‘Dokta Nchia’: Mpishi wa Nyerere

Asema Mwalimu alipofungwa bao hakula

“Dokta Nchia”, kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alivyopenda kumuita, hakuwa daktari wa binadamu au mifugo. Alikuwa daktari wa mlo.

Evaristus Nchia (50), Mwalimu alimwita “dokta” kutokana na utundu wake wa mapishi ya vyakula, hali iliyomfanya Mwalimu amvulie kofia na kumpa hadhi ya “udokta”.

Historia yake ilianza Novemba 1991 alipoajiriwa Ofisi ya Rais, Idara ya Utumishi, ambayo kwa sasa inaitwa Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Ghafla, anasema Desemba Mosi, mwaka huo akatakiwa aripoti Msasani nyumbani kwa Mwalimu, na baadaye Butiama akiwa kama mmoja wa wapishi wa Baba wa Taifa.

 

“Mpishi alihitajika kwa Mwalimu baada ya wengine kusita kwenda kuishi naye kijijini. Nilipoambiwa nakwenda Msasani kuripoti, kwa kweli sikuamini kama kuna siku naweza, si tu kuwa mtumishi wa Mwalimu, bali hata kumsogelea.

“Sikuamini kama nimefika kwa Baba wa Taifa. Nikasafiri hadi Butiama. Nikaona mazingira tofauti – ya kijijini – na mtu ambaye ni maarufu si nchini au Afrika tu, bali ulimwenguni kote. Nikastaajabu kuona mazingira mazuri na ya asili.

“Kitendo cha mimi kuwa mpishi wa mtu huyu mkubwa duniani kilinipa wasiwasi. Nilikaa nikifanya kazi yangu ya upishi kwa wiki nzima bila kukutana na Mwalimu ana kwa ana. Mara zote nilikuwa napata shida, najiuliza; ‘Hivi kweli mimi naweza kuzungumza na Mwalimu ambaye ni mtu wa kimataifa?’

“Siku moja nikapata salamu kuwa Mwalimu amepata taarifa kuna mpishi amefika, lakini hajamwona, hivyo angependa kumwona. Nikaletewa taarifa na Mzee Batao (Lawrence Batao aliyekuwa Katibu wa Mwalimu). Niliogopa sana. Mzee Batao akanipeleka ofisini kwake. Mwalimu alinikaribisha vizuri sana. Akaniuliza swali; ‘Umekuja kijijini utaweza kuishi huku?” Nikamjibu, ‘Wewe Mwalimu umeweza, na mimi nitaweza’.

“Akaniambia, ‘utaratibu hapa nyumbani kwangu ni kilimo. Uko tayari kwenda shamba?’ Nikasema, ‘nipo tayari’. Nikadhani atanipa jembe. Akasema haya twende. Tukatoka nje na akanitaka tuingie kwenye gari lake. He! Mimi napanda gari moja na Mwalimu? Sikuamini. Nikaogopa, lakini nikajipa faraja. Tukaenda hadi Kyarano. Nikakuta mahindi makubwa – ya miezi miwili hivi – akanionesha shamba akasema, ‘hili shamba unaliona? Shamba hili ni lako’. Ukubwa wake ulikuwa ekari mbili.

“Kwa kweli shamba hilo lilinisaidia sana. Kuanzia hapo nikawa mkulima. Akawa ananipa mimi na wenzangu pembejeo za kilimo. Aliniambia kuwa shamba lile litanisaidia maana siwezi kuishi kwa mshahara pekee wakati naweza kulima na kujipatia chakula. Kwa kweli Mwalimu alikuwa mtu mwenye upendo na wa ajabu sana. Nilichogundua ni kwamba alitaka watu wajitegemee kwa vitendo,” anasema Nchia.

Alivyomfahamu Mwalimu

“Kitu kikubwa sana alichokuwa anafundisha ni kujitegemea. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa kujitegemea kama vile alivyoonesha mfano wa kunipa shamba. Ujue unaishi kijijini, lazima ulime pamoja na kazi ile unayoifanya ambayo ni ya mwisho wa mwezi, lakini je, utakabiliana na mwisho wa mwezi bila kuwa na kitu chochote pembeni? Haiwezekani. Kwa hiyo tulikuwa tunaishi kwa njia hiyo na Mwalimu.

