Takriban miaka miwili baada ya Rais John Magufuli kuvunja Mamlaka ya Kuendeleza Makao Makuu Dodoma (CDA) na kuitangaza Dodoma kuwa jiji Aprili mwaka huu, ujenzi wa miundombinu ya kisasa, zikiwamo barabara mpya unaozingatia viwango vya kimataifa, ulianza kwa kasi ukilenga kulifanya jiji hilo kuwa salama zaidi Afrika.

Viwango vya ujenzi wa barabara mpya inayoitwa Waziri Mkuu, vilivyoshuhudiwa na JAMHURI vinakidhi viwango vya usalama vinavyopendekezwa kimataifa na kupigiwa chapuo na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Barabara hiyo ina upana wa kutosha huku alama zote muhimu za ardhini zikiwa zimechorwa na taa za usalama barabani zikiwa zinafanya kazi. Aidha, zimetengwa njia mahsusi kwa ajili ya watembea kwa miguu na watu eanaofanya mazoezi ya kukimbia, waendesha baiskeli na bodaboda kama njia ya kuhakikisha kuwa watumiaji wote barabara wako salama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, anasema tayari ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa kuzingatia viwango vya kisasa vya kimataifa umeshaanza na kazi hiyo itakapokamilika Dodoma litakuwa jiji la mfano barani Afrika. Aidha, kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kuondoa msongamano wa magari katika barabara za jiji.

Kunambi anasema kulingana na mpango mji huo, kutakuwa na barabara nne za mzunguko (ring road) ambazo zitaunganisha barabara kuu zitokazo mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Singida na Arusha.

Kunambi anasema kwa kuzingatia kuwa mkoa wa Dodoma umeunganisha nchi za Afrika, kutokana na ukweli kwamba itapita barabara kuu inayotoka Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Cairo, Misri, itasaidia kuboresha zaidi barabara za Dodoma.

“Ujenzi huo umeanza licha ya kuwa kuna marekebisho kidogo ya kisheria kulingana na mipango miji. Lakini kama unavyoona ujenzi wa barabara maeneo kama Kizota na Kilimani umeshaanza, na barabara zote zinazingatia viwango vinavyotakiwa kimataifa.

 “Iwapo watu wakiamua kutumia baiskeli badala ya magari kwenda kazini watafanya hivyo, wakiamua kutembea kwa miguu pia ni sawa kwa sababu barabara zitakuwa salama na bora kwa watumiaji wote kwa sababu haziingiliani,” anasema Kunambi.

Ujenzi huo utakapokamilika ni dhahiri changamoto ya barabara kwa wafanya mazoezi itakuwa imepata suluhisho jambo litakaloyoa hamasa kwa watu wengine kufanya mazoezi hivyo kuunga mkono juhudi za serikali za kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.

Ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye viwango vya kimataifa jijini Dodoma pia utasaidia kuimarisha uchumi na uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza uzalishaji wa hewa chafu, kwani watumaji wake wataweza kutumia usafiri wa baiskeli badala ya magari kama inavyofanika katika nchi zilizoendelea.

Hatua ya serikali kuja na mkakati unaolenga kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa yasioambukiza unatokana na ukweli kuwa maradhi hayo yanatishia uhai wa Watanzania kwa kiwango kinachotisha kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la afya Duniani (WHO) ya mwaka 2016 inayojulikana kama “Risk of Premature Death due to NCD’s”. Ripoti hiyo inabainisha kuwa magonjwa hayo yakadiriwa kuchangia vifo kwa asilimia 33 nchini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza vimeongezeka mara mbili zaidi kutoka asilimia 19 mwaka 1990, hadi kufikia asilimia 34 kwa mwaka 2015. Ripoti hiyo inapendekeza kufanya mazoezi kama moja ya njia ya kupunguza magonjwa hayo.

Lakini pendekezo hilo limekuja huku kukiwa na changamoto ya miundombinu ya barabara isiyozingatia viwango vinavtotakiwa kama vile barabara za watembea kwa miguu, barabara za waendesha baiskeli pamoja na alama za barabarani.

Barabara nyingi nchini zimejengwa bila kufuata viwango vya kimataifa hivyo kusababisha changamoto kwa watumiaji wake wakiwemo wanaofanya mazoezi, wanaotumia baiskeli kwenda kazini au kutembea kwa miguu kukosa barabara maalumu na hatimaye kutumia barabara za vyombo vya moto na hivyo kuhatarisha maisha yao.

Mwenyekiti wa klabu ya mazoezi ya Dodoma Fitness Jogging and Sports, John Banda, anasema iwapo kutakuwepo kwa barabara za watembea kwa miguu itasaidia wafanya mazoezi kuwa na eneo rafiki tofauti na sasa ambapo wanatumia barabara zinazotumiwa na vyombo vya moto hivyo kuhatarisha maisha yao na hata wao wenyewe kuwa kero kwa watumiaji wengine wa barabara.

