SEMMY KIONDO SAME MASHARIKIKushindwa kufikia malengo, kukwama kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wa Jimbo la Same Mashariki, ni baadhi tu ya sababu zinazoamsha ari na kuchochea mori wana-CCM wanaojipanga kumng’oa Mbunge, Anne Kilango.
  Mama Kilango alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2005 baada ya kumng’oa ‘kigogo’ aliyewahi kuwa Waziri wa Fedha, Daniel Yona, aliyeingia Mwaka 1995 hadi 2005. Mwaka 2010 alitetea ubunge wake.


Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuteuliwa kwake hivi karibuni kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kumeongeza kasi ya kuachia jimbo  kutokana na kutotembelea mara kwa mara baada ya kutingwa na majukumu ya kitaifa.
Tofauti na alivyokuwa mbunge, alitembelea jimbo kila hali ya hewa ilipochafuka na kuweka mambo sawa, ambapo sasa analazimika kumsaidia Rais Jakaya Kikwete katika sekta ya elimu kwa nchi nzima.


Pamoja na dhana ya mbunge anapoteuliwa kuwa Waziri au Naibu Waziri humuongezea hadhi jimboni hata kuongeza kukubalika na kuaminika zaidi, lakini ni wazi kuwa hatua hiyo huwapa wakati mgumu majimboni.
Tayari kitimtim Same Mashariki kimeanza kwa mwanachama wa CCM na aliyewahi kuwa Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Arusha na Mwandishi wa Habari, Semmy Robson Kiondo, kuelezea waziwazi  nia yake ya kumng’oa Mama Kilango.
Anasema yapo mengine yanayomsukuma kwenda Same Mashariki kuleta mabadiliko ya kifikra kwa wananchi na viongozi ikiwamo kutambua uhalisia wa maana ya mapinduzi.


  Kiondo anayataja mambo ya msingi katika mapinduzi kuwa ni elimu, afya, uchumi, kilimo, Msitu wa Shengena, ulinzi na usalama na miundombinu ya barabara.
“Kinachonisukuma kwenda Same Mashariki ni kuhakikisha madhumuni ya chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kutimiza malengo yanafanikiwa,” anasema Kiondo katika mahojiano na mwandishi wa makala hii.
“Malengo ya mapinduzi hayajatimia, angalia sekondari za kidato cha tano na sita kwa Same Mashariki, zipo ngapi? hakuna hata moja.


“Katika mapinduzi, tunaamini kwa watu wa chini, watu wa kawaida waweze kujikwamua. Tuna Shule ya Parane na Suji zinamilikiwa na Kanisa la Sabato,” anasema Kiondo.
Anasema ili mapinduzi ya kielimu yafikiwe Jimbo la Same Mashariki lenye Kata 14, ipo haja ya kutengeneza mfumo utakaowezesha kuwapo shule moja au mbili za kidato cha tano na sita.
Anasema malengo hayo yatawezesha watoto wanaomaliza kidato cha nne kuendelea na kidato cha tano, badala ya kumaliza kidato cha nne na kukosa nafasi.


 “Arusha kuna Sekondari ya Baraa, ile ina kidato cha tano hadi sita, tunajiuliza kwanini Same Mashariki hatufanyi hivyo?” Anahoji Kiondo na kuongeza:
“Tatizo ni uongozi, mbunge kweli yupo,  lakini ana mtizamo kwa mambo haya? Kwa sababu unapozungumzia mapinduzi lazima uwe na mtizamo wa maono yanayokuonesha unakwenda wapi, mimi nina mtizamo na maono ambayo muda ukifika nitayaeleza kwa wananchi na wapiga kura,” anasema Kiondo.
Akizungumzia suala la mapinduzi katika sekta ya afya anasema mwananchi wa aliyepo Same Mashariki akiugua husafiri kwenda Same mjini.


