Vijana wengi wa leo hapa nchini kwetu hawajui juu ya mambo aliyoyafanya Mwanadiplomasia huyu mahiri Dk. Salim Ahmed Salim. Dhumuni la makala hii si kuandika wasifu wa Dk. Salim, bali kuwajuza vijana nini alichofanya akiwa na umri mdogo sana.

Haijawahi kutokea tena katika historia ya nchi yetu mtu kuteuliwa kuwa balozi (siyo balozi wa nyumba kumi) – Balozi wa nchi za nje akiwa na umri wa miaka 22 tu. Salim alikuwa kijana mbichi mwaka 1964 mwanzoni alipoteuliwa na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Abeid Amani Karume kuwa Balozi wa Zanzibar nchini Misri.

Alikuwa hajaoa, ikabidi afanye hima kuchumbia na kumuoa Amne Rifai kabla hajaenda kuanza kazi mjini Cairo. Mwaka huo huo Zanzibar na Tanganyika zilipoungana na kuwa taifa la Tanzania, Mwalimu Nyerere alimteua Salim kuendelea kubaki Cairo kuwa Balozi wa Tanzania nchini humo.

Tangu mwaka huo wa 1964, Dk. Salim aliendelea kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania kwenye nchi mbalimbali – India 1965-1968, mwaka 1969 alipelekwa kuwa Balozi wa Jamhuri wa Watu wa China na Korea Kaskazini; kazi aliyoifanya kwa mwaka mmoja na kuhamishiwa Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1970. Akiwa India hakuridhika na ubalozi wake, aliingia darasani na kupata shahada iliyompatia cheo cha daktari.

Dk. Salim akiwa Balozi nchini China pamoja na umri wake mdogo, alifanya kazi nzuri sana ndani ya mwaka mmoja tu aliokuwa pale. Alikubalika, alijijengea na kulijengea Taifa letu heshima na urafiki mkubwa na Wachina; heshima na urafiki ambavyo vimedumu hadi sasa mpaka Wachina wameona anastahili tuzo waliyomtunukia ya Urafiki Uliotukuka.

Dk. Salim alikubalika haraka kutokana na uwezo wake na kutokana na Wachina walivyokuwa wakimheshimu ‘Mjamaa’ mwenzao Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Akawa yuko nyumbani. Aliruhusiwa kwenda kokote alikotaka nchini humo bila pingamizi lolote na alikuwa akipewa nafasi ya kuonana na viongozi wa juu nchini humo – Mwenyekiti Mao Tse Tung, Waziri Mkuu Chuo en Lai, wakati wowote hata usiku wa manane!

Miongoni mwa siri ya mafanikio yake Mheshimiwa Salim ni utu alionao, upendo kwa watu, ucheshi na umahiri wake katika kufanya kazi. Mchanganyiko wa sifa alizonazo vilifanya Mwalimu Nyerere aelewe haraka kwamba ana kijana wa kumuamini na kumpa majukumu mbalimbali. Kwa hiyo, uwezo huo wa Dk. Salim ndiyo ulimwezesha kufanya shughuli za kidiplomasia kwa ufanisi mkubwa popote Mwalimu alikompeleka.

Balozi Salim hakukaa sana Uchina, akapelekwa Umoja wa Mataifa mwaka 1970 na akiwa huko alikuwa pia Balozi wa Cuba, Jamaica, Trinidad & Tobago, Guyana na Barbados. Huko nako akawa amefika. Alifanya makubwa yatakayoendelea kukumbukwa daima. Wa-Cuba nao walimkubali, akawa rafiki mkubwa wa Rais Fidel Castrol na ujio wa Wacuba kusaidia shughuli za maendeleo nchini mwetu ni matokeo ya kazi nzuri ya Salim.

Wachina wao wana kila sababu ya kumkumbuka na kumtuza kwa sababu alipokuwa huko Umoja wa Mataifa, pamoja na umri wake mdogo wa miaka 28 alitumia akili nyingi alizonazo, akachanganya na utu na karisma aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu kuweza kukubalika na kuwafanya mabalozi wa nchi za Afrika wawe kitu kimoja.

Alikuwa msemaji mkuu si wa mabalozi wa nchi za Afrika tu, bali pia nchi za Dunia ya Tatu. Jambo hilo lilisaidia sana katika mapambano ya kuisaidia Jamhuri ya Watu wa China kuingizwa kwenye Umoja wa Mataifa. Ilikuwa haiingii akilini kwamba nchi yenye watu milioni 800 wakati huo, isiwe kwenye Umoja wa Mataifa kwa sababu tu Marekani walikuwa hawapendi na walitaka kuweka masharti yao kutokana siasa zao za ubeberu na ubepari dhidi ya Ukomunisti.

