shukuru kawambwa 222Kama ilivyoripotiwa katika toleo lililopita kwamba umbali mrefu kati ya shule za sekondari za kata na makazi ya wanafunzi, unachangia kwa kiasi kikubwa ‘anguko’ la wanafunzi katika matokeo ya mwisho ya wahitimu wa kidato cha nne kila mwaka.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa muda wa miezi mitano umebaini kuwa ufaulu hafifu wa wanafunzi hao husababishwa na umbali mrefu uliopo kati ya shule na makazi ya wanafunzi.


Kadhalika, sababu nyingine ni uteuzi holela wa wanafunzi wa mijini wanaojiunga na shule za sekondari za kata. JAMHURI ilifika katika shule ya sekondari Kiloka na kumtafuta Mkuu wa Shule hiyo, Anna Mbaga. Hata hivyo, Kaimu Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Frank Bankwistu, akasema kwamba bosi wake yuko likizo ya uzazi, lakini shuleni kwake kuna ufaulu haba.


Akizungumzia changamoto zinazosababisha ufaulu hafifu, Mwalimu Bankwistu anasema changamoto ni nyingi hasa katika shule yao, na changamoto hizo zinawaathiri zaidi wasichana kuliko wavulana.


Anasema kwamba wanaoacha masomo hapo Kiloka kutokana na changamoto mbalimbali ni wengi. Kwa mwaka 2013 wanafunzi walioacha masomo wanafikia 33. Idadi hii inajumuisha na wale waliopata mimba.
Bankwistu anasema kuwa ufaulu hafifu unaitesa Kiloka kwani mwaka 2013 wanafunzi 44, kati ya 62 walipata sifuri na zaidi ya hapo hawakuwa na wanafunzi waliopata daraja la kwanza wala la pili.


Anasema kwamba kutokana na wanafunzi wengi kutoka mbali ya maeneo wanaoishi na shule, walianzisha kambi shuleni kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha nne.
  “Madhumuni yalikuwa kupandisha ufaulu. Hata hivyo, hilo nalo lilikabiliwa na changamoto. Tukaamua tena, kambi hizi ni maalum kwa wanafunzi wa kike tu,” anasema Mwalimu Bankwistu.


  “Tulilazimika kufanya hivi kutokana na wasichana waliokuwa wakipangiwa vyumba karibu na shule kujiingiza katika tabia hatarishi. Wanafanywa wake za vijana na wanaume waishio mitaani.
  Hali hiyo inasababishwa na wazazi wengi kushindwa kugharamia gharama za wanafunzi. Kuna wazazi waliokuwa wakiwapa watoto wao Sh. 2,000 kwa mwezi kama gharama ya kujikimu.


“Sasa hapo ndugu mwandishi unatarajia nini kitafanyika kwa mwanafunzi huyo? Wa kiume uamuzi uliotolewa ni kuwa wanatakiwa waishi makwao,” anaeleza Mwalimu Bankwistu.
Anaendelea kusema, “Kwa ujumla kutokana mazingira magumu yaliyopo hapa shuleni wanafunzi wengi hawafurahii kuwapo hapa shuleni. Wanatoka mbali, hapa shuleni maji ni shida. Tunalazimika mara kwa mara kuteua darasa kwenda kuchota maji. Nako wanakofuata maji ni mbali. Kisima unachokiona hapo kinajengwa kwa msaada wa Benki ya Dunia. Bado hakijakamilika.


Hali iliyoko katika Shule ya Sekondari Kiloka ndiyo iliyoko karibu kwenye shule zote za sekondari za kata Tanzania. Yawezekana katika shule nyingine adha hizi zikawa zaidi ama pungufu.
Uthibitisho wa hili ni ufaulu hafifu uliopo katika shule hizo. Serikali nayo imethibitisha hili kupitia Tamko la Sera mpya ya elimu ya 2014.


“Matokeo katika mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne yamekuwa yakishuka kutoka asilimia 54 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 31 mwaka 2012 kwa upande wa elimu ya msingi; na asilimia 90 mwaka 2007 hadi asilimia 43 mwaka 2012 kwa elimu ya sekondari, wakati idadi ya watahiniwa inaongezeka mwaka hadi mwaka,” inasema ripoti inayozalisha sera hiyo.


Esther Thomas Kizenga, mkazi wa Manispaa ya Morogoro Mjini, ambaye ni mama mzazi wa Edward Constantine, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Mgulasi iliyo katika Manispaa ya Morogoro, anasema; “Mimi ni mkazi wa Mji Mpya. Mwanangu amechaguliwa kwenda kusoma Shule ya Sekondari Mgulasi iliyoko Chamwino. Kutoka Mji Mpya hadi Chamwino ni zaidi ya kilimita 10. Wakati mwingine mwanangu analazimika kutembea kwa miguu kutokana na hali ngumu ya maisha tuliyonayo.”


