Kumekuwa na matukio ya mauaji ya watu mara kwa mara katika wilaya za Urambo na Kaliua mkoani Tabora, yanayofanywa na baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola, hali inayoendelea kutishia maisha ya watu, huku ikionesha kuwa hakuna hatua za kuridhisha zinazochukuliwa kukabili tatizo hilo.

Katika hali isiyokuwa  ya kawaida, mkazi  wa Usinge wilayani  Kaliua, Kipara Issa, ameuawa  baada  ya kupigwa  kwa  muda  mrefu  na watu  wanaodaiwa  kuwa  ni  maofisa  wanaoendesha  operesheni ya  kusaka silaha  haramu na kulinda misitu katika  maeneo  mbalimbali  ya  mkoa huo.

Tukio  hilo  lililotokea hivi karibuni, ambapo  maofisa  hao  wakiwa  katika  magari  ya  operesheni hiyo, waliokuwa  wamevalia  sare za  Jeshi  la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, maofisa Usalama na Maliasili wanadaiwa  kufika  nyumbani  kwa  mtu  huyo  kwa  nia ya  kutaka  kumfanyia  upekuzi  baada ya kumshuku  anamiliki  silaha  kinyume  cha  sheria.

 

Wakiwa  katika  upekuzi  huo, walikutana  mke  wa Kipara, Tabu Maganga,  ambaye  ni  askari  polisi  katika kituo  cha  Usinge na kuanza kumhoji kuhusu mumewe na shughuli anazozifanya, huku wakidaiwa kumpiga hadi akapoteza fahamu mara kadhaa.

Hali ilivyokuwa

Wakati mke wa Kipara, Maganga, ambaye ni askari polisi mwenye nambari WP 6985 akiendelea kupata suluba kutoka kwa maofisa  hao  waliokuwa  na  bunduki na  rungu, watoto wa  umri wa  kati  ya  miaka  13 na  17 waliokutwa nyumbani  hapo pamoja  na  bibi yao nao walishambuliwa.

Mama mzazi wa Kipara, Magreth Kajoro,  akielezea  mkasa  huo,  alisema  wakati  amekaa  nyumbani  kwa  mwanaye huyo  alishangazwa  kuwaona  maofisa  hao  walivyofika na  kuanzisha  tukio  hilo  la  kinyama,  na  kwamba alipojaribu  kuhoji walianza kumpiga.

“Walinikamata  na  kuniingiza  ndani  wakanilazimisha nioneshe silaha ambayo walidai inatumiwa na mtoto wangu, lakini baya zaidi mmoja  wao  ambaye  alikuwa  kavaa  mavazi  ya Jeshi  la  Wananchi  aliniwekea bunduki kichwani huku  wakiniambia  nisali sala yangu ya mwisho,” alieleza  Magreth.

Aliendelea kueleza;  “Baada  ya  muda  mfupi  nilisikia  kishindo kikubwa na baadaye kufuatiwa  na  kauli  ya  amri  ya kukatazwa  kufyatua risasi, ndipo  Kipara  akafika  hapo  nyumbani  akipigwa huku akiambiwa  aoneshe  bunduki anayofanyia uhalifu, jambo ambalo lilikuwa ni geni sana kwetu hapo nyumbani.”

Katika upekuzi huo, maofisa hao ambao imedaiwa kuwa walipata taarifa za uhalifu zilizowahusisha watu wanane wa maeneo ya Wilaya ya Kaliua akiwamo Kipara kwamba mbali ya kumiliki silaha haramu, ilidaiwa alikuwa anamiliki sare za JWTZ ambazo huzitumia kufanyia vitendo vya kihalifu na akizihifadhi ndani ya magunia ya mahindi na mpunga nyumbani kwake.

Askari hao wa operesheni maalum wakati wa kusaka silaha na sare za JWTZ kabla ya kumwadhibu Kipara hadi akafariki dunia, walimwaga unga wa mahindi na mpunga wakiamini kwamba watakuta silaha na sare hizo za jeshi hilo bila mafanikio.

Watoto  Said Auma (14), Anthony Gabriel na Said Kalungumya, walijikuta wakipata adhabu kali ya kubebeshwa milango ya nyumba ambayo ilikutwa ndani kwa ajili ya biashara huku  wakipigwa hadi kupata majeraha makubwa katika maeneo mbalimbali ya miili. Hata hivyo,  baada  ya  kutekeleza  unyama huo, askari  hao  wa  oparesheni hiyo waliamua  kuondoka na Kipara, lakini wakati huo alikuwa na hali mbaya kutokana na kuvuja damu nyingi iliyosababishwa na kipigo kikali.

“Nilimshuhudia kaka yangu wakati  wanamtoa ndani akiwa amelowa damu nyingi baada ya kukosa hiyo silaha waliyokuwa wakitafuta, wakampakiza kwenye gari wakaondoka naye,” alisema Maneno Issa.

