Barua hii imeandikwa na watu waliojitambulisha kuwa ni wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao ni Wajumbe wa Mkutano Mkuu Wilaya ya Hanang’. Iliandikwa Oktoba 19, mwaka huu na kupelekwa kwa Katibu Mkuu wa CCM-Taifa. Kimsingi inapinga ushindi wa nafasi ya NEC wa Dk. Mary Nagu dhidi ya Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye.

YAH: KUPINGA MATOKEO YA UCHAGUZI NAFASI YA MJUMBE WA HALMASHAURI KUU TAIFA (NEC) WILAYA YA HANANG’

Mheshimiwa Katibu Mkuu, kichwa cha habari hapo juu chahusika. Sisi wenye majina na saini zetu hapo chini kwenye kiambatanisho cha barua hii ni viongozi na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM (W) ya Hanang’.

 

 

Kwa niaba ya wajumbe wenzetu, tukiungwa mkono na wanachama/ wananchi wanaokitakia mema Chama Cha Mapinduzi, tunawasilisha kwako pingamizi juu ya uchaguzi uliofanyika tarehe 29/10/2012 hapa wilayani Hanang’ kwa nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu –Taifa (NEC) kupitia Wilaya.

 

Tunapinga matokeo hayo kwa sababu zifuatazo:

A)  Kwa ujumla uchaguzi huo uligubikwa na mazingira yenye kuashiria rushwa tangua hatua ya mwanzo ya uchukuaji fomu, kurudisha fomu, na ndani ya siku za kampeni, na mwisho siku rasmi ya uchaguzi


B)  UCHUKUAJI FOMU

1) Mshindi wa nafasi hiyo siku ya uchukuaji fomu alitumia nafasi hiyo kuwakusanya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya wakiwamo wananchi na kufanya mkutano wa hadhara Stendi ya Mabasi mjini Katesh akitumia mkutano huo kukabidhi matrekta kwa baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya, waliopewa mikopo ya matrekta na kusema kuwa bila yeye kuwa Mjumbe wa NEC misaada kama hiyo haitaweza kupatikana ndani ya wilaya.


2) Kwa kupitia kauli zake hizo ambazo aliendelea kuzisema kwenye vikao vya kampeni zilionesha wazi kuwa nia yake ni kuwahofisha wajumbe kama hatapata nafasi hiyo, basi wilaya hii haitapata misaada tena.


3) Pia mazingira ya rushwa yaliongezeka pale alipoanza kutoa mabati huko kwenye matawi yafuatayo: (1) Qabata bati 100 (2)Qareda bati 100 (3) Gawidu bati 200 (4) Endasiwald akitoa Sh 1,000,000.


(4) KIPINDI CHOTE BAADA YA KURUDISHA FOMU

Mgombea alitumia ofisi ya umma (mbunge) na nyumbani kwake kama maeneo ya kufanyia vikao vya kampeni hasa nyakati za usiku, wajumbe kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya walisombwa na magari aliyotoa kuwafikisha sehemu hizo na magari ya Serikali yalitumika, hususan gari lake la kazi likiwa na bendera ya Taifa, yakiwamo na magari ya Halmashauri ya Wilaya. Pia kuwagawia fedha na kuwarudisha maeneo walikotoka.


5) Mgombea alitumia nafasi zake alizonazo kuwaita makatibu wa CCM wa Kata na kufanya nao vikao vya mara kwa mara:

1) akitumia ofisi ya CCM Wilaya,

2) maeneo ya Hotel Summit iliyoko Katesh,

3) ofisi za Matawi na Kata za chama.

Sehemu hizo zote zilitumika kama maeneo ya kuweka mikakati ya kumuwezesha kushinda zikiwemo ahadi za kupewa pikipiki endapo atashinda.


C: USIKU WA KUAMKIA UCHAGUZI TAREHE 28/9/2012

(1) Kwa kawaida tulifahamu kuwa wajumbe wangesafirishwa na CCM Wilaya, kwa mshangao, wilaya ilijitoa kusafirisha wajumbe na mgombea kuchukua nafasi ya kusafirisha baadhi ya wajumbe usiku huo na kuwapatia malazi na fedha na mahitaji mengine hadi asubuhi alipowafikisha eneo la uchaguzi.


D: SIKU YA UCHAGUZI 29/09/2012

Ratiba ya uchaguzi ilionesha kuwa kikao kingeanza mapema saa 4:00 asubuhi. Lakini bila kufahamu sababu, kikao kilianza mnamo saa 8:00 mchana. Kwa hiyo muda wote huo kuanzia asubuhi wajumbe waliachwa kuzagaa nje ya ukumbi na wale waliokuwa wapambe wa mgombea (mshindi) walitumia fursa kuwalaghai wapigakura kwa njia zote walizoweza ikiwa ni pamoja na kuwapeleka kwenye migahawa/baa, pamoja na kuwa vyombo vya dola vilikuwapo, lakini havikuthubutu kudhibiti hali hiyo.


(2)NDANI NA NJE YA UKUMBI WA UCHAGUZI

(i) Maandalizi ya ukumbi hayakuwa mazuri kwa vile ilikuwa hakuna utaratibu wa kudhibiti uhalali wa wajumbe na wasio wajumbe.


(ii) Hali ilikuwa mbaya zaidi nje ya ukumbi kwani mita tano kutoka lango kuu viliruhusiwa vibanda vya pombe, vyakula na huduma nyinginezo. Hali hii ilisababisha wajumbe kunywa pombe muda wote ndani na nje ya ukumbi na wengi wao kuishiwa kulewa.

 

(iii) Kundi la mgombea lilitumia mwanya huu kuwapenyeza mamluki ndani ya ukumbi na kupiga kura. Pia wapambe wa mgombea (mshindi) walipiga kura. Mfano ni Mathew Derema, msaidizi wa Mbunge.


(iv) Baadhi ya kata zilionyesha kuwa na idadi kubwa ya wajumbe kuliko zilizotolewa mwanzo na makatibu wa kata na iliyokuwepo wilayani kama vile Kata B/lalu, Laganga, Getanuwasi, Gehandu na GIsambalang.


NB: Wakati wa uchaguzi, kata hizo, baada ya  kupewa karatasi za kupigia kura kulingana na orodha na wajumbe, wasimamizi wa kata yaani makatibu waliwatanguliza mamluki, na wao kuwa wa mwisho, na hivyo kulazimu msimamizi kuongeza karatasi za kupigia kura nje ya orodha iliyokuwapo wilayani.


v) Pia kulijitokeza matawi ambayo hayakufahamika kabla ya siku ya uchaguzi. Mfano Tawi la  Mmbuyuni, Maslahh’aa n.k.


vi)  Kabla na wakati wote wa kampeni, mgombea huyo (mshindi) katika kampeni zake alikuwa akikejeli na kukashifu kazi zilizofanywa na mtangulizi wake na mgombea mwenzake, Mbunge mwanzilishi na Waziri Mkuu mstaafu kwamba “hajafanya lolote kwa kipindi chake chote ikiwa pamoja na kuwa Waziri Mkuu mwaka miaka kumi”.

 

Mheshimiwa Katibu Mkuu, baada ya maelezo (malalamiko) haya, tunaomba Chama Cha Mapinduzi kichambue malalamiko yetu na mwisho kifute matokeo hayo na uchaguzi urudiwe.

 


 

1535 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!