Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein amefanya uteuzi wa viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Jumamosi Septemba 29, 2018 na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Abdulhamid Yahya Mzee, inaeleza kuwa Dk Shein amemteua Dk Abdulla Mohamed Juma kuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii.

Dk Juma anachukua nafasi ya Dk Vuai Idd Lila ambaye atapangiwa kazi nyengine.

Pia, Dk Shein amemteua Khalfan Sheikh Saleh kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Serikali wa Uchapaji na mpigachapa mkuu wa Serikali, anachukua nafasi ya Mohamed Suleiman Khatib atakayepangiwa kazi nyingine.

Katika uteuzi huo, Dk Shein amemteua Said Juma Ahmada kuwa Mkurugenzi wa Baraza la manispaa ya mjini Unguja akichukua nafasi ya Aboud Hassan Serenge ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria.

Pia, amemteua Amour Ali Mussa kuwa mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi “A”kuchukua nafasi ya Said Juma Ahmada ambaye amehamishiwa Manispaa ya Mjini.

Rais Shein amemteua Ali Abdulla Said Natepe kuwa mkurugenzi wa baraza la manispaa ya Magharibi “B”akichukua nafasi ya Amour Ali Mussa ambaye amehamishiwa Manispaa ya Magharibi “A”.

Taarifa hiyo imesema uteuzi huo unaanza Oktoba Mosi, 2018.

1069 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!