*Asema Takukuru haizuii watu kujenga mahekalu

*Wadau wataka wanaothibitika kula rushwa wauawe

 

Ujasiri na ushirikiano wa dhati vimetajwa kuwa ni miongoni mwa nyenzo thabiti, zinazoweza kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini.

 

Changamoto hiyo imeelezwa katika kongamano la mwaka 2012 la wadau wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), lililofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam, Septemba 24, mwaka huu.

 

 

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk. Edward Hoseah, anasisitiza umuhimu wa wananchi kuongeza ujasiri wa kufichua vitendo vya rushwa katika jamii ili wahusika wachukuliwe hatua haraka.


Anasema ofisi yake inafanya kila liwezekanalo kuongeza wigo wa ushirikiano wa dhati na sekta mbalimbali, katika juhudi za kukabili ipasavyo tatizo la rushwa linalotazamwa kama adui wa haki katika jamii.


Hata hivyo, anaamini kuwa vitendo vya rushwa havijaongezeka katika siku za karibuni na kwamba wananchi wengi wana uelewa mkubwa juu ya tatizo hilo.


“Uelewa wa Watanzania kuhusu rushwa umeongezeka maradufu, sasa hivi hatungojei kutafuta habari, wananchi wana nafasi kubwa ya kutoa taarifa za rushwa,” anasema Dk. Hoseah.

 

Anadokeza kuwa katika kipindi cha mwaka huu, pamoja na mambo mengine, Takukuru imefanikiwa kuokoa Sh bilioni saba za Serikali zilizokuwa zimeelekezwa na ‘wajanja’ wachache katika malipo ya walimu hewa.

 

“Pia mpaka sasa tumeshatekeleza utaratibu tuliojiwekea kama taasisi (Takukuru), wa kukamilisha kesi tano kubwa za rushwa (hakuzitaja) katika mahakama,” anaongeza Dk. Hoseah.

Walioficha fedha Uswisi

Akizungumzia suala la viongozi wanaodaiwa kuficha mabilioni ya fedha katika benki za Uswisi, Dk. Hoseah anasema tayari amekwisha kuiomba kwa maandishi serikali ya nchi hiyo imtumie majina ya watuhumiwa hao.

 

“Tayari nimeshaiandikia serikali ya Uswisi barua kuiomba initumie ripoti ya maelezo yakiwamo majina ya Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha huko ili ufuatiliaji wa kisheria uanze kuchukua mkondo,” anasema.

 

Wakati Dk. Hoseah akielezea msimamo huo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), ameshaahidi kuwataja walioficha mabilioni ya fedha Uswisi katika kikao kijacho cha Bunge mwishoni Oktoba, mwaka huu, ikiwa Serikali haitawataja kabla ya muda huo.

 

Inadaiwa kuwa dola za Kimarekani milioni 186 (sawa na Sh bilioni 300 za Kitanzania) zimefichwa katika benki tatu tofauti nchini Uswisi, ambapo fedha hizo zinahusishwa na ufisadi uliofanywa na viongozi kadhaa nchini.


Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amewahi kuwataka watu wanaowafahamu walioficha fedha hizo Uswisi wajitokeze kuwataja hadharani iwe rahisi kwa Serikali kuwachukulia hatua za kisheria.

Maofisa Takukuru wala rushwa

Kuhusu tuhuma kwamba baadhi ya maofisa wa Takukuru huomba na kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa, Dk. Hoseah anasema ofisi yake inawasaka kwa udi na uvumba ili washughulikiwe haraka.

 

“Kwa yeyote anayewafahamu maofisa wa Takukuru wanaokula rushwa asisite kuniletea majina yao, hilo ni kosa ambalo halivumiliki katika taasisi yangu,” anasema Dk. Hoseah na kuendelea:

 

“Nikipata majina ya maofisa hao nitachukua hatua mara moja, mtumishi akilalamikiwa inatakiwa tuchukue hatua mara moja. Tumeshachukua hatua kwa watu chungu nzima, wengine tumewafukuza kazi.”


Uchu wa kutaka utajiri kwa njia ya mkato ndiyo chanzo cha baadhi ya viongozi wa umma wakiwamo maofisa wa Takukuru wasio waadilifu kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa, hususan wanaokwepa kulipa kodi za Serikali.

Rushwa katika chaguzi

Dk. Hoseah anakiri kwamba vitendo vya rushwa katika chaguzi, hususani za kisiasa bado ni tatizo kubwa nchini linalohitaji juhudi za pamoja kulikabili.

 

“Wagombea wengi wanatumia fedha (kushawishi wapigakura wawachague) na wapigakura wengi wanaomba fedha (kutoka kwa wagombea ili wawapendelee kwa kuwachagua),” anasema.


Wadadisi wa masuala ya uchaguzi wanasema dhana ya kutumia fedha kutafuta uongozi imejengeka karibu kwa kila mgombea uongozi wa kisiasa katika ngazi za kitongoji, mtaa, kata, jimbo na Taifa.


