ViongoziWaafrika tulipokuwa tunaimba na kucheza ngoma, kusherehekea uhuru na matunda yake, vizazi vya waliokuwa wakoloni vilikuwa vinakuna vichwa kutafuta jinsi na namna ya kufuta hiyo furaha kutoka kwenye nyuso zetu milele.
  Uchambuzi wa kina waliufanya kujua kilichosabisha wakoloni washindwe vita dhidi ya wapigania uhuru wa nchi za Afrika na sehemu nyingine vita ambazo, kifedha na kisilaha, hawakustahili kushindwa.
  Jawabu walilopata lilikuwa ni woga wa kifo; wakoloni walikuwa tayari kuua, lakini hawakuwa tayari kufa.


Juhudi zao zote basi zilielekezwa kwenye kutafuta uvumbuzi wa tatizo hilo; na baada ya nusu karne tu wamefanikiwa kutengeneza silaha itakayowawezesha kuua watu bila wao wenyewe kuwa katika hatari yoyote ya kuuawa.
Silaha hii inaitwa “drone” au “unmanned aerial combat vehicle – UACV” – ndege ya kivita ambayo haichukui rubani.


  Wapo wachambuzi wa siasa wanaosema kuwa nchi kama Uingereza, Ufaransa, Uholanzi na nyinginezo zilizokuwa na makoloni zililazimika kutoa uhuru kwa makoloni yao kwa sababu baada ya Vita Kuu ya Pili nchi hizo zilikuwa katika hali mbaya mno ya kiuchumi.
Laiti utajiri pekee ungeliweza kuhakikisha ushindi katika vita, basi Marekani iliyoibuka kutoka kwenye vita hiyo tajiri kuliko nchi nyingine yoyote duniani isingelishindwa Vietnam.


  Hizi “drones” au UACVs ni ndege ambazo tayari zimeanza kuua watu Somalia, Libya, Yemen, Iraq, Afghanistan, Pakistan na sehemu nyingine wakati watu wanaoziendesha au maopereta wake wapo kilometa karibu 10,000 kutoka sehemu za mauaji – kwenye chumba chenye “air-condition” labda na kikombe cha chai au kinywaji baridi mkononi.
  Hizi ni ndege zinazogeuza (concept) ya vita badala ya mapambano kuwa ni mauaji (massacre); ni ndege zitakazozika jadi ya kupigania uhuru na uwezekano wa kuua kabisa uhuru wenyewe katika bara la Afrika upo tena ni mkubwa.
  Fauka ya hili, roboti zitakazotumika nchi kavu na baharini aidha tayari zipo au katika hatua ya juu kabisa ya kuwapo.


  Nchi karibu 50 hivi sasa zinajishughulisha kwa dhati na teknolojia hii ya mauaji ya “remote control”; na katika hizi, haipo nchi ya Kiafrika hata moja.
  Hivyo basi, kabla viongozi wa Afrika hawajamaliza kukabidhi bara zima kwa wakoloni wanaokwenda kwa jina la “Wawekezaji katika ardhi”, itakuwa ni bora kama watafanya tafakari na tathmini ya kina juu ya matokeo au “implications” ya hizi silaha katika siku za usoni.
  Na tena hasa ikizingatiwa kuwa kwenye karne ya 19, wakati wakoloni wanajigawia bara la Afrika kwa kiburi na jeuri, kujiamini kwao kulitokana na uhakika wa kwamba, “What-ever happens, we have got the maxim gun, and they have not”.


  Wazungu walikuwa na maana kwamba “Vyovyote itakavyokuwa, tuna mzinga wa maxim, na wao hawana.” Hii ndiyo iliyosababisha wageni kuvamia bara letu bila woga, yaani sisi Waafrika tulikuwa na mikuki na mishale, wao walikuwa na mabunduki na mizinga.
Ilichukua miaka mingi na uhai wa mamilioni ya Waafrika kujinasua kwenye ukoloni huo. Na ushindi ulitokana na ujasiri na misimamo imara ya watangulizi wetu waliokuwa tayari kuiaga leo yao kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kutakuwa na kesho ambayo ni azizi kwa vizazi vyao vijavyo.


Wakati wakoloni, walikuwa tayari kuua ili waendelee kutawala Afrika, lakini hawakuwa tayari kufa. Walichotaka ni kubaki hai wafaidi matunda ya kutawala bara letu; na hicho ndicho kilichowafanya wakoloni washindwe kwenye vita dhidi ya wapigania uhuru, licha ya utajiri mkubwa na vifaa bora vya vita walivyokuwa navyo.
  Kwa kuweka mikuki na mishale pembeni na kuanza kutumia bunduki za kawaida kama AK 47 Waafrika waliotawaliwa na Wareno, mathalani, walipata katika muda wa miaka 10 uhuru waliokuwa wanaulilia kwa muda wa miaka 500.