Nilivyopokewa Butiama

“Kilichonipeleka ni kuangalia chakula cha Mwalimu. Sasa nipo kijijini, na mimi nilijifunza vyakula tofauti na yeye alivyokuwa anapendelea wakati alipokuwa kijijini, maana kabla ya hapo nilikuwa nafanya kazi katika hoteli za kitalii kule Seronera. Mimi nilizoea kwenye mahoteli, tofauti na yeye kwenye maisha yake ya kijijini. Kwa hiyo ikanilazimu sasa nijue ni kitu gani Mwalimu anapendelea. Chakula aina gani na kwa muda gani?

“Mwalimu alikuwa anapendelea ugali. Ugali wake ni mchanganyiko wa nafaka – mtama na muhogo. Vinachanganywa. Kwa hiyo mchana alikuwa anapenda kula ugali huo na mboga. Ugali japo unaitwa wa ulezi, lakini ulikuwa unachanganywa nafaka tatu – ulezi, mtama na muhogo. Ni chakula kizuri sana kwa kweli. Mchana anakula chakula hicho. Kitoweo kilikuwa samaki, hasa samaki wakavu kule kwao kuna samaki wanaitwa vibambara (ng’onda), alikuwa anapenda sana vibambara vya sato; au nyama ya ng’ombe iliyokaushwa…kuna kitu kinaitwa kimoro, sijui lugha yake. Kiswahili najua ni nyama iliyokaushwa. Kizanaki wanaita mkutira. Alikuwa anapenda sana.

“Jioni wewe kama mpishi unapanga menu yako vizuri. Chakula cha jioni kwa wastani kinatakiwa kiwe chakula ambacho si cha kumsumbua usiku, si sisi tumezoea kula ushibe tu. Tulikuwa tunapika wali kidogo, ndizi kidogo na matunda. Alikuwa anapenda hicho.

“Vilevile wakati huo kinywaji alikuwa anapenda, lakini Mwalimu hakuwa mnywaji wa kusema mnywaji. Hakuwa anakunywa kinywaji kama ulevi. Hapana. Hapana. Mpaka naondoka sikupata kumwona Mwalimu amekunywa pombe nikaona huyu mzee vipi mbona anaimba! Akiimba alikuwa anaimba kwa furaha zake mwenyewe. Anaimba nyimbo za dini. Alikuwa anakunywa bia yake moja tu, ilikuwa Pilsner.

“Halafu na wine moja Mateus. Alikuwa anapendelea kunywa hiyo. Mateus akishakunywa ka-glasi kake kamoja, basi. Anakunywa huku anaendelea kucheza bao. Burudani yake kubwa ni bao. Wapinzani wake walikuwa Nyang’ombe – namkumbuka kwa jina moja, halafu na mdogo wake Daniel Ihunyo. Hao ndiyo wapinzani wake. Na akifungwa anaweza hata chakula asile vizuri, akifungwa anaweza asile. Hata kama umeenda kumwita anacheza bao, ‘Bwana chakula kipo tayari’ hawezi kutoka mpaka ahakikishe na yeye ameshinda.”

Mwalimu na wageni

“Mzee hakuwa na ubaguzi. Pamoja na kwamba alikuwa anaondoka kwenda shambani na vijana wa pale kijijini, na siyo wajukuu peke yake, na wenyeji wa pale kijijini na wengine wanatoka huko vijiji vya jirani, lakini wote walikuwa meza moja. Wanakula meza moja. Meza kama meza ilikuwa na viti vyake, wengine tunawaandalia pembeni, lakini wengi wao walikuwa wanakula meza moja. Na alikuwa hachagui huyu ni nani, huyu nani, hapana. Wote alikuwa anawaita ‘njooni hapa, sasa tunakula chakula’. Kama anakula ule ugali niliokuambia, anakata yeye na wale wengine wote anawapa kile chakula.

Shambani

“Kupeleka chakula shambani ilitegemeana na siku anazoshinda huko. Kama siku wanashinda shambani walikuwa wanapelekewa uji wa ulezi kwenye makeni. Kama wanafika mpaka mchana walikuwa wanapelekewa makande. Siyo ugali. Lakini yeye alikuwa anapelekewa soda tu. Alikuwa hali chochote. Soda alikuwa akinywa Fanta au maji. Maji alikuwa hanywi sana. Na kwa kweli maji yalikuwa yanaweza yakarudi, lakini soda anakunywa.

“Wakati nimefika (Butiama) nilikuwa ana mtindo wa kutengeneza aina fulani ya biskuti. Nilipofika nilijitahidi kumtengenezea chakula cha kumpa nguvu maana ni mzee, maji au soda peke yake nikaona havitoshi. Nikaamua kutengeneza aina fulani ya biskuti ambazo baadaye alizipenda sana. Akawa anakula aina hiyo ya biskuti na Fanta. Basi akishakula hicho mpaka jioni atakaporudi.