Pamoja na kujua ukubwa wa tatizo la rushwa katika chaguzi, Takukuru haijafanikiwa kulidhibiti kwa kiwango kinachostahili. Madhara ya rushwa katika chaguzi ni pamoja na kuchaguliwa kwa watu wasiyo na sifa za uongozi.

Matajiri wanaojenga mahekalu

Katika kujibu swali la mmoja wa wadau wa kongamano hilo, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Takukuru dhidi ya watu wanaojenga mahekalu (nyumba za kifahari zaidi) nchini, Dk. Hoseah anasema ofisi yake haiwezi kuzuia jambo hilo.


“Ni kweli kuna baadhi ya watu waliojenga na wanaoendelea kujenga mahekalu nchini, lakini hatuwezi kumzuia mtu kufanya hivyo kwa sababu kitendo hicho si dhambi.

 

“Sisi (Takukuru) tunachoweza kufanya ni kuchunguza ili kujua kama rushwa ndiyo iliyowawezesha watu kujenga mahekalu, vinginevyo hatuwezi kuzuia watu kujenga nyumba nzuri kwa namna wanavyopenda,” anasisitiza.

Ludovick Utouh

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, anasema Serikali inaendelea kujitahidi kwa kila uwezo kuwezesha ofisi yake kutekeleza majukumu yake kwa ushirikiano na Takukuru.


Kwa kutambua umuhimu wa CAG, Serikali imekuwa ikiongeza wafanyakazi wa ofisi yake, hususan wakaguzi wa hesabu kila mwaka, kama njia mojawapo ya kuboresha utendaji kazi kwa manufaa ya umma.


“Kwa mfano, mwaka jana tuliajiri wakaguzi (wa hesabu za Serikali) karibu 100, na mwaka huu tuna mpango wa kuajiri wakaguzi 120, tunaongeza wafanyakazi kulingana na ongezeko la kazi za ofisi ya CAG,” anafafanua Utouh.


Wadau wanena

Kwa upande wao, baadhi ya wadau wa Takukuru katika kongamano hilo, wanapendekeza adhabu ya kifo kwa watu wanaotiwa hatiani kwa makosa ya kuomba, kupokea na kutoa rushwa nchini.


“Ninadhani Serikali iangalie uwezekano wa kuidhinisha adhabu ya kifo kwa kila mtu anayekutwa na makosa ya rushwa, ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kujihusisha na vitendo vya rushwa nchini,” anasema mdau mmoja. Wadau wengine wanasema elimu zaidi juu ya rushwa inahitajika kwa wananchi, hususan wanaoishi maeneo ya pembezoni (vijijini) mwa nchi, waweze kujua madhara na namna ya kupambana na tatizo hilo.


Wengine wanaishutumu Takukuru wakidai mara nyingi hushindwa kutoa ushahidi makini dhidi ya washitakiwa wa makosa ya rushwa, na hivyo kusababisha mahakama kuwaachia huru baada ya kukosa ushahidi wa kuwatia hatiani.


“Kuachiwa huru kwa watu wanaoshitakiwa kwa makosa ya kuomba, kupokea na kutoa rushwa ni kielelezo kuwa maofisa wa Takukuru hawako makini katika kutoa ushahidi wao,” anasema mdau mwingine.


Katika hatua nyingine, Dk. Hoseah anaahidi kuwa ofisi yake itaendelea kuboresha ushirikiano na vyombo vya habari kuviwezesha kupata taarifa vinazozihitaji kwa wakati na bila mizengwe. Pia anaahidi kuufanyia kazi ushauri wa wadau wanaotaka Takukuru kutojiweka kando na mchakato wa Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Kwamba taasisi hiyo inapaswa kuwa na mkakati madhubuti wa kufuatilia kwa karibu mwenendo wa shughuli za kuhamasisha, na kutoa maoni ya Katiba mpya kuhakikisha haziathiriwi na vitendo vya rushwa.


Akijibu malalamiko ya wadau kuhusu kutokuwa hewani kwa namba 113 iliyotangazwa na Takukuru kwa ajili ya kupokea taarifa za rushwa kutoka kwa wananchi, Dk. Hoseah anasema:

 

“Wakati fulani namba 113 tuliyoiweka kwa ajili ya kupokelea taarifa za rushwa inashindwa kufanya kazi kutokana na matatizo ya mitambo ya TTCL (Kampuni ya Mawasiliano Tanzania) inayosimamia mawasiliano hayo,” anasema Dk. Hoseah.


Hatimaye Mkurugenzi Mkuu huyo wa Takukuru anatumia nafasi hiyo pia kutoa wito maalumu kwa wananchi kutokata tamaa ya kufichua vitendo vya rushwa katika jamii kuwezesha hatua stahiki kuchukuliwa haraka dhidi ya wahusika.


“Wananchi wasikate tamaa ya kuendelea kuibua matatizo ya rushwa kwa sababu Takukuru haiwezi kufanikiwa bila kupata ushirikiano wa wananchi,” anasisitiza.

 

1235 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!