Twaha Ally, mkazi wa Mtaa wa Sadani katika Manispaa ya Morogoro, analalamikia mwanaye Abdul Twaha kuchaguliwa katika Shule ya Sekondari Mwembesongo. Twaha anasema, umbali kati ya Sadani na Mwembesongo ni mrefu.
“Mwanangu analazimika kupanda magari mawili kwenda, mawili kurudi. Hii ni gharama kubwa hususani kwa watu wa kipato cha chini kama sisi. Wakati angechaguliwa kwenda hapa katika Shule ya Sekondari ya Morogoro nisingekabiliwa na gharama hizi. Hata mtoto naye asingekabiliwa na changamoto zinazomkabili.”
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwenye Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 imeeleza kuwa mwenye jukumu la usimamizi wa utekelezaji wa Sera ya Elimu katika ngazi ya mkoa ni la Afisa Elimu Mkoa.  


Mwandishi wa habari hii alifika katika Afisi za Ofisa Elimu Mkoa wa Morogoro, Waliombora Nkya, kuzungumza naye kuhusiana na hali ya elimu ilivyo katika mkoa huo.
Baada ya kupewa hali ya elimu mkoani kwake, Nkya mara moja anang’aka akihoji, “Nani kakwambia hapa Morogoro kuna ufaulu hafifu? Kwanza masuala ya ufaulu nenda kawaulize Maafisa Elimu Sekondari Wilaya ama kawahoji Wakurugenzi wa Wilaya, siyo mimi.”
Anaongeza; “Kama unataka kunihoji kuhusu masuala ya elimu ya sekondari uje na kibali kinachokuruhusu kupata taarifa unazohitaji kutoka kwangu.”


JAMHURI ilifika katika Afisi za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini. Afisi hizo zimo katika Manispaa ya Morogoro Mjini na kuzungumza na Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri hiyo, Mwalimu Salome Mwitumba, ambaye amesema, “Ufaulu hafifu unaweza kuwa unasababishwa na sababu nyingi ikiwamo hiyo ya umbali.”
Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni akiwa afisini kwake jijini Dar es Salaam, Afisa Utafiti na Takwimu wa shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu, Flunge Lyelu, amesema, “HakiElimu haina matokeo ya utafiti ambao ni mahususi kwa ufaulu tu wa shule za sekondari za kata. Ila ina matokeo ya tafiti nyingi zilizofanywa zinazoihusu elimu ya Tanzania.”


Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa wakati shule kadhaa za kata zikiwa zimezungukwa na matatizo lukuki mithili ya visiwa vilivyozungukwa na maji ya ziwa ama bahari, Serikali kwa miaka minne mfululizo imeshindwa kutumia zaidi ya shilingi bilioni 190 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya maendeleo.
Kutotumika kwa pesa hizo kunathibitishwa na matokeo ya utafiti wa HakiElimu uliochapishwa kwenye chapisho la ‘Je, Bajeti ya Elimu inalenga kutatua Changamoto za Elimu’?
“Kwa miaka minne mfululizo kuanzia mwaka 2009 hadi 2013, zaidi ya bilioni 190 zilizotengwa na Serikali kwa matumizi ya utekelezaji wa bajeti ya maendeleo ya Serikali lakini hazikutumika,” imeelezwa.


Inasema kama pesa hizo zingetumika, zingefuta tatizo la maji linalozikabili shule nyingi za kata. Inasema wakati wa masomo wanafunzi wasingeendelea kusomba maji. Wangeweza kukaa darasani kujifunza.


Inafafanua; “Ufaulu wao nao ungepanda na kuwaondoa katika fedheha ya kushindwa kila mwaka. Ikumbukwe kuwa maji ni moja kati ya mahitaji muhimu kwa maisha ya binadamu.”
Katika matokeo ya utafiti mwingine wa Desemba 2013 imeelezwa kinagaubaga kuwa matokeo ya mitihani ya wanafunzi kwa kiasi kikubwa yanategemea aina ya shule anayotoka.


  Taarifa imefafanua kuwa hali ya ufaulu kwa mwaka 2013 ni asilimia 65.5 ya wanafunzi waliohitimu katika shule za sekondari za kata waliopata ufaulu hafifu. Anasema kwamba asilimia 33 ya wanafunzi wa shule nyingine zinamilikiwa na Serikali, ilipata ufaulu hafifu. Shule zisizomilikiwa na Serikali zenyewe ni asilimia 15.6 pekee ndiyo iliyofanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka huo.


Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kupitia chapisho la Wizara hiyo la Basic Education Statistics in Tanzania (BEST) 2009-2013 National Data, zimeainisha ufaulu ulivyo kuanzia 2009 hadi 2013.
Imeweka wazi idadi ya shule za sekondari zinazomilikiwa na Serikali. Shule za kata ni 3,121. Zile zinazomilikiwa na Serikali kuu ni 375. Jumla ya shule zote za Serikali ni 3,496.


