p.p1 {margin: 0.0px 0.0px 0.0px 0.0px; font: 12.0px ‘Myriad Pro’}
Rais John Magufuli alipotembelea Gereza Kuu la Butimba, Mwanza.

Mheshimiwa Rais John Magufuli, nachukua fursa hii kukushukuru na kukuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kukupa afya na umri mrefu ili uweze kuendelea kuwatumikia Watanzania, hasa wanyonge wa nchi yetu. 

Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu sana namna unavyoshughulikia changamoto mbalimbali mpaka ninafurahi, ingawa nimo gerezani tangu Agosti 25, 2014.

Mheshimiwa Rais, kwa moyo ule ule ambao umekuwa ukiuonyesha kwa wanyonge mbalimbali – moyo wa huruma na kusamehe makundi mbalimbali, nikuombe sana usikilize kilio changu na kunisaidia.

Mimi ni mkazi wa jijini Arusha. Nimekamatwa na kubambikizwa kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha. Kwa amri halali ya mahakama hiyo nimo ndani ya Gereza Kuu Arusha kwa miaka sita bila upelelezi kukamilika.

Mheshimiwa Rais, mimi Yunusu Salim Msuta, nimekamatwa na kubambikizwa kesi Na. 65/2014 eti ya kushawishi vijana kwenda kujiunga na kundi la kigaidi la Al-Shabaab, Somalia kwa madai ya polisi, kitu ambacho si cha kweli kabisa, kwani kinachosikitisha zaidi nimekamatwa katika mazingira ya kutatanisha, yaani nikitekeleza majukumu ya kiserikali mkoani Arusha kama nitakavyofafanua hapa chini.

Mheshimiwa Rais, Arusha kulishamiri migogoro ya Waislamu kugombea misikiti, hasa ile yenye vitega uchumi au kwa masilahi binafsi kwa kipindi kirefu, hasa baina ya madhehebu na madhehebu kwa kila kundi kujiona lina hadhi zaidi ya jingine hadi kufikia hatua mbaya.

Hali hiyo iliwafanya viongozi wa serikali kuingilia kati na baadhi ya misikiti ilifungwa kuepusha madhara au ugomvi zaidi. Kwa mfano, Msikiti wa Quba ulioko Levolosi ulifungwa; na Msikiti Mkuu Arusha ilifungwa.

Mheshimiwa Rais, RPC Lebaratus Sabasi kwa kubanwa na shughuli nyingi akampa jukumu OCD Gilles Muroto (kwa sasa ni RPC Dodoma) kushirikiana na viongozi wengine kuitisha vikao ili kutatua mgogoro huo. 

Kilichofanyika kwa usimamizi wa OCD huyo, aliandikia taasisi na madhehebu mbalimbali baada ya msikiti kufungwa ili kuja kujadili namna nzuri ya kumaliza mizozo hiyo.

Baada ya barua hizo kusambazwa, wahusika walitakiwa kukutana katika ukumbi wa Police Mess Machi 29, 2014 kwa majadiliano zaidi. Taasisi za kidini kama vile BAKWATA ‘A’, BAKWATA ‘B’ na nyingine kama 15 zilihudhuria. 

Kikao kiliweka ajenda mezani kwa usimamizi wa OCD huyo pamoja na viongozi wa serikali na dini. Baada ya majadiliano ya muda mrefu tukakubaliana kuunda kamati ya watu 15 kutoka kila taasisi ikipewa jukumu la kutafuta vyanzo na namna ya kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo kisha kupeleka ripoti kwa OCD ili kuwaita viongozi wa dini na kuwapa mrejesho wa kilichopatikana kupitia kamati hiyo.

Mheshimiwa Rais, mimi niliteuliwa niwe miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo na ndiye nilikuwa kijana pekee mdogo kuliko wote mwenye miaka 23 (mwaka 2014). Pale Police Mess nakumbuka kila aliyehudhuria ukumbini alipewa Sh 20,000 kama nauli.

Mheshimiwa Rais, tulipokabidhiwa jukumu hilo tulikaa vikao mbalimbali na kuwahoji viongozi waliokuwa wakigombea misikiti hasa Quba na kila baada ya kikao tulimpelekea OCD yatokanayo na kikao. 

Ninawakumbuka viongozi wote tuliokuwa nao kwenye kamati, lakini ninahifadhi majina yao, hata wale tuliowahoji ninawakumbuka pia.

Mheshimiwa Rais, Mei 14, 2014 OCD aliwajulisha viongozi hao wa dini tukutane Arusha Day ili kuwasomea ripoti halisi kuhusu tulichokigundua na hapo alikuwepo ODC huyo, ambapo kama kawaida katibu na mwenyekiti wa kamati waliniteua mimi nisome ripoti hiyo kwa waliohudhuria. 

Nilisoma ripoti yote, lakini michango iliyotolewa baada ya kumaliza kusoma ripoti, ilionyesha kutoridhika kwa baadhi yao.

Mheshimiwa Rais, tulikubaliana kwamba ule Msikiti wa Quba wenye mgogoro uliofungwa usimamiwe na kamati yetu ya watu 15 mpaka pale uchaguzi utakapoitishwa kwa mujibu wa ratiba na katiba ya taasisi husika, lakini wiki iliyofuata Waislamu, yaani makundi yenye kutaka madaraka waliendelea kwenda kuswalia pale nje ya Msikiti wa Quba kwa kuhofu kundi moja lisije kuingia na kujimilikisha msikiti huo.