Muda mfupi baadaye familia hiyo iliamua kwenda kituo cha Polisi Usinge kufungua kesi wakiwa na mke wa Kipara, Tabu, ambaye inadaiwa kuwa wakati akipata kipigo alidhalilishwa kwa kuvuliwa nguo akiamuriwa na maofisa hao wa operesheni kugaragara kwenye maji machafu.

DC Kaliua

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Saveli Maketa, alithibitisha kupata taarifa za tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa rasmi baada ya kufanyika kwa uchunguzi, huku akibainisha kuwa anachokijua kuhusu Kipara aliyeuawa ni kwamba alikuwa mhamiaji haramu na mtuhumiwa wa ujambazi anayehifadhiwa na mke wake huyo ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi, Usinge.

“Sasa unafikiri ndugu mwandishi hao maofisa wangeenda kufanya upekuzi hapo nyumbani kwa huyo jambazi bila kufanya kash-kash hata kidogo, lazima waende kijeshi kama walivyofanya kwa kuwa tuna taarifa rasmi kuwa anamiliki silaha,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

Hata hivyo, hakuzungumzia vitendo vya udhalilisha dhidi ya askari huyo wa kike na kuwapiga watoto na mama mzazi wa Kipara.

Maiti ya Kipara Issa

Baada ya saa  kadhaa  kupita huku familia ya marehemu Kipara Issa wakishirikiana  na  baadhi  ya  wanakijiji cha Usinge, walianza harakati za kumtafuta Kipara kwa  kupiga simu na kuuliza kwenye vituo vya Polisi tarafa na wilayani bila mafanikio.

Wakati mdogo wa Kipara, Maneno Issa,  akifuatilia huko wilayani Urambo, alipata taarifa kuwa kaka yake amepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Urambo tayari akiwa amekufa, jambo ambalo lilimlazimu afike haraka na kuhakiki maelezo aliyoyapata.

“Niliingia mpaka chumba cha kuhifadhia maiti nikamkuta kweli ni yeye, nikajaribu kumwangalia kwa haraka haraka, lakini kilichoniuma zaidi ni kuona kang’olewa meno na uso wake ulikuwa umevimba mno,” alisema Maneno.

Kamati ya Ulinzi na Usalama Tabora

Kufuatia tukio hilo ambalo lilikuwa likitafutiwa njia ya kufichwa, hatimaye taarifa zilizagaa hadi zikamfikia Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora, ambaye pia ni Mkuu wa mkoa huo, Fatma Mwassa, na kuamua kufunga safari akiwa na wajumbe wa kamati hiyo kwenda kujiridhisha katika tukio hilo la ukatili.

Ujumbe huo wa Kamati  ya  Ulinzi na Usalama ulifika na kutoa pole kwa wafiwa na baadaye kuzungumza na wakazi wa Usinge, ambao walitoa kilio chao kuhusu mauaji yaliyofanywa na maofisa hao sambamba na kumdhalilisha askari wa kike na kuwashambulia watoto sita wa familia hiyo.

Mkuu  huyo wa mkoa baada  ya  kusikiliza kwa makini malalamiko ya wakazi hao dhidi  ya unyama  waliofanyiwa,  kwa  niaba  ya  Serikali aliomba radhi tukio la mauaji hayo  huku  akieleza kuwa licha ya  kuwa operesheni hiyo ni halali, lakini nguvu iliyotumika si halali na hivyo  kuahidi kuwa Serikali italishughulikia kwa makini na wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo,  matukio  ya  mauaji yanayofanywa na  vyombo vya dola katika Wilaya za Urambo na Kaliua yamekuwa yakitishia amani kwa wananchi, hasa wakati wa operesheni hizo za maliasili, ambapo wananchi wamethibitisha kuwa askari wamekuwa wakitumia mwanya huo kuwadhulumu raia badala ya kutekeleza malengo ya operesheni hizo.

RPC Tabora

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Peter Ouma, alikiri kuwepo kwa tukio hilo la mauaji na kwamba anasubiri matokeo ya uchunguzi wa timu ya maofisa aliowatuma huko Usinge.

Hata hivyo, baada ya kiongozi huyo mwenye dhamana ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kufika eneo la tukio na kuupata ukweli alijibu kama ifuatavyo:

“Ni kweli nimefika na kuangalia kilichotokea na kwa sasa siwezi kusema chochote kwa kuwa najisikia kichwa kinaniuma.

 

”Mei 28, 2011 saa 10 jioni eneo la Usinge ya Kati, askari polisi waliwafyatulia risasi mfululizo wananchi baada ya kukamata ng’ombe 6,301 wao, na katika tukio hilo, Juma Said (21) alipoteza maisha kwa kupigwa risasi mgongoni na wengine wanne kujeruhiwa na hakuna hatua zilizochukuliwa kwa wahusika.

Matukio mengi ya mauaji yanayofanyika kimya kimya katika maeneo hayo yamekuwa yakijenga taswira mbaya na kuonesha kuwa Serikali haichukui hatua, hali ambayo inafanya watu wengi kudhani huenda inabariki uovu huo unaofanywa na taasisi zake.

1787 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!