  Wizara imeeleza kuwa mwaka 2012 asilimia 32.8 ya wanafunzi wa kiume walio kidato cha pili waliacha shule. Vile vile, asilimia 33 ya wanafunzi wa kike walio kidato hicho hicho waliacha shule mwaka huo. Hizo ni takwimu zinazoonesha asilimia ya wanaoacha shule wakiwa kidato cha pili. Kuna taarifa za wanaoacha shule kwa kila kidato. Kuanzia cha kwanza hadi cha sita.


Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema, “Kwa mwaka huo huo wa 2012 pekee, jumla ya wanafunzi wote waliotahiniwa walikuwa ni 397,222. Idadi hii inajumlisha wanafunzi wote — wa shule za binafsi, Serikali kuu na za kata. Katika matokeo ya mwaka huo asilimia 0.9 walipata daraja la kwanza. Asilimia 2.8 walipata daraja la pili, asilimia 5.9 walipata daraja la tatu, asilimia 33.5 walipata daraja la nne na asilimia 56 waliambulia sifuri.”


  Ripoti ya jumla ya Ukaguzi wa Ufanisi na Ukaguzi Maalum kwa kipindi kinachoishia tarehe 31 Machi, 2014 uliofanywa na Afisi ya Taifa ya Ukaguzi, imeonesha kuwa mamlaka zenya jukumu la kusimamia mazingira hatarishi yanayowakabili watoto ni dhaifu.
  Watoto wanaokabiliwa na mazingira hatarishi ni pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari za kata walio chini ya umri wa miaka 18. Ripoti hiyo imesainiwa na aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh.
 Matokeo ya ripoti yameeleza kuwa Mifumo ya Serikali ya Utambuzi wa Watoto Waishio Kwenye Mazingira Hatarishi ni dhaifu, haifanyi kazi vizuri na kwenye Halmashauri nyingine mifumo hii ni mfu.


Wakati wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule za kata nchini wanabebeshwa mizigo ya michango hadi michango ya kuilinda shule, bado shule hizo pia hazina miundombinu inayofaa.
Nyingi hazina huduma muhimu za kibinadamu, Ripoti nyingine iliyotolea hivi karibuni na Afisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa Wananchi (2012/2013) inasema kuna Halmashauri ambazo hazikusanyi mapato, inasema.


 “Mapato ambayo hayakukusanywa ni zaidi ya shilingi bilioni 7. Halmashauri zilizobainika kutokusanya mapato ni nyingi.  Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa iliyopo mkoani Morogoro nayo ikiwamo. Kilosa haijakusanya mapato ya shilingi milioni 845.8,” inasema.
  Inasema kwamba fedha hizo zingetosha kupunguza adha zilizopo kwenye shule za kata. Angalau, zingetumika kuboresha madarasa na kuweka huduma za maji katika shule hizi.


Ripoti hiyo inaeleza zaidi kuwa kuna Halmashauri 31 ambazo zimekusanya mapato ila hayakupelekwa benki. Mapato ambayo yalikusanywa na hayakupelekwa benki ni Sh. milioni 585.5
JAMHURI limebaini hali zilivyo kwenye shule za kata na zinavyowaweka hatarini wanafunzi  wa shule hizo hususani wasichana.


Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inatoa muongozo wa usimamizi na utoaji wa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu kama haya ya shule za kata. Sheria hii inazitaka Serikali Kuu na Serikali za Mitaa kuhakikisha kuna mfumo imara wa kutoa huduma kwa watoto walio kwenye mazingira magumu.
Sheria Namba 7 ya mwaka 1982 inazitaka Serikali za Mtaa kuratibu utekelezaji wa utoaji wa huduma za msingi kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi katika maeneo yao.


Nayo Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 1996 imeainisha haki za msingi za mtoto. Miongoni mwa haki zilizoainishwa kwenye sera ni haki ya kuishi, haki ya ulinzi na usalama na haki ya kupata maendeleo.
Maendeleo ya watoto wa kike wasomao shule za kata yanakwamishwa kwa kutwishwa mimba wakiwa katika harakati za kusaka elimu kama walivyoeleza walimu, wazazi na walezi waliozungumza na JAMHURI.


Uchunguzi huu umebaini kuwa kama Serikali haitachukua hatua za haraka kutatua matatizo haya, kuna hatari ya hali ya elimu kwa shule za kata kuendelea kudidimia, mipango ya elimu nayo kukwama na hata Dira ya Maendeleo ya Taifa kutofikiwa ifikapo 2025.
 
Uchunguzi huu umefanywa kwa udhamini wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF)

By Jamhuri