“Kwa kifungua kinywa alikuwa anapendelea kahawa, na kitafunwa inategemea na nini tumetengeneza, labda tosti (mkate uliokaushwa) au chapati hasa chapati za maji; na pia kuna ndizi za kisukari tulikuwa tunatengeneza banana filter… nami niliona nimwekee vionjo vya namna hiyo.

Kuugua kwa Mwalimu

“Niliendelea kuishi Butiama hadi mwaka 2006 nikarudi Dar es Salaam. Mwalimu kama binadamu alikuwa anaugua, lakini hakuwa anaugua ile ya kitisho sana kama alivyougua kipindi cha mwisho. Alikuwa anaugua mafua na homa za kawaida tu.

Mwalimu alikuwa anafanya mazoezi asubuhi. Alikuwa na baiskeli ya mazoezi ndani kwake. Kwa hiyo alikuwa mkakamavu sana. Si kwamba alikuwa akigua mafua hawezi kwenda shamba, au haendi kanisani. Hapana. Alikuwa anaenda kanisani asubuhi na jioni, na huwezi kujua Mwalimu ana homa. Ukisikia amelala, labda ni hii iliyokuja mwishoni mwa maisha yake. Homa za kawaida zilikuwapo, lakini sikuwahi kuona Mwalimu akitetereka.

Alipoanza kuugua

“Alipoanza kuugua utata ulikuwapo. Kwanza kilikuwa kipindi cha mikutano ya usuluhishi ya Burundi. Mimi mmojawapo nilikuwa Arusha. Kidogo ndipo nilipoanza kumwona ana mabadiliko fulani. Lakini kama nilivyokwambia, alikuwa haoneshi moja kwa moja. Wageni walikuwa wanakuja anaongea nao vizuri tu. Sasa ilipofika hatua ya kumaliza ule mkutano kurudi nyumbani, mimi niliondoka kwenda likizo. Niliagana naye nikiwa Arusha kule kule kwamba nikifika Dar es Salaam nitakwenda likizo nyumbani (Nachingwea), kwa hiyo tukaagana kule.

“Nilipofika Nachingwea nikapata taarifa – yeye si amesharudi Butiama – kwamba hali ya Mwalimu si nzuri. Nilikatiza likizo. Nikarudi Butiama. Niliporudi nilimkuta yupo kitandani, serious kabisa ya kuumwa. Nilikwenda kumwona chumbani kwake, nikakuta amekaa nje ya chumba. Nilisikitika sana aliponionesha ni kitu gani kilichokuwa kinampa matatizo.

Nikaangalia. Nikajua kweli Mwalimu anaumwa. Sasa sikuelewa tatizo alilonalo ni nini maana ni mambo ya kidaktari…ule ugonjwa wa mkanda wa jeshi. Na matibabu alikuwa anapata.

 

Madaktari wa pale pale Butiama walikuwa wanakuja, tena daktari mmoja namkumbuka alikuwa ndiye daktari wale. Alikuwa anakuja kila mara kumwangalia.

Namkumbuka kwa jina moja daktari huyo ni Dokta Malima. Alishirikiana na wenzake. Kila wakati tulikuwa naye. Baadaye tukaambiwa kuwa Mwalimu atasafirishwa kwenda hospitali ya nje.

“Lakini wakati huo si ile hali ya yeye kubebwa. Hapana. Alitoka akiwa anatembea mwenyewe vizuri tu, tena siku hiyo anaondoka kulikuwa na vichekesho. Tukawa tunatafuta moja ya fimbo zake anayoitaka yeye. Kila iliyokuwa inapelekwa alikuwa anasema ‘siyo hii’. Walichelewa kutoka pale (msafara) kwenda Musoma kwa sababu ya fimbo. Ilipopatikana, Mwalimu aliondoka.

Dalili za kustaajabisha

“Kitu cha kwanza cha ajabu nilichokiona, Mwalimu siku ile kabla hajaingia kwenye gari alisimama akaangalia mandhari ya pale nyumbani kana kwamba alikuwa anaangalia mara ya mwisho. Ndugu yangu kama ungekuwapo siku ile ungesema huyu mtu alikuwa anajua kitakachotokea baadaye ni nini…kabisa kabisa kabisa. Yaani kabisa.

