Kuna kila hali inayoonesha kuwa kwa sasa vitendo vya ubaguzi wa rangi, vinazidi kushika kasi katika soka barani Ulaya, pamoja na kuwa kumekuwa na kampeni za hapa na pale za kupiga vita dhidi ya vitendo vya ubaguzi.

Mwamuzi aliyesimamia mechi ya Klabu Bingwa Barani Ulaya kati ya Manchester City dhidi ya CSKA Moscow wiki iliyopita, Ovidiu Hateganabout, amelalamikiwa hadi kufikia hatua ya kusemwa kuwa  hafai tena kuchezesha mechi yoyote, kwani alishindwa kuzuia matukio ya ubaguzi wa rangi uwanjani.

Hayo ni maoni ya Mwenyekiti wa Chama cha Kuzuia Ubaguzi wa Rangi katika Soka nchini Uingereza cha Kick It Out, Lord Ouseley. “Huyu mwamuzi hafai kuchezesha tena mechi, ameshindwa kutekeleza wajibu wake, hili ni suala la wazi ambalo UEFA inafaa kupambana nalo,” alilielezea Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Katika mechi hiyo ambayo Manchester City walishinda kwa mabao 2-1, mchezaji wa timu hiyo, Yaya Toure (pichani juu), anadai mashabiki walimtukana kwa kutumia matamshi ya ubaguzi wa rangi. Toure alionekana kumlalamikia refa Hateganabout kutokana na kelele za kibaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki wa CSKA katika mechi yao uliopigwa katika Uwanja wa Luzhniki. City walikuwa ugenini.

 

Kutokana na mwongozo uliotolewa na Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) mwaka 2009, waamuzi wana mamlaka ya kusitisha matamshi ya ubaguzi wa rangi uwanjani kutoka kwa mashabiki. Katika hatua za awali, mwamuzi anaruhusiwa kusitisha mchezo na kuamuru kutumika kwa vipaza sauti uwanjani katika kuwaonya mashabiki.

Hatua ya pili ya mwamuzi ni kuusimamisha mchezo kwa muda, na endapo vitendo vya ubaguzi wa rangi vitaendelea ana haki ya kusimamisha mechi isiendelee.

Kati ya hatua ambazo zimetekelezwa na UEFE dhidi ya klabu zilizohusika katika matukio ya ubaguzi wa rangi ni pamoja na kuwafungia mashabiki viwanja vya Dinamo Zagreb ya Croatia, Legia Warsaw ya Poland na Honved ya Hungary. Uwanja wa Lazio pia ulikuwa umefungwa, lakini baada ya kukata rufaa mashabiki waliruhusiwa tena kuingia uwanjani.

Viwanja ambavyo bado havijafunguliwa kikamilifu kwa mashabiki ni vile vya Poland, Lech Poznan na Piast Gliwice, na vile vya Apoel Nicosia ya Cyprus na HNK Rijeka ya Croatia.

Kwa kuwa Toure aliripoti matukio hayo kwa mwamuzi wakati wa mechi, na pia kuzungumza naye baadaye, tukio hilo litaandikishwa katika ripoti rasmi ya mechi na kufikishwa katika uongozi wa UEFA.

Manchester City, kama klabu pia imewasilisha malalamiko yake. Hata hivyo, uongozi wa Klabu ya CSKA Moscow umediriki kusema kuwa Toure peke yake ndiye aliyezisikia kelele hizo za ubaguzi wa rangi.

1186 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!