  Anasema kipo kituo cha afya Mamba Miamba cha miaka mingi kilichopaswa kupewa hadhi. Lakini asilimia kubwa ya wagonjwa hukimbilia Hospitali ya Roma inayomilikiwa na kanisa Katoliki .
“Tunafanya nini? Ndugu zangu tunatakiwa kufanya mapinduzi katika afya, nimejiandaa kwa mapinduzi vizuri kabisa,” anasema Kiondo.


Anasema ili kukamilisha malengo ya mapinduzi ni vyema kushirikisha watu kutokana na kuwa na ufahamu na ndoto katika sekta hizo zinazowagusa mmoja mmoja.
“Hivi tunatumia majimbo haya kama mradi? Hapana, naamini kuwa mbunge ni kuleta chachu ya maendeleo kwa waliokuchagua wakiamini utawafikisha mahali,” anasema Kiondo na kuongeza: “Msimamo wangu ni kusimama katika mapinduzi kwani wapo viongozi wengine hawana mapinduzi hata ya kiakili. Lakini pia wabunge wasitumie majimbo kama ajira za kudumu.”


Akifafanua maendeleo yayofikiwa katika miaka 10, Kiondo anasema ni kidogo sana ukilinganisha na muda wa kiongozi kuwatumikia wananchi.
“Huwezi kukaa miaka 10 ukakwangua barabara ya vumbi bila kuweka lami, kiongozi  tuliyemchagua ameanzisha kiwanda cha tangawizi, tujiulize leo kimewaletea nini wananchi.
  “Mimi ni mkulima, hakuna kitu pale. Ukweli ni kwamba mbunge ameanzisha kiwanda na wakulima wakauzia mazao yao pale  mwisho wa siku,  wametapeliwa hakuna aliyelipwa.


“Tukimuuliza anasema ulikuwa ni ushirika, hahusiki, hajawahi kununua tangawizi, hiyo ni kauli ya kuwajibu wananchi?  Nikiwa mbunge nasema sihitaji kujenga kiwanda cha tangawizi, cha nini, huo ni wizi mtupu.
“Mapinduzi yetu ni kutengeneza soko huria au mnada wa wazi  utakaowawezesha wananchi kuuza tangawizi kwa bei wanayoitaka. Tumeona korosho, mahindi na tumbaku wakulima wanavyolia,” anasema Kiondo.
Anasema jambo muhimu ni kutengeneza mnada huo wa wazi  utakaomuwezesha mkulima kuuza tangawizi yake na akiona soko halijamridhisha atarudisha nyumbani.


“Tumedanganywa kwamba tangawizi imesagwa, sijui wamekula, mara viongozi wanasema imeharibika basi tuipime tena kama itakuwa sawa na ile ya awali?” anahoji na kuongeza:
  “Mapinduzi kwenye zao la tangawizi ni kutafuta masoko kisha kuuza kwa mnada utakaopangwa. Hii itabadilisha zaidi kwa sababu ipo wazi, mkulima halazimishwi kuuza,” anasema Kiondo.


  Kiondo, mmoja wa wasiasa vijana, tena machachari, anasema malengo yaliyopangwa kuwasaidia wakulima wa tangawizi hayajafikiwa kutokana na tangawizi kuliwa na wachache.
  “Wana-Same Mashariki tunaoishi Arusha kutokana na majukumu ya kikazi, tulichanga Sh. milioni 11 kwa ajili ya kiwanda, Rais Kikwete alikuwa mgeni rasmi wa kupokea fedha za kiwanda Sh. milioni 300. Nikiwa Katibu wa kamati ya harambee  nilipeleka fedha Dar es Salaam  nikapewa cheti kwa jitihada tulizofanya, kwa hiyo katika kuchangia maendeleo ya Same nipo. Lakini mashaka yetu ni kwamba uwekezaji uliofanyika haulingani na fedha zilizochangwa, ni kama Rais alitumika kupata fedha ambazo hatujui zilifanyiwa nini,” anasema.


