetea Assange anayetakiwa nchini Sweden na baadaye nadhani Marekani, kujibu mashitaka mbalimbali baada ya kuwachukiza wakubwa. Uingereza haitaki kupoteza urafiki na washirika wao wakubwa na wanaona kinyaa kwamba Assange yupo hapa.


Nikiwa wazi hapa, mimi si mmoja wa wanaounga mkono mambo ya Assange, maana wakati mwingine ukianika kila kitu ilimradi ni ukweli, ndiyo mwisho wako.

 

Tukirudi kwa makachero wanaokesha hapo saa 24 kwa siku saba za kila wiki, ni kwamba walitishia kuingia ndani ya ubalozi, halafu wakashituka kumbe wao ni ‘viranja’ wa sheria.


Nilipita pale Hans Crescent, Jumamosi, nikiwa na hamsini zangu bwana, wala sikuwa najua ubalozi wa Ecuador ndiyo upo pale, hadi ‘tasha’ nililokuwa nalo likanitoa wasiwasi kuona hali ilivyokuwa, akaniambia wanamsubiri Assange atoke ndani.


Nilipomuuliza kama alikuwa anatoka kwa sababu gani na aliingia kufanya nini, alicheka akaniona sijui mambo. Lakini alimalizia kwa kuwachapa kijembe Wangereza wenzake, akasema si kwamba anatoka kweli, bali wanasubiri kama fisi anavyomfuata mwanadamu kusubiri mkono uanguke, eti kwa vile anaona unaning’inia!

 

Hawawezi kuingia ndani ya jengo la Ubalozi wa Ecuador kwa sababu ya kinga ya kibalozi, yaani ukishasogelea kuta za lile jengo na kuanza kuingia ndani, ni kwamba upo nchini Ecuador.

 

Kwa hiyo hawawezi askari wale wa Scotland Yard kuingia mle kwa nguvu, labda wakaribishwe na Waecuador wenyewe wanaomlinda ndani ya kuta za jengo lao kwa kujigamba.

 

Sasa nimesikia kwamba suala hilo la kidiplomasia na yatokanayo katika kusubiri kwa makachero nje ya ubalozi, sasa gharama imeenda juu kufikia paundi milioni 3, takriban Sh bilioni 7.5.


Jamaa wanaona wakiondoka naye tu, Assange anaweza kutoka wakaadhirika, wakibaki gharama inaendelea kuwa kubwa mno na si ajabu ikawagharimu walio madarakani kwenye uchaguzi ujao.


Wapo njiapanda, na Assange yuko kule ndani ya ubalozi anaendelea kuandaa fataki za kuchafua wakubwa.


Ajabu ni kwamba kosa walilomwandikia mahakamani si la kuchapisha habari za uongo wala za uchochezi, isipokuwa ni makosa ya kujamiiana. Lakini yeye na wenzake wanahisi akishakamatwa ataandikiwa hayo ya kutoa siri kuu.


Sijui tutasubiri hadi lini kuona makachero wale ambao wangefanya kazi nyingine, lakini UK wanasema wanao wajibu wa kumkamata na kumkabidhi Assange, wakati Ecuador wanasema pamoja na udogo na umaskini wao wana kila sababu za kumlinda raia huyo wa Australia.

Sisi tutathubutu kufanya kitu kama hicho kama Watanzania?


Tuwasiliane kupitia: leejoseph2@yahoo.com.

Alamsiki wana-JAMHURI wote.

1179 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!