Aprili 26, ni siku ya maadhimisho ya miaka 49 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Sherehe za maadhimisho haya zitafanyika katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Saalam.

Sherehe hizo zinafanyika kukiwa na maswali kutoka kwa wananchi wa pande zote mbili, yanayohusu kero zinazoukabili Muungano huo.

Hadi sasa Serikali inajinasibu kutatua kero tisa kati ya 13 ambazo ni utekelezaji wa haki za binadamu kwa Zanzibar, Uwezo wa Zanzibar kujiunga na Merchant Shipping Act ya Jamhuri ya Muungano, kujiunga na International Maritime Organization (IMO) na Zanzibar kushiriki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).


Kero nyingine ni Zanzibar kulipa kodi nje ya nchi, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kulipa kodi mara mbili, kuvua katika ukanda wa uchumi bahari kuu, ongezeko la bei ya umeme kutoka Tanesco kwenda Zesco na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.


Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Bunge la 11, imeibuka na kutonesha vidonda vya kero hizo, baada kuibuka na kero ya ubaguzi na Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo.


Hoja hiyo iliibuliwa na Msemaji Kambi hiyo, Ofisi ya Makamu wa Rais, David Silinde (Chadema-Mbozi Magharibi), aliyesema:


“Katika kurekebisha hali ya utata iliyojitokeza kwenye majimbo ya Zanzibar, SMZ imeamua kuanzisha Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo, kwa wajumbe wa Baraza hilo na kufanya hoja hii kuhitaji kupatiwa ufumbuzi.


“Hii ni kwa sababu sasa kila jimbo la uchaguzi la Zanzibar litapata mafungu mawili ya fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo, wakati majimbo ya Tanzania Bara yakipata fungu moja.”


Silinde alisema majimbo hayo madogo na yenye idadi ndogo ya watu, sasa yatapata fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kutoka Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huku majimbo makubwa ya Bara na yenye watu wengi yakipata fedha kutoka chanzo kimoja.


Kambi hiyo iliitaka Serikali ilieleze Bunge kama ni halali kwa fedha za umma kuendelea kutoa ruzuku mifuko ya Maendeleo ya Majimbo ya Zanzibar, wakati sasa itakuwa inapata fedha kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano) Samia Hassan Suluhu, amejibu hoja hii. Anasema fedha za Mfuko wa Jimbo zinatolewa kwa uwiano wa watu, hivyo kwa Zanzibar jimbo lenye kupata fedha nyingi kupitia mfuko huu linapata Sh milioni 25, wakati kwa Tanzania Bara majimbo yanapata hadi Sh milioni 100.


Kuhusu wawakilishi kuundiwa Mfuko wa Jimbo, Samia alisema mfuko huu umeundwa kwa nia ya kuwaongezea hadhi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ambao watakuwa wakipewa Sh milioni 10 kila jimbo.


Hoja nyingine ni Watanganyika wanabaguliwa kwa kunyimwa haki ya kumiliki ardhi visiwani na Wazanzibari kujazana kwenye Bunge la Muungano, wakati Watanganyika hawaruhusiwi kuingia kwenye Baraza la Wawakilishi.


“Hivyo basi, wakati Bunge la sasa mbunge mmoja anawakilisha watu 157,000, mbunge mmoja wa Zanzibar anawakilisha wastani wa watu 16,000,” anasema Silinde. Anasema Bunge la sasa, kuna Wazanzibari 83 kati ya wabunge wote 357.


Amenukuhu kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Kwanza wa Zanzibar, Wolfango Dourado, aliyesema akimnukuu Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, akisema,  “Msiwe na wasiwasi, sisi tuna haki ya kuwakilishwa katika Bunge lao, lakini wao hawana haki ya kuwa kwenye Baraza letu la Mapinduzi.”


Hoja hii Serikali imeijibu kwa maelezo kuwa Zanzibar ina ardhi kidogo, hivyo kuruhusu watu wengine kumiliki ardhi kutazidi kupunguza uwezekano wa Wazanzibari kumiliki ardhi. Suala la wingi wa wabunge kutoka Zanzibar kwenye Bunge, Serikali imesema suala si idadi ya watu, bali hizi ni nchi mbili ziliungana.


Mawazo ya Silinde, yanashabihiana na ya wananchi wengi waliobaki na maswali kuhusu muundo na mfumo wa Muungano. Wapo wanaotaka muundo wa serikali tatu na pia wapo wanaodai mfumo wa serikali mbili katika Muungano.


Wapo waliokwenda mbili zaidi, kwa kusema muundo wa Muungano wetu ni wa kipekee duniani ndiyo sababu kuna kero nyingi za Muungano.


Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria nyingine zimeshindwa kuzingatia na kutambua maana, dhamira na matakwa halisi ya Muungano huu kupitia hati asili za Muungano, kwa kuthubutu kubadilisha hata mambo ya msingi ambayo yaliwekwa na waasisi wa Muungano ndani hati ya Muungano.


Wengine wanasema msingi huu wa hati asili na matakwa yake, zilikiukwa za kukidhi matakwa ya watu fulani.


Mfano halisi ni  pale ulipopitishwa muswada wa kubadilisha nafasi ya Makamu wa Rais kutoka kwa Rais wa Zanzibar na kuweka mfumo uliopo sasa, kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge, ibara ya 98(1)(b) haikuzingatiwa, hali iliyoleta mabadiliko yaliyoondoa dhana mzima ya kuwa na Muungano unaotokana na pande mbili.


Mabadiliko haya, mbali na kuwa yalishindwa kuzingatia matakwa ya Katiba ambayo tunaiita sheria mama ya nchi, pia yalifuta kipengele muhimu katika Makubaliano Halisi ya Muungano. Hili lilionekana kuwa suala dogo wakati huo, lakini kwa sasa madhara yake ni makubwa.


Hali ilivyo sasa ni tofauti na ukweli huu. Kuna mambo mengi yaliyofanywa chini ya Katiba hizi mbili nje ya Mkataba wa Muungano. Mfano, nyongeza ya kwanza ya mambo 11 yanayosemwa nayo ni ya Muungano kwa sasa. Jaji Mkuu wa kwanza mzalendo, Francis Nyalali, alinukuliwa akisema:


“Kwa kuwa makubaliano ya Muungano ndiyo chimbuko la Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ipo haja ya kuisoma na makubaliano hayo ili kuielewa vizuri.”


Kwa mantiki hiyo, Katiba haiwezi kubadili vipengele vya Muungano (Articles of Union). Kwa kuwa vilitungwa na serikali mbili, na kwa kuwa moja ya serikali hizo haipo tena, wenye mamlaka ya kuamua kimsingi ni wananchi wa nchi mbili hizi, ambao ndiyo chimbuko la mamlaka yote ya dola.


Hii ina maana kwamba kama lipo jambo katika Katiba ya sasa ya 1977 au katika marekebisho yake, ambalo linakiuka Vipengele vya Muungano, jambo hilo haliwezi kuwa na nguvu za kikatiba isipokuwa kama lina ridhaa ya wenye mamlaka ya mwisho; yaani wananchi kupitia kura ya maoni.

Historia

Jina ‘Tanzania’ limeundwa kutokana na majina ya Tanganyika na likitoka Zanzibar. Hapa wabunifu walimega Tan- kutoka Tanganyika na Zan- kutoka Zanzibar, kisha kumalizia irabu mbili i na a kuliwezesha kusomeka. Nchi hizi mbili zilikuwa zote chini ya utawala wa Uingereza hadi zilipopata Uhuru, lakini hazikuwa makoloni ya kawaida.


Tanganyika iliwahi kuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, halafu ikawa chini ya uangalizi wa Uingereza kama eneo la kudhaminiwa kutokana na Azimio la Shirikisho la Umoja wa Mataifa lililoipa Uingereza mamlaka ya kuwa mdhamini wa Tanganyika.


Tanganyika na Zanzibar zilikuwa nchi mbili tofauti hadi 1964 zilipoungana na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwalimu Julius Nyerere alikuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na  kiongozi wa mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume akawa Makamu wa Kwanza wa Rais.


Mambo yafuatayo yalikubalika kuwa shughuli za Muungano. Jeshi la Ulinzi, Polisi, Mamlaka ya Dharura, Uraia, Uhamiaji, Biashara ya Nje, Utumishi wa Umma, Kodi ya Mapato na Ushuru wa Forodha, Bandari, Usafiri wa Anga, na Posta na Simu.

 

Hata hivyo, leo orodha imeongezeka hadi 22 na wachambuzi wanasema ukiimega vyema mambo ya muungano yanafikia 37 kwa sasa. Je, tunaelekea wapi? Tutafute ufumbuzi. Mungu ibariki Tanzania.


0713 393 393


Please follow and like us:
Pin Share