Wakati huo huo, sisi kama kamati tuliendelea kuwasihi wavute subira mpaka pale mambo yatakapokaa sawa na kila Ijumaa polisi walikuwa wanakuwapo pale msikitini ili kusitokee vurugu baina ya makundi   husika. 

Nakumbuka siku moja baada ya kuona hali si nzuri, siku ya Ijumaa nikiwa nimebeba begi langu mgongoni lenye nyaraka (documents) zinazohusu mgogoro huo pamoja na ripoti ya kamati, nilipita pale nikienda Msikiti Mkuu nikitokea Shule ya Swiff Academic kufundisha. 

Nikapita pale nikakutana na hali hiyo. Baadhi ya watu waliokuwa kwenye kamati ya usuluhishi wakaniomba kuwatuliza hao Waislamu ikiwamo kuwaonyesha tulichokubaliana, lakini kabla sijasimama nje ya msikiti kwa kuwa kulitanda magari ya polisi kila kona ya eneo hilo, nilikwenda moja kwa moja kwa askari mmoja maarufu kwa jina ‘Bwaksa’ ili kushauriana kuhusu hali hiyo. 

Akaniambia niende kuwaambia waondoke pale, lakini njia pekee iliyokuwa inaendana na hali ya wakati huo ni kuwatuliza, wakishakaa wako tayari kusikiliza ndipo niweze kutoa maelekezo yoyote. 

Na hicho ndicho kilichofanyika baada ya kukaa chini pale barabarani huku wengine wakiwa wamesimama, nilichowaambia ni kwamba: “TUTUMIE ELIMU ZETU VIZURI ILI KUNUFAISHA JAMII,  SI KUWAYUMBISHA.”

Mheshimiwa Rais, polisi baada ya kunikamata walidai waliniona eneo hilo nikihubiri. Nikawaomba wanipe mkanda au video waliyorekodi tuone nilichozungumza. Hawakunipa. 

Nilishangaa mno kilichotokea ndicho hiki ninachokilalamikia kwa kuonekana nikitekeleza majukumu niliyopewa na viongozi wangu wa serikali. Inauma sana.

Mheshimiwa Rais, nilipomaliza kuzungumza na kutoa maelekezo baadhi yao walielewa na kuondoka. Mimi niliondoka zangu. Sikujua kilichoendelea nyuma, lakini ninakumbuka Juni 12, 2014 Ijumaa, makundi hayo yalikwenda tena pale msikitini kwa sababu walisikia Mahakama ya Ardhi inatoa hukumu kuhusu msikiti huo. 

Mimi na wenzangu tulichukua hiyo hukumu tukaenda nayo pale msikitini ambayo ilisema Waislamu wayamalize wao wenyewe. Lakini tulipofika tulikuta mlango umefunguliwa kwa ndani na polisi wanawatafuta vijana waliohusika ambao tulikuta kati yao wamewashikilia vijana wawili – mmoja wao ni kinyozi eneo hilo akiwa na wenzake. 

Nilishangaa askari Bwaksa akaagiza polisi waliokuwapo wanipandishe kwenye gari niende polisi nikatoe maelezo eti nitakuwa ninawajua wahusika wengine.

Baadaye aliletwa imamu wa msikiti huo tukawa wanne ambao tulikaa kituoni siku mbili tukadhaminiwa. Tukawa tunakwenda kuripoti kwa tuhuma za kuvunja msikiti. Baadaye tukaambiwa yamekwisha, tusiripoti tena.

Mheshimiwa Rais, Juni, 2014 nilitumika kama mkalimani katika mahakama niliyoshitakiwa mbele ya Mheshimiwa Mnguruta.  Hayo yote niliyafanya kwa moyo mmoja na usikivu kwa masilahi ya taifa langu. Pamoja na yote hayo, Agosti 9, 2014 nilikamatwa nikatoa maelezo Agosti 24, 2014.

Agosti 25, 2014 nilipandishwa mahakamani na kusomewa kesi tajwa. Hakika inauma, kwani ninakumbuka tukiwa rumande polisi waliulizana: “Tumpe kesi gani huyu?” Mwishowe nikapewa kesi ya kushawishi kinyume cha ukweli ili kukosa dhamana. 

Nikashitakiwa kwa kifungu Na. 18(1)- ugaidi. Kwanini isiwe kushawishi chini ya kifungu Na. 390 Penal Code ili nipate dhamana? Sijui makusudi ni nini hasa.

Mheshimiwa Rais, ninasikitika kubambikizwa kesi hii nikitekeleza majukumu niliyopewa na serikali, kwani kama si hivyo nisingeonekana maeneo hayo. 

Mimi si kiongozi wa dini sehemu yoyote ile. Nilisikiliza na kuwatii viongozi wangu. Badala ya shukrani, ndiyo hivyo tena.

Mheshimiwa Rais, kwa kuwa yamepita, mimi nimesamehe walionitendea. Nakuomba unisaidie nikaangalie familia yangu. Wanateseka kwa miaka mingi. 

Asante.

Wako mtiifu,

Mahabusu Na. 2479/2014 Yunusu Salimu,

Gereza Kuu Arusha,

S.L.P 309,

ARUSHA.

By Jamhuri