Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amewataka askari polisi kumcha Mungu na kutenda haki.

Sirro ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Septemba 29, 2018 katika mazishi ya IGP mstaafu Samuel Pundugu aliyezikwa katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Pundugu aliyekuwa IGP wa tatu tangu Tanzania ipate uhuru, alifariki dunia Septemba 26, 2018 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Ibada ya mazishi imefanyika nyumbani kwake Kigamboni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na IGP Sirro.

Akizungumza katika ibada ya mazishi Sirro amesema marehemu ameacha alama ya kumcha Mungu katika jeshi hilo.

“Bila yeye jeshi lisingekuwa kama lilivyo sasa. Sisi tuliopewa kijiti hiki tutatenda kama alivyotaka,” amesema Sirro

Akizungumzia familia ya marehemu yenye watoto 11, wajuu na vitukuu, IGP Sirro amesema miongoni kwa watoto hao mmoja wao ni mchungaji na kuwataka askari kuiga mfano huo na kutenda haki.

“Mtoto wa line Polisi ameweza kuwa mchungaji, Polisi tujifunze. Familia ya marehemu inamjali sana Mungu. Tukumbuke kwenda kanisani na misikitini walau siku moja. Leo tunayo haya magwanda kesho hatutakuwa nayo. Tutende haki,” amesema Sirro

Kwa upande wake, IGP mstaafu Omari Mahita amesema marehemu Pundugu aliwapokea katika jeshi hilo wakitokea kwenye vyuo vya ualimu na aliwalea hadi kufikia vyeo vya juu.

Amesema kifo hakizoeleki hata kwa wachungaji, mashehe hivyo akawataka waombolezaji kumwomba Mungu awaweke tayari na siku ya mwisho.

Awali, mchungaji Andrew Fabian wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (KLPT), amewaasa waombolezaji kujiweka tayari kwani hakuna mtu anayejua siku ya kufa.

Viongozi wengine waliohudhuria Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo, Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Davis Mwamunyange na maofisa wengine wa majeshi ya ulinzi na usalama.

Akisoma wasifu wa marehemu, kamishna msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeki amesema alizaliwa mwaka 1928 wilayani Bariadi na alikuwa IGP wa tatu tangu Tanzania ipate Uhuru mwaka 1961.

By Jamhuri