Wakoloni, hasa Waingereza, walikuwa na ubaguzi wa hali ya juu. Miongoni mwa raia wao walikuwapo walioitwa raia halisi (British nationals), na raia watawaliwa (British subjects).

Kabla ya Uhuru wetu, sisi Watanganyika tulipewa pasipoti za Kiingereza zenye maneno British Subject. Lakini siku tulipopata Uhuru wetu Desemba 9, 1961 Mwalimu Nyerere alitangaza hivi, “Every Tanganyikan can now say I am a citizen of a Sovereign Independent State”  (Nyerere: The State and the Government 10 Dec. 1962).  Yaani, “Kila Mtanganyika sasa anaweza kusema ‘mimi ni raia wan chi huru’”.


Kwa kuwa wananchi wote kuanzia siku ile tulikuwa raia huru wa Taifa letu, basi tulitakiwa sote kwa umoja wetu na utaifa wetu tujenge taifa safi lisilo na ubaguzi wa aina yoyote.


Ninakumbuka enzi za miaka ya 1960 kule Marekani alichaguliwa Rais kijana, John Fitzgerald Kennedy, kuongoza Taifa lile kubwa. Siku chache kabla ya kuapishwa kwake Januari 20, 1961 aliulizwa swali na wanahabari: Mr. President, you are a Roman Catholic, won’t you be taking orders from the Pope in Rome and implement them here in the USA?”. Rais mteule yule kwa tabasamu sana aliwathibitishia Wamarekani wote kuwa dini yake haihusiani na uraia wake.


Alisema hivi na nukuu, “I am primarily an American and secondly a Roman Catholic!” Hapa alionyesha wazi wazi kuwa yeye kimsingi kwanza kabisa ni raia wa Marekani, hii dini yake ya ukatoliki imefuata baada ya ule uraia wake. Kwa hiyo, basi hapa nchini masuala ya dini yalianzaje hata siku hizi yanaelekea kuonekana katika elimu, sensa na kazi? Upungufu au dosari za udini zimeanza kuonekana tangu enzi za ukoloni kama nitakavyoeleza hapa katika makala yangu haya.


Kwa muda mrefu nimekuwa ninajiuliza dosari zinazojitokeza katika elimu hapa Tanzania zimesababishwa na nini au chanzo chake hasa ni kipi? Kuna upungufu mwingi katika elimu tangu utaratibu wa elimu ya kawaida (yaani formal education) uingizwe katika nchi hii, pale ilipokuwa koloni la Tanganyika hadi sasa Taifa huru la Tanzania lililosherehekea miaka 50 ya Uhuru wake baada ya kujikomboa kutoka mikononi mwa ukoloni wa Waingereza.

 

Katika tafuta tafuta yangu ilinibidi nijikite katika kusoma vitabu vilivyoandikwa na Wazungu na vile vilivyoandikwa na Waarabu na pia vilivyoandikwa na sisi Watanzania wenyewe.

 

Maandiko na majarida mbalimbali yamenipa mwanga angalau kihistoria nini kilikosewa na kwa nini hakikuwekwa sawa na mamlaka husika katika nchi yetu. Wapo walioandika kwa mtazamo ninaouita wa kimagharibi. Wapo walioandika kwa mtazamo wa kimashariki ya kati ambao ndiyo wageni wa kwanza kuingia pwani ya Tanganyika karne nyingi kabla ya Wazungu kutufikia.


Lakini upo mtazamo au dira ya Serikali ya Taifa huru la Tanzania katika jitihada za kujenga Taifa la Kitanzania lisilofungamana na upande wowote wa dunia, si Magharibi wala Mashariki. Hayo yote yametoa changamoto na ndipo nikaamua nami nitoe mawazo yangu katika hili suala la dosari zilizojitokeza katika elimu ya hapa Tanzania.


Tangu zamani Watanzania kila kabila lilikuwa na namna yake ya kuelimisha watoto wake katika mila na desturi za kabila lenyewe. Hapo watoto walipewa ujuzi na maarifa ya kikabila na pengine waliwekwa mahali fulani pamoja wakapewa miiko ya kabila, njia za uzalishaji mali katika kabila, namna ya kulinda kabila lao na namna ya kuanzisha familia zao ndani ya kabila.

 

Haya yote walielimishwa katika majando/unyago na walimu tunaowaita mangariba, waliopewa jukumu katika ukoo au kabila kutoa elimu kwa vizazi vipya katika kila jamii. Mapokeo namna hii ya elimu yamejulikana kama “informal education” yameendelezwa kutoka kizazi hadi kizazi.