“Lakini baadaye akaondoka kuelekea Musoma. Sasa ya Musoma sijui, maana sisi tulibaki pale. Waliokwenda Dar es Salaam kwa ajili ya safari ya London walikuwa wengine.

“Tuliobaki pale Butiama hali haikuwa nzuri. Kwanza kabla hajaondoka, kulikuwa na simanzi kubwa kutokana na hali yake ilivyokuwa. Tulikuwa hatulali. Kwa kawaida tulikuwa tunatoka pale saa nne, saa tano usiku; lakini kipindi kile alichokuwa anaumwa mpaka saa saba, saa nane ndiyo tunakwenda kupumzika; na saa 11 tunarudi pale. Na pale nyumbani kukawa kuna watu wanabaki – walinzi na watumishi wengine. Kwa kweli ilikuwa kazi nzito sana, lakini tuliifanya kwa sababu tulimpenda mno Mwalimu.

Ishara za msiba

Baada ya kifo cha Mwalimu wengi tumetetereka. Si mimi tu peke yangu. Sisi watumishi – watu wa karibu tuliokuwa pale, kila mmoja nadhani anazungumza hicho kitu. Hali ni tete. Unajua baba anapoondoka sehemu, familia inakuwa inatetereka kwa mambo mengi sana. Kwa mfano kuna mahitaji mengi sana, kikubwa ni busara. Baba anapokwambia usifanye hivi na hivi, halafu baadaye tena ukamkosa mtu wa kukupa mawazo na busara ya namna hiyo kwa kweli hali yako inakuwa si nzuri. Lazima utetereke.

Ila kuna kitu ninachokumbuka. Kuna kitu kilitokea nadhani hata ninyi sijui kama mliambiwa. Palitokea popo mchana. Wapo popo, lakini walitokea mchana, kitu ambacho si kawaida. Mbayuwayu unawajua? Basi, wale popo ni kama kulikuwa na sherehe au mkusanyiko usio wa kawaida, yaani kama giza kabisa. Popo wengi sana walitanda, wengi sana.

Nilikuwa na dereva mmoja anaitwa Salum. Tunaitana mjomba, mjomba. Akasema mjomba hapa hapako shwari, hawa popo siwaelewi… Hawa popo wanaruka mchana jua kali si kitu cha kawaida. Sasa kwa imani yetu tukaona pale kuna ishara fulani si nzuri. Kesho yake ndiyo tukaanza kusikia hali ya Mwalimu si nzuri. Siku hiyo ikawa tarehe 14 Oktoba ndiyo tukaambiwa mzee amefariki dunia.

“Mapokeo ya kifo cha yule mzee hakuna aliyepokea kwa kawaida. Kama ni ukimya…sehemu nyingine walikuwa wanaangalia kwenye televisheni, tulikuwa tunasikia watu wanaanguka…kile kijiji kilikuwa kimya. Kile kijiji (Butiama) watu wanapenda starehe, lakini siku hiyo ya msiba kilikuwa kimya kabisa kabisa.”

Tumesahaulika

Nchia anasema pamoja na kumhudumia Mwalimu kwa upendo na unyenyekevu wa hali ya juu, siku ya mazishi watumishi hawakupewa nafasi rasmi ya kumuaga. “Waliitwa watu wengi wakapewa nafasi, sisi hata kupewa nafasi ya kuweka shada la maua kwenye kaburi hatukupewa… sisi tuliokuwa karibu kabisa na Mwalimu hatukupewa heshima hiyo. Pia Serikali imeshindwa kabisa kutukumbuka kwa lolote kama sehemu ya kutambua mchango wetu wa kumhudumia Baba wa Taifa, maisha yetu ni ya shida tu,” analalamika.

Nchia anasema mwaka 2006 alihamishwa kutoka Butiama na kupelekwa Dar es Salaam baada ya kupata matatizo ya kiafya. Anasema baada ya afya yake kutengamaa alipelekwa katika Ofisi ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambako anaendelea na kazi kama mhudumu wa ofisi.

“Kazi yangu ni upishi, hii ya uhudumu wa ofisi naifanya kwa sababu ya tabia ya kuheshimu kazi ambayo tulifundishwa na Mwalimu,” anasema Nchia.

Ni kutokana na uchapaji kazi, mwaka jana alichaguliwa kuwa Mtumishi Bora wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma. Huyo ndiye “Dokta Nchia” ambaye anasema ilikuwa bahati kubwa kwake kuwa mpishi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Evance Nchia kwa sasa anaishi na kufanya kazi Dar es Salaam. Anapatikana kupitia simu na.

0716241702