Ni jambo lisilokuwa na ubishi kuwa elimu ndicho chanzo muhimu kabisa kitakachomletea maendeleo na ukombozi wa kweli wa  mwanadamu, elimu inawatoa wanadamu katika gugu la ujinga.
Umuhimu wa elimu umeelezwa kwa kina katika vitabu ya dini na katika vitabu vingine, lakini pia mafundisho ya wanafalsafa wengi wamejikita katika kuhimiza watu kusoma kujiongezea maarifa katika fani mbalimbali.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, aliwahi kusema; “Elimu ni silaha madhubuti inayoweza kubadili dunia.” Umuhimu wa elimu namna ulivyosisitizwa na wanafalsafa wengi, hauwezi kupimwa katika kipimo chochote kile.
Ulimwengu wa leo unavyozidi kusonga mbele kwa wavumbuzi kutumia vipawa vyao, elimu itamsaidia mwanadamu kutoachwa nyuma katika uvumbuzi na kazi za stadi za maisha.
Katika dunia inayoungana kimawasiliano na kugeuka kuwa kijisehemu kidogo, elimu inakuwa nguzo, hazina na daraja litakalomvusha binadamu katika hali yake ya unyoge wa fikra, mawazo na atayatanua maisha yake kuendana na maendeleo endelevu.
Katika kipindi cha miaka saba ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, sekta ya elimu imeonesha mafanikio makubwa na zaidi pale mkakati wa Serikali kuongeza idadi ya shule za sekondari ulivyosimamiwa kwa umakini utekelezaji wake.
Zanzibar imetekeleza malengo ya milenia kuhusu elimu. Idadi ya shule zimeongezeka ambapo shule za maandalizi sasa zimefikia 270 kutoka 238 mwaka 2010.
Mbali na kufikia kiwango cha asilimia 100 ya uandikishaji wa watoto wanaoingia darasa la kwanza, pia hakuna mwanafunzi anayetembea umbali wa zaidi ya kilomita tano kutafuta elimu.
 Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, zinaonesha kuwa shule za msingi zimeongezeka kutoka 299 mwaka 2010 hadi shule 370 mwaka 2016, ambapo Serikali inajiandaa kujenga shule mpya 10 za ghorofa kuongeza nafasi kwa wanafunzi.
Hivi karibuni, Rais Dk. Shein alisema kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, Serikali inatekeleza mradi inaohusiana na masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika shule za msingi 248 Unguja na Pemba.
Shule hizo zimepatiwa vifaa mbalimbali na kompyuta, vitabu na vifaa vingine vya ufundi wa TEHAMA pamoja na kuwapatia mafunzo watendaji wanaosimamia mradi huo.
Uongozi wa Rais Shein umetilia mkazo suala zima la kuimarisha mazingira ya ufundishaji na usomaji, ambapo walimu wamekuwa wakiendelea kupatiwa mafunzo mbalimbali ya kuwaongezea ujuzi.
Wanafunzi nao wameendelea kujengewa mazingira bora zaidi ya kujifunzia ikiwa pamoja na kujenga shule mpya 21 kuongeza nafasi, huku SMZ ikizifanyia matengenezo makubwa shule sita za sekondari Unguja na Pemba na kuzipatia vitabu, vifaa vya maabara na samani.
Mwenye macho haambiwi tazama, katika kipindi cha miaka saba ya uongozi wa Rais Dk Shein, Serikali imejenga shule mpya za sekondari 19 Unguja na Pemba.
Kila mmoja ameshuhudia ujenzi wa shule 19 ambazo zimejengwa kwa gharama za fedha za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambazo ni za kisasa na tena ni miongoni mwa shule za mfano kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Tunaona Serikali imechukua jitihada maalumu kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalumu wanapata haki yao ya elimu katika shule mbalimbali, kupitia mpango wa elimu mjumuisho.
Serikali imeimarisha mafunzo ya elimu ya amali na ufundi katika vituo vya Mwanakwerekwe, Mkokotoni na Vitongoji.
Vituo hivyo vimetoa mchango mkubwa wa kuwapatia vijana mafunzo mbalimbali ya fani za ufundi zikiwamo uashi, useremala, ushonaji, uhunzi, upishi, uchoraji, ufundi bomba, ufundi umeme, magari, majokofu, teknolojia ya habari na fani nyinginezo.
Zanzibar imeshuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu kwani mpaka sasa kuna vyuo vya elimu ya juu vitatu; Chuo cha Elimu Chukwani, Chuo Kikuu cha Tunguu na kile cha Serikali yaani Zanzibar State University (SUZA) ambavyo kwa pamoja vyuo hivyo vimekuwa vikichangia kwa kasi ukuaji wa elimu na upatikanaji wa wataalamu wa fani mbalimbali.
Itakumbukwa kwamba mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964, Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, alitangaza elimu bure kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba.
Haya ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya uongozi wa Rais Dk. Shein katika kukuza sekta ya elimu nchini, lakini pia mafanikio haya yanamuhusu kila mmoja wetu kuona sasa wanaweza kutembea kifua mbele katika macho ya ulimwengu kuwa hatukuachwa nyuma na matakwa ya kimataifa.

By Jamhuri