Wakati wa kushughulikia Wachina kuingia kwenye Umoja wa Mataifa, Dk. Salim alilivalia njuga sawasawa jambo hilo, akaubeba ujasiri wa Mwalimu, akachanganya na wa kwake binafsi na kuwapa shida sana Wamarekani na washirika wao. Mwisho wa mapambano hayo, Salim aliibuka kidedea pamoja na umri wake mdogo. Akawa ndio ‘habari ya mjini’ kwenye vyombo vya habari nchini Marekani na duniani!

Mwandishi wa habari mmoja akampakazia kwamba baada ya Jamhuri ya Watu wa China kutangazwa kwamba wameshinda kuingia kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa, Dk. Salim kwa ujana wake aliruka kutoka kwenye kiti chake na kuanza kucheza twist!- jambo ambalo halikuwa kweli. Ila ni kweli ushindi ule ulishangiliwa sana na mabalozi wa nchi za Kiafrika ambazo ndizo zilizokuwa mstari wa mbele kuipigania China zikiongozwa na Dk. Salim!

Miaka minane baadaye akiwa na umri wa miaka 37 alipendekezwa bila kupingwa na nchi za Kiafrika kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Wamarekani hawakumsamehe kwa kuwashinda kwenye suala la Jamhuri ya Watu wa China kuingia Umoja wa Mataifa. Pia hawakumsamehe kwa vile alikuwa mwiba katika kuwashambulia Marekani kwa kujiingiza na kuleta matatizo nchini Vietnam. Waliamua kumuadhibu Dk. Salim kwa kutumia kura yao ya turufu (veto) mara 16 kukataa asiwe Katibu Mkuu wa Umoja huo. Pia, walikuwa na hasira naye kwa sababu huko nyuma wakati Salim akiwa Balozi Umoja wa Mataifa, Mwalimu Nyerere aliwahi kumuadhiri Rais Reagan kwenye moja ya mikutano kati ya baadhi ya viongozi wa nchi zinazoendelea na wa nchi zilizoendelea, uliofanyika Cancun nchini Marekani. Hoja alizozitoa Mwalimu kwenye mkutano huo zilifanya Rais Reagan aonekane mbumbumbu!

Hata hivyo, muungwana Dk. Salim suala hilo la kunyimwa Ukatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa halikumkatisha tamaa. Kwake yeye na kwa Waafrika ilikuwa ni ushindi pia wa aina yake kwa sababu alikuwa amewasafishia njia mabalozi wengine wa Kiafrika waweze kupitishwa kugombea nafasi hiyo. Ndio maana baada ya hapo walifuata Makatibu Wakuu kutoka Afrika – Boutrous Ghali (Misri) na baadaye Kofi Annan (Ghana) na mpaka leo hakuna tena suala la Waafrika kutokubalika kwenye nafasi za uongozi za Umoja wa Mataifa.

Barani Afrika nako Salim alifanya kweli alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU). Haijawahi kutokea tena kwa mtu yeyote kuchaguliwa kwa vipindi vitatu mfululizo. Dk. Salim alikuwa Katibu Mkuu wa OAU kwa vipindi vitatu. Huko nako uongozi wake mahiri ulidhihirika kutokana na ubobezi wake katika masuala ya kidiplomasia. Dk. Salim alitoa mchango mkubwa sana katika kuhakikisha nchi za Kusini mwa Afrika ambazo zilikuwa bado zinatawaliwa, zinapata uhuru na ubaguzi wa rangi uliokuwa ukiendelea Afrika Kusini ulikomeshwa – na uhuru ukapatikana. Yapo na mengine mengi yanayohitaji makala nyingi tu!

Hapa nyumbani nako, mbali ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje mwaka 1980; mwaka 1984 Mwalimu Nyerere alimteua Dk. Salim kuwa Waziri Mkuu baada ya kifo cha Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine. Kama kawaida ya baadhi ya Watanzania wasiokuwa na nia njema, waliubeza uteuzi huo wakidhani kwamba mtu aliyekuwa nje ya nchi tangu akiwa na miaka 22 atawezaje kumudu Uwaziri Mkuu? Wakampachika na jina la TX (enzi hizo wataalam toka nje walioitwa ‘expatriates’ walikuwa wanaitwa ma-TX).

Dk. Salim akawakosoa wakosoaji hao wote. Huyu Mheshimiwa sana Dk. Salim Ahmed Salim ana sifa moja kubwa, nzuri sana na muhimu kwa viongozi wote kuwa nayo – UTU. Dk. Salim ana utu sana, ana upendo uliokithiri kwa binadamu wenziwe na ana huruma sana kwa wenye shida na wanyonge. Wakati wote huwa yuko tayari kumsaidia yeyote yule mwenye shida anayemwendea kuomba msaada wake.