“Kiwanda kile sasa ni cha mabwanyenye, hakisaidii wakulima badala yake kimewapa umaskini na wamerudi nyuma kimaendeleo  kwani mkulima alipeleka kilo zote kwa ahadi ya bei ya juu Sh. 2,000 wakati huo kilo Sh. 1300, leo hata ya chini hakuna,” anasema Kiondo.
  Anasema akifanikiwa kuwa mbunge atahakikisha wote walioshiriki kuwaletea umaskini wananchi wanafikishwa katika mkondo wa sheria.  
  “Nitahakikisha waliokula tangawizi ya watu wanafikishwa mahakamani, wajiandae kujibu tuhuma hasa wizi wa tangawizi,” anasema Kiondo.  


 Kiondo analiangalia pia suala la Msitu wa Shengena kama dhahabu ya Same Mashariki isiyowanufaisha wananchi wake, kutokana na kuzuiliwa kuvuna miti.
Anasema endapo atafanikiwa anahakikisha anashawishi wataalamu na serikali ili kuona ni kwa namna gani wananchi wanaweza kuanza kuvuna miti kwa njia inayostahili kitaalamu.
“Misitu ulivunwa zamani, hatuwezi kulinda kitu kisicho na maslahi. Nia yangu ni watu na serikali wanufaike.Ile ni dhahabu ya upareni, nitapambana tuvune miti mikubwa badala ya kuanguka yenyewe.


Akiwa amejitokeza kupitia CCM anasema, yeye ni mwanapinduzi hivyo anataka viongozi wengine ndani ya chama kubadilika kutokana na ukweli kwamba majimbo ya wapinzani yapo tofauti na ya CCM.
“Tofauti yetu ni mapinduzi ya kifikra, lisilowezekana linawezekana. Ndani ya CCM sehemu kubwa ya viongozi wamejichukulia kuwa wao sasa ni miungu-watu, tofauti na wenzetu wapinzani “.
“Eti tunajiona tuna Serikali, wakuu wa wilaya, Afisa Mtendaji, badala ya kufanya tunasema atafanya Afisa Mtendaji au Katibu Tarafa, hili ni kosa. Tunachotakiwa kwa sasa ni kuushtua na kuurekebisha  mfumo uliopo,” anasema.


Akijibu kuhusu endapo jina lake litakatwa anasema; “Mimi ni mwanasiasa, nina uzoefu na siasa, sioni litakatiwa wapi na sioni wapi ntashindwa kupata kura. Nina uhakika najua ushindani upo hata Biblia imesema watakaouona na kuurithi ufalme wa Mungu ni wale wenye nguvu sio goigoi, nina nguvu na wanamapinduzi wenzangu wa Same wameniomba kwenda kugombea na kufanya haya. Hivyo sioni nitashindiwa wapi, najua tutaenda kwenye kura za maoni. Labda rushwa itumike, lakini naamini vyombo  vya serikali vipo vitaona na utaratibu utafuatwa,” anasema Kiondo.
Hata hivyo, anatoa tahadhari kwa viongozi ndani ya chama kuacha mizengwe kwa sababu tu ya kupewa fedha kidogo na badala yake wanapaswa kuangalia wananchi wanahitaji nini.


“Najua viongozi waliopo hawajaleta maendeleo kwa namna ambavyo wananchi walihitaji, ila kwa vile wana watu ndani ya chama na ndani ya mfumo mzima wa chama.
“Watu hawa wapo kwenye malipo (payroll) za kuhongwa, kupewa rushwa, posho au takrima vyovyote, za viongozi. Kwa hiyo wazo jipya linapokuja huonekana kama mchawi kaingia.
“Wana wa Israel walipoambiwa waende nchi ya ahadi, walisema aaa huyu Musa, pamoja na ishara zote walikuwa na shaka. Mimi ni Musa wa Same Mashariki nataka niwapeleke nchi ya ahadi ya asali na maziwa,” anasema Kiondo.

2160 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!