Kwa miaka mingi, eneo la Loliondo katika Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, limekuwa kama ‘jamhuri’ ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Eneo hili lenye utajiri mkubwa wa wanyamapori, limekuwa likiongozwa na asasi zisizo za serikali (NGOs) zenye nguvu za ushawishi zinazotokana na mabilioni ya shilingi kutoka kwa wafadhili mbalimbali wa ndani, na hasa nje ya nchi. 

Kabla ya kuendelea, ni vema kwanza kuifahamu Loliondo na Ngorongoro kwa ufupi.

Wilaya ya Ngorongoro ni moja ya wilaya saba za Mkoa wa Arusha. Wilaya hii ina ukubwa wa kilometa za mraba 14,036. Asilimia 59.1 ya eneo lote ni la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), asilimia 30 ni eneo la Pori Tengefu la Loliondo na Ziwa Natron na eneo lililobaki, yaani asilimia 10 ni eneo la hifadhi ya misitu. 

Kiutawala, Wilaya ya Ngorongoro imegawanyika katika Tarafa 3 za Ngorongoro, Sale na Loliondo. Wilaya hii ina kata 28 na vijiji 72. Shughuli kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro ni ufagaji (80%) na inayobaki ni kilimo na biashara. 

 

Loliondo

Pori Tengefu la Loliondo lina ukubwa wa kilometa 4,000 za mraba. Pori hili ni kitalu cha uwindaji kinachoendeshwa na Kampuni ya Ortello Cooperation Business (OBC). Katika Pori Tengefu la Loliondo shughuli mbalimbali za kiuchumi zinaendeshwa ndani ya eneo hilo. Shughuli hizo ni pamoja na ufugaji, utalii wa picha, makazi ya watu na kilimo. 

Uhifadhi katika Pori Tengefu la Loliondo upo njia-panda kutokana mfumko mkubwa wa shughuli zisizo rafiki na uhifadhi, yaani ongezeko kubwa la shughuli za kibinadamu. 

 

Umuhimu wa Loliondo kwa Ikologia ya Serengeti

Pori Tengefu la Loliondo ni kiungo kikubwa katika uhifadhi wa ikolojia ya Serengeti. Ikolojia ya Serengeti inajumuisha maeneo ya hifadhi mbalimbali ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba la Maswa, Ikorongo, Gurumeti, na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA).

Pori Tengefu la Loliondo ikiwa ni moja ya hifadhi katika Ikolojia ya Serengeti, limekuwa sehemu nyeti mno katika uhifadhi wa Ikolojia ya Serengeti-Maasai Mara. 

Umuhimu huo ni pamoja na:-

• Eneo hilo ni mazalia ya wanyamapori kama vile nyumbu, pundamilia na wengineo kipindi cha masika.

• Mapitio ya wanyamapori (ushoroba) kutoka Ngorongoro (NCAA) na Ziwa Natron kwenda Serengeti na Maasai-Mara na kurudi.

• Vyanzo vya maji kwa Hifadhi ya Serengeti, mfano Mto Pololeti na Gurumeti hadi Ziwa Victoria. Asilimia 47 ya maji yote ndani ya Serengeti yanatoka Loliondo.

• Pori Tengefu la Loliondo limekuwa ushoroba kwa wanyamapori kwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Ni dhahiri kuwa bila Pori Tengefu la Loliondo Hifadhi ya Serengeti inakufa.

 

Ziara ya Waziri Mkuu

Desemba 15, mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifika wilayani Ngorongoro kuendelea na ziara aliyoahirisha siku kadhaa kabla ya maadhimisho ya Uhuru. Alitua moja kwa moja Loliondo na kufungua ukurasa mpya kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kuutatua mgogoro wa robo karne katika Loliondo.

Hii ilikuwa siku ngumu kwa NGOs zipatazo 30 zilizoandikishwa kufanya kazi katika eneo hili, lakini 19 kati ya hizo ndizo zikiwa imara zaidi.

Waziri Mkuu aliitisha mkutano wa pamoja katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Wasso na kuhudhuriwa na watumishi na watendaji wa vyombo vyote vya Serikali, wawekezaji, viongozi wa NGOs na wadau mbalimbali.

Katika mkutano huo, Waziri Mkuu hakutaka kumung’unya maneno, badala yake aliamua kupasua ukweli wa mambo kuhusu ushiriki wa NGOs kwenye mgogoro wa Loliondo.

“Wilaya yenu ni nyeti, ina shughuli nyingi za kitalii, sehemu kubwa ya ardhi inamezwa na utalii. Taifa linategemea utalii kupata fedha-mapato makubwa yanayotokana na utalii. Hakuna aliye na kitu asitake kukiendeleza. Sheria za kutunza na kuhifadhi mazingira zipo. Maeneo hayatoshi ndiyo maana tunakuwa wakali kwa wageni wanaokuja kulisha mifugo na huku.

“Maeneo ya utalii lazima yasimamiwe na sheria za uhifadhi. Hapa kuna Pori Tengefu, maeneo haya yana sheria zinazoyalinda. Tufanye marekebisho kadhaa ikibidi, lakini wajibu wetu ni kulinda shughuli zinazotuletea tija ili tutoe huduma. Tusiingize chuki, tusiingize migogoro, watu hawaishi kwa migogoro. 

“Migogoro hapa ipo ama wawekezaji, au utalii, au uwekezaji au sheria za uhifadhi. Kuna vijiji tulivyosajili, kama tulifanya makosa, tuliyafanya.

“Ndiyo maana nimetaka Kamati iliyoundwa chini ya RC (Mkuu wa Mkoa wa Arusha), ifanye kazi na baadaye nitawatuma mawaziri watatu – (Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) – ili tufanye mabadiliko. Hatuhitaji tena migogoro,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

 

Salamu kwa NGOs

Akiwa ameshika nyaraka mbalimbali zenye kuonesha anatambua vema vyanzo vya migogoro Loliondo na wahusika wake wakuu, Waziri Mkuu hakusita kuanika ukweli.

“NGOs zinachochea migogoro hapa, kuna nyingine hazijasajiliwa, wengine hawafanyi kazi zao…Nimeshituka wilaya moja (Ngorongoro) ina NGOs nyingi kweli. Kuna nini Loliondo? Kuna NGOs zaidi ya 30 lakini zilizo active ni 15. Zipo zinazotuhumiwa kuchochea vurugu. Hiyo msahau katika nchi hii – kujiingiza nje ya utaratibu, kama utamaduni huo upo, uishe. Tutawafutilia mbali. Kama tumeweza kusajili, tutakufuta pale usipofanya yale yaliyofanya usajiliwe.

“NGOs ni wadau muhimu kama wanafanya kazi vizuri. Tunathamini mchango mzuri, lakini nje ya hapo hatuwezi kuvumilia. Hizi NGOs idadi yake ni kubwa, hili ni swali la kujiuliza,” alisema.

Waziri Mkuu akasema fedha zinazokusanywa na NGOs hizo kutoka kwa wafadhili wake ni nyingi mno, lakini hakuna thamani ya hizo fedha.

“Tuna taarifa za benki, kazi mnazofanya hazilingani na fedha. ACCORD Tanzania mpo? PWC? UCRT? PINGOs, Oxfam, NGONET, Makao, Engudeo, KIDUPO, Frankfurt…

“Kuwa na NGOs siyo tatizo, tatizo ni function ya hiyo NGOs,” alisema.

Waziri Mkuu akasema anazo taarifa za NGOs ambazo baadhi zinaundwa na wanafamilia, na kusema hilo si kosa hata kama NGO husika inaundwa na watoto na wazazi, lakini tatizo ni pale zinapoacha kutekeleza yaliyo kwenye usajili wake na kuamua kujihusisha na uchochezi.

“Nikikugundua unafanya uchochezi nakufutilia mbali. Kauli hii isikukwaze kama huhusiki na mambo nje ya malengo ya kusajiliwa kwako. Kama ni siasa sajili chama cha siasa. Wote hapa mmesajiliwa kwa ajili ya kuleta maendeleo,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa akiwanyanyua baadhi ya wamiliki wa NGOs hizo na kuwauliza bajeti zao. Wengi walitoa majibu ya kujikanganya, jambo lililozua vicheko ukumbini.

“Tunajua mnayofanya, wengine mna akaunti Kenya. Mna- operate Tanzania, lakini akaunti ziko Kenya. Serikali hii haitaruhusu…lazima mwende na filosofia mpya ya Serikali, hatutaki ubabaishaji,” alisema.