Banda anasema wanachama hao zaidi ya mia moja wamekuwa wakifanya mazoezi kwa hofu kubwa kwani wamekuwa wakitumia barabara zinazopita magari na pikipiki jambo ambalo limekuwa likiwakatisha tamaa baadhi yao.

“Mazoezi tunafanya kwenye viwanja vya michezo na barabarani, lakini ukweli barabara tunazotumia siyo zetu, ni za vyombo vya moto, sisi tunatakiwa kufanyia mazoezi kwenye barabara za watembea kwa miguu, lakini hazipo,” anasema Banda.

Mwenyekiti wa klabu ya Muungano Jogging and Sport, Amin Mushi, anasema licha ya kukabiliwa na changamoto ya ufinyu wa barabara, wamekuwa wakisababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara hivyo kuitaka serikali kuyafanya makao makuu ya nchi yaendane na viwango vya kimataifa.

“Sisi hatuna kabisa barabara kwa ajili ya mazoezi, tunatumia za magari, wakati mwingine tunalazimisha magari yasimame yatusubiri tupite, kwa hiyo tunawasababisha wenzetu usumbufu na kuwachelewesha kwenye majukumu yao,” anasema Mushi.

Kauli hizo zimeungwa mkono na Mkurugenzi Msaidizi kutoka kitengo cha magonjwa yasiyoambukiza, Sara Maongezi, ambaye amekiri kwamba mkakati wa kuhamisha wananchi kufanya mazoezi umeshindwa kuonyesha mafanikio yaliyokusudiwa kwa sababu baadhi ya watu wanashidwa kujitokeza kwenye mazoezi kwa kuhofia usalama wao wawapo barabarani.

Anasema mkoa wa Dar es Salaam umeongeza hamasa ya ufanyaji wa mazoezi lakini changamoto inayolalamikiwa na wananchi ni ukosefu wa miundombinu rafiki ya barabara itakayowawezesha watembea kwa miguu, wapanda baiskeli au wakimbiaji kuwa salama kwa sababu mipango ya ujenzi barabara haukuzingatia hayo.

Maongezi anasema wanaendelea kuzungumza na wizara husika ili suala la usalama kwa ajili ya watu wanaofanya mazoezi liingizwe kwenye mkakati utakaoweka mabadiliko kwenye miradi ya ujenzi wa barabara kwa kuzingatia uwepo wa barabara maalumu kwa ajili ya watembea kwa miguu na wafanya mazoezi.

Changamoto hii inakumba majiji mengi bara la Afrika yanayokuwa kwa kasi. Kutokana na hali hiyo, ripoti ya jarida la City Metric (2018) linashauri kuwa wakati umefika sasa kwa watunga sera Afrika, kuzingatia zaidi waenda kwa miguu na siyo idadi ya magari katika mipango miji yao. Dodoma iko mbioni kuvuka kigingi hiki.

Taarifa kutoka kitengo cha Usalama Barabarani nchini zinasema kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2017 hadi 2018 ajali za barabarani zimepungua kutoka 5,574 hadi 3,732 sawa na wastani wa asilimia 33, huku idadi ya vifo navyo vikipungua kutoka 2,581 hadi vifo 1,788 sawa na asilimia 31.

Katika ripoti ya WHO ya mwezi Disemba, 2018 ijulikanayo kama Global Status Report on Road Safety 2018, imeelezwa kuwa matukio ya ajali za barabarani yanayosababisha vifo na majeruhi kuwa bado ni tatizo sugu. Ripoti hiyo inasema inakadiriwa kuwa kundi la watembea kwa miguu ndilo lililoongoza kwa asilimia 31 ya vifo vitokanavyo na ajali za barabarani.

Hata hivyo, ripoti kutoka kitengo cha Usalama Barabarani mkoa wa Dodoma, inaonyesha kuwa mwaka 2017 kulitokea ajali 218 na kusababisha vifo 92 huku mwaka 2018 zikitokea ajali 212 na kusababisha vifo 78.

Utafiti uliofanywa na Wakala wa Mradi wa Mabasi ya Mwendokasi (DART), Mhandisi Jumbe Katala, kwa mwaka 2012, umebaini madhara ya kiafya kwa binadamu kama moja ya hasara zitokanazo na foleni katika jiji la Dar es Salaam.

Ameyataja maradhi yatokanayo na foleni kwua ni pamoja na magonjwa ya moyo na akili yanayotokana na kuvuta hewa chafu hususani miongoni mwa madereva. Pia kuna maradhi ya pumu, mfumo wa hewa pamoja na mzio utokanao na mafuta.

Kuna uhusiano mkubwa kati ya barabara salama na afya njema kwa wakazi wa jiji lolote duniani kwani kwa mujibu wa WHO maisha ya watu milioni tano yanaweza kuokolewa katika muongo iwapo miundombinu ya barabara itakuwa salama.

By Jamhuri