KAHAMA

Na Antony Sollo

Waziri wa Madini, Dk. Dotto Biteko, ameagiza kusimamishwa kazi maofisa saba wa madini wa mikoa mbalimbali kutokana na utovu wa nidhamu.

Akizungumza na wafanyabiashara wa madini wa Kanda ya Ziwa mjini hapa, Dk. Biteko amesema wapo baadhi ya maofisa Madini Wakazi wa mikoa wanaojihusisha na udanganyifu, ikiwamo kuwapunguzia wachimbaji viwango vya ubora wa madini ili wajipatie fedha.

“Ninawatahadharisha maofisa madini wa mikoa yote nchini kuwa makini na kuwabaini watu wa aina hii; wanaoshirikiana na baadhi ya wafanyabiashara kupaka mafuta kwenye mashine ya kupimia ubora wa dhahabu hivyo kusababisha kupata viwango vya chini ya uhalisia,” amesema Dk. Biteko.

Waziri amemwagiza Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, kuwashughulikia maofisa saba wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Pia amesema wapo wafanyabiashara ya dhahabu wanaowafanyia utapeli wenzao kutoka nje ya nchi kwa kuchukua fedha zao wakiahidi kuwanunulia madini lakini hawafanyi hivyo, wakisingizia kuugua Uviko – 19.

“Hivi karibuni Mzungu mmoja alifika ofisini kwangu analia kutapeliwa dola za Marekani 800,000 sawa na Sh bilioni 7.2. Tukampigia mhusika akatujibu kuwa anaumwa corona wakati si kweli,” anasema.

Anasema utapeli huu umekuja baada ya serikali kudhibiti mianya ya utoroshaji madini nchini uliokuwa ukiikosesha mapato makubwa.

Kuhusu ukusanyaji maduhuli ya serikali, Dk. Biteko anasema soko la madini la Geita limeongoza kwa mwaka 2020/21 kwa kukusanya Sh bilioni 211.5, likifuatiwa na Mara lililokusanya Sh bilioni 109.3 huku soko la Kahama likikusanya Sh bilioni 93.7 na kushika nafasi ya tatu.

Awali, Dk. Biteko alikutana na maofisa Madini Wakazi wa mikoa ya kimadini ya Kahama, Mbogwe,  Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu, Mwanza, Singida, Kigoma, Kagera na Tabora.

By Jamhuri