Moja ya uamuzi mgumu uliofanywa na uongozi wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, ni kumsimamisha mchezaji wake, Haruna Moshi ‘Boban’, kwa kosa la utovu wa nidhamu.

Uongozi huo pia umemwadhibu beki wake, Juma Nyoso, kwa kumshusha daraja kutoka timu ‘A’ hadi kikosi cha pili ajifunze tabia licha ya kupandisha kiwango chake.


‘Boban’ amekumbwa na adhabu hiyo baada ya kudaiwa kudanganya kuwa ni mgonjwa, hivyo kutoichezea Simba dhidi ya Coastal Union ya Tanga katika mashindano yanayoendelea ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.


Inadaiwa kuwa adhabu hiyo ni ombi la kocha wa Simba, Milovan Cirkovic, jambo ambalo hata hivyo, kwa tabia ya mchezaji huyo, inaweza kuwa kutwanga maji kwenye kinu.

 

Ni shabiki gani wa kandanda asiyemfahamu ‘Boban’ hapa nchini kwa kutandaza soka la kuvutia anapokuwa uwanjani? Yupi asiyejua umuhimu wake kwa timu yoyote anayokuwa nayo iwe klabu au timu ya taifa (Taifa Stars)?


‘Boban’ ana uwezo anaopaswa awe nao mchezaji, amezaliwa na kipaji hicho. Anaweza kuwekwa kundi moja na viungo mahiri wa zamani kama Sunday Manara ‘Kompyuta’, Charles Boniface Mkwasa, Octavian Mrope, Mwanamtwa Kihwelo, marehemu Ezekiel Greyson ‘Jujuman’, marehemu Saidi Mwamba ‘Kizota’, marehamu Khamis Thobias Gaga, miongoni mwa wengine.

 

Saidi Mwamba angeweza kuamka akiwa kwenye kilevi, akapanda ndege na kusafiri kwenda mji wa mbali na jioni yake akaingia uwanjani na kuonesha soka la kiwango kikubwa.

 

Moja ya mitanange mikali zaidi aliyocheza na kushangaza wengi ni ile ya kwanza kabisa kuichezea Dar es Salaam Young Africans dhidi ya Pamba ya Mwanza mwaka 1987, katika mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza. Alikuwa ndiyo kwanza amesajiliwa na vijana hao wa Jangwani akitokea klabu ya Tindo ya nyumbani kwao Tabora.

 

Baada ya kuonesha umahiri mkubwa kwa muda mrefu wa kupokea mipira, kupiga chenga za maudhi na kutoa pasi zinazokwenda utadhani zina macho, kila mchezaji wa Yanga, Pamba na mashabiki wote wakajua kazi yake kubwa ni kufanya hivyo na hana uwezo wala lengo lolote la kutikisa nyavu.


Kila alipopata mpira hata kama anaangaliana uso kwa uso na kipa wa Pamba, wakati huo Paul Rwechungura, hakujaribu hata mara moja kupiga shuti lolote zaidi ya kusubiri adui aje, ampige chenga, amtazame usoni ajue kama anakuja tena ampige ‘kanzu’ nyingine, kisha atoe pasi hata ya nyuma tena kwa kisigino, endapo atamuona mchezaji wa Yanga mwenye nafasi.

 

Mazoea hayo ya kila mtu uwanjani yalimpumbaza hata kipa Rwechungura ambaye wakati wote ambao ‘Kizota’ alipokea pasi alikuwa akiwaelekeza mabeki wake wamkabe nani, kazi aliyokuwa akiifanya kwa mazoea kuwa kiungo huyo mkabaji, yule ambaye siku hiyo alicheza namba 6 na kupanda mara kwa mara alikuwa akicheza soka la maonesho zaidi.


Wakati kila mmoja kuanzia wachezaji wote aliokuwa nao uwanjani, wachezaji wa akiba, makocha, mashabiki na kila mmoja akiamini hivyo, ‘Kizota’ alipokea pasi huku akiwa amelielekezea mgongo lango la Pamba na kama alivyokuwa amewajengea imani, mabeki wote walimkimbia na kwenda kuwabana washambuliaji waliotarajiwa angewagawia “pande” wasilete madhara (aah! kosa).


Ndivyo pia kipa Rwechungura alivyokuwa akiwaelekeza mabeki wake hao nani wa kumkaba ili akipewa pasi asipate nafasi ya kuudhibiti mpira.

 

Lakini wakati wakifanya hivyo huku mashabiki nao wakisubiri kuangalia ujuzi wake wa kupiga chenga, ‘Kizota’ aliyeipokea pasi hiyo kwa kifua aligeuka kwa kasi isiyotarajiwa huku mpira huo ukiwa umeganda palepale utadhani umewekewa gundi, akaushushia pajani kwa kasi ileile na kabla ya kugusa chini aliachia shuti lililokwenda moja kwa moja wavuni na kuuacha uwanja mzima ukichemka kwa nderemo, vifijo na hoihoi.


Ndivyo pia alivyo Haruna Moshi ‘Boban’ naye anavyocheza mpira wa kipaji na akili zaidi, ndiyo maana nimesema kwamba ni mmoja wa wachezaji wenye uwezo na ujuzi mkubwa dimbani. Lakini kwa vile hakuna kizuri kisichokuwa na kasoro, kiungo huyo pia ana matatizo lukuki kwa tabia zake.


Haaminiki kama alivyo mshambuliaji Mario Balotelli wa Manchester City ya England na timu ya taifa ya Italia (Azzuri). Ingawa naye ana kipaji na uwezo mkubwa uwanjani, lakini hakuna anayeweza kumwamini. Anaweza kufanya lolote wakati wowote na mahali popote bila kujali kama ni jema au ni hatari kwa timu yake. Bila shaka mtu pekee anayeweza kumvumilia ni kocha mkuu wa Manchester City na Mtaliano mwenzake, Roberto Mancini.

 

Inawezekana ‘Boban’ hawezi kuvumiliwa na mtu mwingine isipokuwa kaka yake, Idd Moshi ambaye pia ni kiungo mahiri aliyewahi kutokea hapa nchini, wazazi wake na ndugu zake wengine. Nje ya hapo ni kazi ngumu.


Ndiyo maana hata kocha mwenye sifa kubwa ya kuwavumilia wachezaji wake, kuwalea kama wanaye, kuwafundisha kwa juhudi na maarifa yake yote wawe na maadili mema nje na ndani ya uwanja, aliyewahi kumfundisha alipokuja kuinoa Taifa Stars, Marcio Maximo, hatimaye ‘alinawa’.


Akamtimua yeye pamoja na kipa namba moja wa Simba, Juma Kaseja, na kuapa kwamba asingewachukua tena kuichezea timu hiyo akiwa kocha wa Stars, ahadi aliyoitekeleza bila kuyumba hadi anaondoka na kurudi kwao Brazil mwaka 2010.

 

Ndiyo maana kuna watu wanauliza kuwa kama hata kocha Maximo naye alishindwa, nani anaweza kumvumilia mchezaji huyo?

By Jamhuri