Mwanadiplomasia huyu Mwalimu alipomteua kuwa Waziri Mkuu wa tano wa nchi yetu, wabezaji walidhani Mwalimu kakosea na kwamba viatu vya Uwaziri Mkuu havitamwenea ama havimfai, eti kwa sababu tu kaishi sana nje ya nchi. Hawakujua kwamba ili uwe kiongozi mzuri kwenye nchi iliyojaa maskini na wanyonge, utu na upendo kwa binadamu wote bila kubagua ndiyo silaha muhimu.

Hadi leo hii, ukienda mikoa ya Kusini mwa Tanzania – Lindi, Mtwara, Ruvuma nk. jina la Salim bado linavuma kutokana na utu wake aliouonyesha kwa wananchi wa mikoa hiyo alipokuwa Waziri Mkuu.

Baada ya kuvaa ‘viatu vya Waziri Mkuu Sokoine’ Salim alitembelea karibu mikoa yote nchini kwa nia ya kujua matatizo ya wananchi. Kipindi hicho nchi ilikuwa katika kipindi kigumu kutokana na mabeberu kuipiga vita Siasa ya Mwalimu Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea. Mwalimu naye, katu hakutaka kusalimu amri na kuwa kibaraka wa mabepari na mabeberu. Dk. Salim alikwishaishi na mabeberu kwa hiyo alijua namna ya kuwashughulikia.

Kutokana na hali ngumu ya uchumi iliyosababishwa na mapambano ya siasa za ujamaa na ubepari, kulitokea uhaba wa nguo na bidhaa nyingine nchini. Dk. Salim alipoenda mikoa ya Kusini alikuta watu wanavaa magunia! Wananchi wa mkoa mmoja, kwa heshima na unyenyekevu sana walimpa zawadi ya kanga (ndege)! Dk. Salim alielewa zawadi hiyo ilikuwa inatoa ujumbe kwamba akina mama hawana nguo wanahitaji kanga za kuvaa.

Aliporudi kutoka huko alikwenda kutoa ripoti kwa Mwalimu na kutoa ushauri. Haikupita muda Dk. Salim alirejea huko Kusini akiwa na shehena ya nguo. Ikawa zamu yake yeye kuwazawadia kina mama na kina baba wa mikoa hiyo kanga na nguo zilizokuwa zikihitajika. Alipata wapi shehena hiyo ya nguo? Uchina. Alikwenda kwa marafiki zake, marafiki wa Mwalimu, na marafiki wa nchi ya Tanzania, Wachina wakatoa nguo hizo ndugu zao Watanzania waje wavae!

Sasa vijana nyie wa Tanzania msiopenda kufuatilia mitandaoni mambo muhimu ya nchi yenu, jueni kwamba mitumba tunayovaa chimbuko lake ni Dk. Salim; ni yeye aliyeruhusu mitumba iingizwe nchini alipokuwa Waziri Mkuu.

Ni yeye Dk. Salim aliyeshughulikia majanga mbalimbali kwa ufanisi mkubwa, ukiacha hilo la wananchi kuvaa magunia, kulikuwa matatizo mengine mengi yaliyolikumba Taifa letu kipindi hicho – majanga ya ukame, matatizo yaliyokuwapo baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuungua kwa Benki Kuu, kuzama kwa kivuko Ziwa Victoria, Vita ya Kagera, na kadhalika. Ndani ya mwaka ule mmoja wa Uwaziri Mkuu wa Dk. Salim, kabla Mwalimu hajaachia madaraka mwaka 1985, alionyesha umahiri mkubwa wa kuongoza hata ndani ya nchi yake kama ilivyokuwa huko nje, akawaziba midogo waliombeza!

Mema na mazuri ya huyu Dk. Salim Ahmed Salim ni mengi mno yanahitaji vitabu kuyamaliza! Tuzo aliyopewa na ndugu zetu Wachina inapasa kutufikirisha sisi Watanzania na kujiuliza ni kwa kiasi gani tunathamini mchango mkubwa na kazi kubwa aliyoifanya mwanadiplomasia huyu katika kutuletea Watanzania maendeleo na sifa kubwa duniani. Tujiulize tumewahi kufanya nini kumuonyesha kuwa tunathamini huo mchango wake?

Wale kina Mama na waume zao wa mikoa ya Kusini walizaa watoto na kuwapa jina la Salim! Mpaka leo wanamkumbuka na kumuenzi kwa utu wake na uongozi wake uliotukuka. Wachina wametuonyesha njia, hatujachelewa. Sisi nasi, wananchi wa kawaida na viongozi wetu tufuate nyayo za Wachina na kumtunuku Dk. Salim heshima na tuzo anazostahili.

Hongera sana Dk. Salim Ahmed Salim!

Mwandishi wa makala hii, Anna Julia Mwansasu, ni Katibu Muhtasi mstaafu wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Anaishi Mpakani mwa Kivule na Msongola, Dar es Salaam. Anapatikana kwa simu: 0655774967

13044 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons