Wiki iliyopita Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, amefanya mabadiliko katika Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Amemuondoa Mkurugenzi Mkuu, Modest Kipilimba na kumteua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Diwani Athumani, kuchukua nafasi yake.

Kwa kweli si kawaida Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kuondolewa katikati ya kipindi cha uongozi wa rais aliyepo madarakani, kabla rais hajamaliza kipindi chake. Ni kwa mshituko huo, hata sisi tunalazimika kuandika maoni kumshauri Mkurugenzi mpya wa Usalama wa Taifa aliyeingia, kwani hata kama sisi si mamlaka ya uteuzi, lakini kama wafuatiliaji wa karibu wa mienendo ya nchi, tunayo ya kusema.

Idara za Usalama wa Taifa katika nchi nyingi duniani ndiyo jicho la uchumi wa taifa. Uchumi imara ndiyo nguvu ya taifa, si tu kwa wananchi, bali pia kimataifa katika nyanja ya diplomasia. Nchi ikiwa na uchumi legelege, haiwezi kuwa na jeshi imara, polisi imara, usalama imara au wananchi imara. Ndiyo maana leo tunashuhudia nchi kama Marekani inapambana na China. Vinginevyo vyombo hivi vitabaki kuwa kijiwe cha fitina.

Mapambano ya Marekani na China si ya kisiasa, ni ya kiuchumi. Ukienda katika nchi kama Italia, Uingereza, Japan, China na kwingine kwingi, Idara za Usalama wa Taifa ndizo zinachora ramani ya uchumi. Tanzania ilipopata Uhuru mwaka 1961 kwa makusudi iliwekeza katika jukumu la ukombozi wa Afrika. Idara ya Usalama ilifuatilia kila nyendo kuhakikisha mkakati huu unafanikiwa.

Mwaka 1994 Afrika Kusini ilipata Uhuru na kuibakiza Sahara Magharibi inayokaliwa na Morocco, hivyo nguvu ya Idara ya Usalama ndani na kimataifa ikabadilishwa tangu mwaka 2004 kuwa Diplomasia ya Uchumi. Taifa letu limeanza kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali, hasa utalii na madini, ingawa yalikuwapo makosa ya hapa na pale kwa kukosa uzoefu.

Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, ikaanza kwa kishindo cha kurekebisha palipokuwa pameharibika. Serikali ya Rais Magufuli imepambana na rushwa, ikakamata wahujumu uchumi, ikarekebisha Shirika la Ndege la Taifa (ATCL), ikaanza ujenzi wa reli ya Standard Gauge, ikawekeza katika umeme ikiwamo Stiegler’s Gorge, ikarekebisha mfumo wa elimu lakini kubwa ikasimamia SERA YA VIWANDA.

Sera ya Viwanda ililenga kuliondoa taifa letu katika umaskini kwa kishindo. Tunasema, na hapa tunaomba tusamehewe kwa kuyasema haya, huku tukiomba Mkurugenzi mpya Diwani asiingie katika mtego huu, watu wanaamini idara chini ya Kipilimba ilipeleka nchi alijojo.

Ni kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi, watu wameanza kupotea, utekaji umeshamiri katika nchi yetu, idara imeingia kwenye siasa, wanaotaka kupanda vyeo au kupata fedha wanawagawa Watanzania kwa kuwaandikia ripoti au kuwataja kuwa ni wapinzani, kumezalishwa makundi ya wahujumu na mawakala wa mabeberu na watu wanarekodiana hata kazini hakuna uhuru wa kutoa mawazo.

Idara watu wanaiona imegeuza mikutano ya rais wa wananchi kuwa kero. Kukiwa na mkutano anafungiwa vyuma badala ya utepe kama zinavyofanya nchi nyingi duniani, wafungwa wanasindikizwa kwa bunduki za kivita kama vile nchi imo katika hali ya hatari, wakati siyo. Baadhi ya wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa wanatoa matamshi ya hatari wakijinasibu kwa ukaribu wao na Idara ya Usalaam na mengine mengi.

Kwa kweli tunaomba kuwasilisha ombi letu kwa Mkurugenzi Mkuu Diwani, kuwa Watanzania hawataki kutekwa. Idara inapaswa kuwa msitari wa mbele kufahamu watekaji ni kina nani. Idara inapaswa kupigana vita ya kiuchumi badala ya kuendesha fitina za kisiasa na vita ya ushindi majimboni na kwenye kata.

Nchi haitaendelea kwa siasa za majukwaani. Kama tulivyobadili Sera ya Mambo ya Nje ikawa Diplomasia ya Uchumi, ikiwa idara haijajibadilisha, baba tunakuomba uibadili irejeshe amani kwa Watanzania waondokane na woga uliojengwa, usio na afya kwa ustawi wa taifa letu. Idara ya Usalama ijenge uchumi na viwanda. Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri