DRC kupata huduma za afya Tanzania

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imetenga zaidi ya Sh milioni 550 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali na kituo cha afya ili kuwasogezea wananchi huduma na kuokoa vifo vya mama na mtoto.

Ujenzi huo unahusisha Hospitali ya Ikola iliyopo Karema itakayowahudumia pia wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tanganyika, Rojas John, anasema ujenzi wa Hospitali ya Ikola na Kituo cha Afya cha Kasekese umekwisha kuanza na fedha zitakazotumika ni mapato ya ndani.

Hospitali ya Ikola iliyopo mwambao wa Ziwa Tanganyika mpakani na Kongo itagharimi Sh milioni 400 huku kiasi kilichobaki, Sh milioni 150, kikitumika kujenga Kituo cha Afya cha Kasekese.

“Itakuwa ni hospitali kubwa na tunatarajia kuwasaidia hata ndugu zetu wa upande wa pili (DRC),” anasema John.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Hamad Mapengo, anasema kwa sasa huduma ya afya inapatikana katika Kituo cha Afya cha Karema.

“Kwa miaka mingi wananchi wenye mahitaji ya huduma kubwa zaidi za afya husafiri umbali wa kilometa zaidi ya 100 kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi iliyopo Mpanda mjini. Kutokana na umbali huu wapo baadhi ya wagonjwa wamepoteza maisha,” anasema Mapengo.

Mmoja wa wakazi wa maeneo hayo, Mwajuma Hamis, anasema kukamilika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasekese kutaondoa adha kwa wajawazito wengi waliolazimika kufuata huduma bora Mpanda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Taanganyika, Rojas John, akikagua ubora wa matofali yanayotumika kwa ujenzi wa Hospitali ya Ikola iliyopo mwambao wa Ziwa Tanganyika.