Kana kwamba haitoshi, Waziri Mkuu alitaja baadhi ya fedha zinazokusanywa na NGOs hizo kila mwaka, lakini thamani ya fedha hizo imekuwa haionekani.

Alitoa mfano wa PWC ambao kwa mwaka wanapata Sh bilioni 2.5 huku wakidanganya kuwa wamejenga shule lakini ukweli ukiwa kwamba shule hiyo ni ya binafsi inayoendeshwa kibiashara.

“Serikali iko makini, hakuna ubabaishaji, tutafuta zote za ubabaishaji,” akasisitiza.

Akasema kuna NGOs nyingine zinafanya kazi kwenye ‘briefcase’, na akaagiza lazima ziandikishwe BRELA na zilipe kodi zinazostahili.

“Kama PWC anapewa Sh bilioni 2.5 kwa mwaka na shirika la UCRT linapokea Sh bilioni 1.5 kwa mwaka, lakini hajui yanafanya nini.

“Nina taarifa zenu mnapata hela nyingi, lakini mnahudumia vipi jamii! hakuna, sasa ngojeni ukaguzi ufanyike halafu nitachukua maamuzi (uamuzi) maana kila siku Loliondo, kuna nini hapa? Mnasajiliwa halafu hakuna cha maana.

“Najua mnachokifanya, sasa nawaambia Serikali haitawafumbia macho kuona hiki mnachokifanya hapa na ikigundulika mnafanya kinyume na matakwa ya usajili tutazifuta,” alisisitiza.

Kutokana na kutoeleweka vema kwa matumizi ya fedha katika NGOs hizo, Waziri Mkuu akamwagiza Mkaguzi Mkuu wa Serikali afike Ngorongoro haraka iwezekanavyo kufanya ukaguzi katika asasi hizo.

“Kwanini nisilete Mkaguzi Mkuu wa Serikali kama kweli tuko serious kuleta maendeleo, na Baraza la Madiwani likapata nafuu, wananchi wakajisikia kupata msaada. Kama haturidhiki, kwanini tusiondoe? Hapa hakuna mchezo. Siyo Serikali hii…” alisema.

Kusikia hivyo, Mkurugenzi wa PWC, Maanda Ngoitiko, alisimama na kutaka kuzungumza, lakini Waziri Mkuu akamjibu: “Sikuja kufanya kesi, natoa maelekezo ya Serikali.

“Taasisi zinazolalamikiwa sana, kwa NGOs zote, nawapa muda wa matazamio kuanzia Januari hadi Juni 2017.

“CAG anakuja kukagua fedha na matumizi na miradi kama zina tija. Atanieleza zipi ziendelee, zipi zisiendelee, nasikia nyingine wajumbe wa bodi ni wanafamilia, sina tatizo, mimi nataka matokeo ya hizo NGOs. Serikali itafanya kazi na wadau. Tulisajili, kama mlikuwa holela, sasa mambo yawe kwenye mpangilio. Nawapa miezi sita ya matazamio – kujua fedha mnazoingiza na kazi mnazofanya kwenye jamii. Lazima mbadilike, na wale wote mnaofanya mambo nje ya utaratibu mnapaswa kuacha mara moja, mkipuuza tutashughulika na ninyi. Fuateni kanuni na sheria. Nidhamu tumeanza ndani ya Serikali na tunataka ifike hadi nje mliko. Hili zoezi ni endelevu, lazima mjue msimamo wetu (Serikali ya Awamu ya Tano), atakuja CAG, tutakwenda saiti kukagua kazi zenu zote. Wenye akaunti nje ya nchi rudisheni nchini. Mnafungua NMB kwa geresha, rudisheni, fanyeni kazi mlizosajili. Serikali hii haina mzaha, wote wa mambo ya ovyo tutawafutilia mbali.

“Watumishi wa Serikali wanaoshirikiana na NGOs tutawashughulikia. Kuna picha zinapigwa za kandambili chafu na kuwekwa kwenye mitandao wanasema ndiyo hali ya Loliondo. Ndiyo kazi mnazofanya? Nitafuta. Mnaandika kwenye mitandao, tutawafuta. Migogoro ya ndani lazima iishie ndani badala ya kuipeleka nje.