Walipoingia wageni kutoka Bara Asia au Ulaya wakaingiza mfumo wao wa elimu ambao ndiyo huu wa darasani (formal education). Waarabu walikuwa Taifa la kwanza hapa nchini kutufundisha elimu ya kusoma na kuandika katika madrasa au shule au vyuo vyao. Wazungu waliita shule namna hiyo Koranic schools.


Historia inasema wazi kuwa wageni kutoka Bara Asia walifika pwani ya Tanganyika tangu karne ya 10 mnamo mwaka 945 AD (Political Development of Tanganyika by J. Clagett Taylor uk. 5), na imethibitishwa kuwa Waajemi walifika Kilwa na kukaa huko enzi hizo.

 

Wareno nao walifika katika visiwa vya Zanzibar na Pemba miaka ya 1499 (Zanzibar – its society and its politics by John Middleton and Jane Campbell uk. 3), na kuanzia muda huo yamekuwapo maingiliano kati ya watu wa mwambao, Zanzibar na Pemba na hao Waarabu kwa karne na hivyo kutokea vizazi vya  wakazi wa pwani na wakajulikana kwa ujumla wao kama Waswahili.

 

Wakaja wageni kutoka Bara Ulaya – Wazungu. Kihistoria huku Afrika Mashariki Wazungu wa kwanza baada ya ujio wa Waarabu walikuwa Wareno mwishoni mwa karne ya 15. Vitabu mbalimbali vinaonesha Vasco da Gama kutoka Ureno alifika Pemba mwaka 1499 (kadiri ya John Middleton na Jane Campel katika historia ya Zanzibar uk. 3), huku J. Clagett Taylor katika The Political Development of Tanganyika uk. 7 anatueleza Mreno Vasco da Gama alitua Kilwa mwaka 1498 akienda India.


Basi, Wareno ndiyo Wazungu wa kwanza kukanyaga ardhi ya Afrika Mashariki. Lakini Wamisionari wa kwanza kuja Afrika Mashariki wale wa Anglikana (UMCA) walifika Zanzibari mwaka 1863 na wakaanzisha shule ya kwanza ya Misheni eneo la Kiungani mwaka 1868. Wamisionari Wakatoliki shirika la Holy Ghost Fathers walifika pwani ya Bagamoyo mwaka 1868 na wakaanzisha shule ya kwanza ya Misheni hapo Bagamoyo mwaka 1873.

 

Wazungu Wamisionari hawa walileta mfumo wa elimu tofauti na ule uliozoeleka huku mwambao. Wamisionari walileta mtindo wa elimu ya darasani wa kimagharibi wakati Waarabu walikwishaleta mfumo wa elimu ya darasani wa kimashariki. Lakini elimu hii ya darasani ndiyo leo inayojulikana kama elimu ya kawaida (formal education).


Tofauti kabisa na ile elimu ya kila kabila waliyokuwa wakiwapa watoto wao, hii elimu ya darasani inalenga kumpa mtoto ujuzi na maarifa yatakayomwezesha kutambua mazingira yanayomzunguka mahali anapoishi, inalenga kumjenga kimaadili na kiroho ili aweze kumudu maisha katika jumuiya anamoishi. Elimu hii ya kawaida ni ya kumkomboa mtoto kifikra apate kuyatawala mazingira anamoishi.


Hadi hapo zimefunguliwa shule zenye mlengo wa kiimani za dini. Koranic schools/madrasa zililenga kuwaelimisha watoto Waislamu katika utamaduni wa Kiislamu na waijue imani ya dini yao. Wamisheni walijenga shule kuwaongoa watoto waijue imani ya Kikristu, wasome na waielewe Biblia na wajengeke kwa maisha ya Kikristu.

 

Serikali ya mkoloni kwa kuona kulikuwa na kinyang’anyiro cha watoto na mvutano kati ya shule za madrasa na shule za Misheni, maeneo ya mwambao iliamua kuanzisha shule za Serikali kwa watoto wote wa nchi hii bila kuegemea imani ya dini yoyote.


Shule za madrasa zilikuwa kwa watoto wenye imani ya Kiislamu wakati shule za Misheni zilikuwa kwa watoto wenye imani ya Kikristo. Je, watoto wasio na dini (wapagani) walio na dini za asilia wakasome wapi? Jibu ndiyo huo uanzilishi wa shule za Serikali zilizoitwa Secular State Schools. Shule hizi zilikuwa zinatoa elimu ya kawaida – secular education. Serikali ilikumbana na matatizo kadha wa kadha katika uanzishaji wa shule zake za Serikali maeneo ya mwambao.

 

By Jamhuri