  Kama, wakoloni wangelikuwa na uwezo wakati huo wa kuua tu wapigania uhuru bila wenyewe kuwa na hofu ya kuuawa basi bara la Afrika lisingekombolewa kamwe; kwani wakoloni hao wasingelisita hata kidogo kuua kila mtu.
 
Je, wakoloni walipata kujaribu kufuta wazawa katika nchi?
Nasikitika kusema kuwa jibu la swali la hapo juu ni ndiyo, tena si mara moja. Kwa mfano, nchi inayoitwa Democratic Republic of Congo (DRC) ilipokuwa ni mali ya Mfalme Leopold wa pili wa Ubelgiji na kuitwa Congo Free State (ingawa haikuwa huru), kati ya mwaka 1885 na 1908, Wakongo zaidi ya milioni kumi waliuawa (nusu ya raia wote); aidha kwa kufanyishwa kazi ya kuvuna raba maporini (wild rubber) mpaka wanakufa au kwa kuwindwa kama wanyama (for sport).


  Kwenye idadi hiyo iongezwe watu ambao maisha yao yaliharibiwa kwa kukatwa mkono au kiungo kingine kwa tuhuma za uvuvi, na watoto waliokatwa mkono wazazi wao walipochelewesha kuwasilisha mavuno ya hiyo raba.
  Na unyama huu wote uliwezeshwa na uhakika wa kwamba Wakongo hawakuwa na jinsi ya kuwaonjesha wakoloni hao ladha ya kifo.
Huko Namibia, wakoloni wa Kijerumani waliua asilimia 80 ya wananchi wa kabila la Waherero na asilimia 50 ya wananchi wa kabila la Wanama.


Nchini Kenya, baada ya serikali ya kikoloni kutangaza hali ya hatari na kuanza kuua watu bila simile, wakati wa vita ya Mau Mau, kati ya Oktoba 1952 hadi 1960, idadi ya Wakenya waliouawa inategemea unafuata takwimu gani:
  Rekodi za kikoloni zinasema 12,000 waliuliwa; wakati Profesa David Anderson wa Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza anasema ni zaidi ya 20,000; Profesa Caroline Elkins kutoka Chuo Kikuu cha Havard, Marekani, aliyefanya utafiti mpana na wa kina zaidi anasema ni zaidi ya wananchi 50,000 waliuawa; na yeye anazidi kuongeza kuwa kuna watu zaidi ya 100,000 waliokufa kwenye makambi (concentration camps) na vijiji ambavyo vilizungushiwa sinyenge vilivyoitwa hifadhi “reserves”.


  Wakikuyu waliokadiriwa kuwa milioni 1.5 nyakati hizo karibu wote waliwekwa kwenye hizi hifadhi na makambi; na vifo sehemu hizi vilisababishwa na msongamano, vipigo, mateso (torture), njaa na magonjwa.
  Katika kitambo hicho hicho (1952-1960) Wazungu walowezi (settlers) waliouawa walikuwa ni 32 tu; na askari Wazungu waliokufa vitani hawakuzidi 69. Kwa maneno mengine ilichukua jumla ya vifo vya Wazungu 101 katika muda wa miaka 8 kuwafanya Waingereza walazimike kutoa uhuru wa bendera kwa Kenya mwaka 1963; baada ya ukoloni wa miaka zaidi ya 70.


  Wazungu waliohamia Marekani kutoka Ulaya pia walifanya mauaji yalioyoashiria jaribio la kutaka kuangamiza (annihilate) Wahindi wazawa wa nchi hiyo.
  Kwa mujibu wa Profesa Ward Churchill wa Chuo Kikuu cha Colorado: “… Idadi ya Wahindi wazawa (natives) wa Marekani iliyokadiriwa kuwa ni milioni 12 mwaka 1500 ilishuka hadi karibu watu 237,000 ilipofikia mwaka 1900.”

  Hilo kama si jaribio la kufuta taifa zima la watu hawa ni kitu gani?
Gazeti la The Sydeny Monitor, liliwahi kuchapisha makala iliyoelezea jinsi Wazungu waliohamishiwa Australia walivyodhamiria kuua taifa zima la watu weusi nchini humo, ambao ni Waaustralia wa asili (siku hizi wanaitwa Waaustralia wa kwanza) – Aboriginals – mnamo mwaka 1838. Lakini naona juhudi zao hazikufanikiwa, kwa sababu mwaka 1984, raia “mlowezi” Lang Hancock, alikuwa anahojiwa kwenye televisheni wazo la kuwaweka pamoja aliowaita “Waaboriginal wabaya” halafu kutia madawa kwenye maji yao yatakayozuia wao kuzaana, kwa lengo la kuwamaliza.
  Sasa wazo kama hili likitolewa na mlevi linakera, lakini linapotoka kinywani mwa tajiri wa kupindukia kama Hancock na ambaye anaondokea kuwa ni rafiki wa karibu wa aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, basi hili huwa ni tishio halisi si masihara.
Hivyo basi, ninaposema aidha wakoloni wasingelisita kuua kila mtu, au hawakuwa tayari kupoteza maisha yao kulinda makoloni, wala sitii chumvi.