“Wapo wanaoshirikiana na raia wa kigeni kuichafua nchi yetu, taarifa zenu zote tunazo, e-mail zenu zote tunazo. Mswedeni alipigwa PI halafu mnamleta nchini kinyemela. Taarifa zote tunazo, na ikibidi tutamfuata huko huko aliko. Ninyi Watanzania ndiyo mnaoshiriki kuichafua nchi. Nidhamu zenu tutazifuatilia ndani na nje ya nchi, ukifanya mambo kwa kunyoosha tutakusifia. Ukichanganya mambo ovyo tupo pamoja na wewe. Kazi yetu sote ni kuwatumikia Watanzania na kuilinda nchi yetu.

“Halafu hizi NGOs kwanini wengine msiende Mbeya? Msiende Uvinza? Msiende Ruangwa? Sasa mmejaa hapa tu, tutajua yale yanayoendelea ili kujenga discipline ndani na nje ya Serikali,” alisema Waziri Mkuu.

Baadaye kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Wasso, Waziri Mkuu alirejea msimamo wa Serikali wa kuzifuatilia NGos ili kukomesha vurugu na migogoro Loliondo.

Alisema inastaajabisha kuona NGOs ikipokea Sh bilioni 1.4 na kutumia Sh milioni 120 pekee kununua mbuzi 400 huku fedha nyingine zikiishia kwa viongozi wa asasi hizo.

“Serikali makini ya Dk. Magufuli haina ubabaishaji. Hakuna ruhusa kwa NGO kufanya chochote eti tu wewe ni NGO, hakuna. Atakayehamasisha wananchi kuvuruga miradi ya maendeleo tutamkamata,” alionya.

 

Wenye NGOs wakacha

Baada ya Waziri Mkuu kuzisema NGOs na kutoa msimamo wa Serikali, viongozi wa NGOs hizo na washirika wao hawakuhudhuria mkutano wa hadhara katika viwanja vya Wasso.

Badala yake walikutana kwa faragha kabla ya kuondoka Wasso mapema asubuhi siku iliyofuata kurejea maeneo yao; na hivyo kutoendelea na ziara ya Waziri Mkuu katika maeneo mengine.

 

Ukweli kuhusu NGOs

Baadhi zinaongozwa na watu ambao, ama si Watanzania, au wengine waliopata uraia wa kuomba.

Miongoni mwao ni Maanda Ngoitiko wa PWC ambaye awali alikuwa CCM kabla ya kuhamia Chadema. Wengine pamoja na Ngoitiko, wanaotajwa kuwa Wakenya ni Samwel Naingiria, Sinandei Mako (UCRT), Tina Timan (mke wa mbunge wa zamani wa Ngorongoro) na Rafael Long’oi.

NGOs kama ya NGONET wamekuwa wakifanya kazi zao kwa miaka mingi bila kuwa na usajili wakiwa na Mkurugenzi wao, Samwel Naingiria. Huyu ni mmoja wa washirika wakuu wa raia wa Sweden, Susanna Nordlund, aliyepigwa PI hapa nchini kutokana na uchochezi wa migogoro Loliondo. Pamoja na kuzuiwa, baadhi ya washirika wake wamekuwa wakimwezesha kupenya na kuingia katika vijiji kadhaa vya Loliondo.

Oxfam imekuwa miongoni mwa NGOs zinazotuhumiwa kuendesha vitendo vya uchochezi. Mbunge wa sasa wa Ngorongoro ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Tate ole Nasha, ni miongoni mwa waliokuwa waajiriwa katika asasi hiyo.

Akiwa mtumishi wake, alihakikisha Oxfam wanapeleka fedha nyingi  kwenye asasi ya PINGOs Forum ambako pamoja na mambo mengine, zilitumika kumsaidia Nasha kushinda ubunge.

Asasi ya Dorobo Safaris,  wamekuwa wakijiendesha kwa mabilioni ya shilingi inazopata kupitia NGOs ya PWC na UCRT. Japo Maanda na mumewe, Mako, wanaonekana kufaidika na fedha nyingi za ufadhili, ukweli ni kuwa sehemu kubwa ya fedha zinazotolewa na wafadhili ughaibuni zinaingia Dorobo Safaris.

 

>>INAENDELEA

2533 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!