Baada ya vizazi vya wakoloni kukamilisha hiyo silaha (inayohakikisha vifo vya maadui wao bila maisha yao wenyewe kuwa hatarini), hatua inayofuata ni kubuni mbinu za kurudi kwenye hizi nchi ambazo walifukuzwa karibu miaka hamsini iliyopita bila wananchi wa nchi hizo kuwashitukia.
Matokeo ndiyo huu ulaghai wa uwekezaji wa waja katika ardhi unaoikumbuka Afrika leo. La ajabu ni kuwa wanatumia mbinu zile zile ambazo mababu zao walitumia zaidi ya miaka mia moja iliyopita.


Lakini jambo la kushangaza zaidi ni kwamba waheshimiwa wanaongoza Afrika leo, ambao ni wasomi na wanajua yaliyojiri zama za nyuma wameingia kwenye mtego ambao mababu zetu waliingizwa bila kujua kwa sababu walikuwa wajinga wa kusoma (ignorant).
Wakoloni walipoingia Afrika na sehemu nyingine walitumia “Chartered Companies” ndiyo zilizokuwa “pioneers” za ukoloni; hivi sasa wamebadili jina, badala ya “Chartered Companies” wanaita “Multinational Corporations”; juzi walidai wanakuja kueneza ustaarabu (civilization) sasa wanasema wanaleta “globalization”; jamani, pamoja na usomi na uzoefu wao wote, viongozi wanashindwa kugundua kuwa hizi ni njama zilezile na zenye malengo pacha? Tuwasome vipi waheshimiwa hawa; wakiitwa akina “Judas Iscariot”, akina “Marcus Brutus” – wasaliti – watakuwa wanawasingiziwa?
  Hawa wakoloni mamboleo wanafahamu kuwa wakishakamata ardhi kwa kisingizio kinachokubalika na kutambulika kitaifa na kimataifa kama vile “uwekekezaji wa nje”, basi kesho na keshokutwa wenye nchi wakizinduka na kuanza kupigania ardhi yao; wao watakimbilia kwenye Kamati ya Usalama (Security Council) ya Umoja wa Mataifa (UN), kuomba kibali cha ulimwengu kuwaporomoshea mabomu kutoka kwenye hizo “drones”, watu ambao watakuwa tayari wamepachikwa nembo ya magaidi (terrorists).


Na madhali UN inadhibitiwa na wao wenyewe, basi maombi yao hayatakataliwa. Lakini la msingi hapa ni kwamba matatizo haya yote yatakuwa yanatokana na hizi sera za kilimo zinazonyang’anya raia ardhi yao na kuwapa wageni milele.
  Kwa mila na desturi, ardhi ni mali ya Taifa na Taifa ni wananchi si Serikali; hivyo kudai kuwa ardhi ambayo wageni wanapewa ni ya Serikali si ya wananchi ni utapeli, na ujambazi wa kisiasa (political banditry).
  Wakati watakuwa wanaporomosha hayo mabomu wanayoyaita moto wa jahanamu (hellfire) kutoka kwenye ma-drone, kweli ya rushwa ya kuwanunua watawala wa Afrika wakubali kuuza ardhi bila idhini ya watu wao, haitakuja kuongelewa kabisa.
Itadaiwa kwamba kwa sababu hizo sera za uwekezaji kwenye ardhi zitakuwa zimepitishwa na mabunge yao, hivyo wananchi wamezikubali, dai ambalo halina usahihi wowote.


  Kwani ubaguzi wa kikaburu wa Afrika Kusini ulioitwa “apartheid” ulipitishwa na Bunge, bado haukuwa halali kwenye macho ya ulimwengu na wananchi waliokuwa wengi nchini.
Ni kweli kwamba Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuchukua ardhi ya wananchi na kuanzisha mashamba ya umma kama NAFCO, ambayo faida iliyotokana na mashamba hayo ilinufaisha wananchi wenyewe.
Hii ni tofauti na NAFCO hiyo kumkabidhi mkoloni anayejiita “mwekezaji” alime kulisha Waarabu au Wazungu wanaoishi nje ya nchi au kuuza nje (export) kwa faida yake.

>>ITAENDELEA
Harid Mkali ni mwandishi wa habari, mchambuzi anayetumia nafasi hizo kuandika vitabu. Ni msomaji wa Gazeti la JAMHURI kupitia tovuti ya www.jamhurimedia.co.tz. Anaishi jijini London, Uingereza. Anapatikana kupitia simu: +447979881555; barua pepe: [email protected] na tovuti yake: haridmkali.com

By Jamhuri